Arsenal, Aston Villa mguu mmoja robo fainali UEFA

Arsenal imetanguliza mguu moja katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 7-1 ugenini dhidi ya PSV Eindhoven jana, Machi 4, 2025.

Nahodha wa Arsenal, Martin Odegaard ameongoza kipigo hicho kizito ambacho Arsenal imekitoa katika Uwanja wa Phillips baada ya kuhusika na mabao matatu kwenye mechi hiyo, akifunga mawili na kupiga pasi moja ya mwisho.

Mabao mengine matano katika mechi hiyo ambayo Arsenal ilitawala kwa muda mrefu yamefungwa na Jurrien Timber, Ethan Nwaneri, Riccardo Calafiori, Mikel Merino na Leandro Trossard.

Bao la kufutia machozi la PSV limefungwa na Noa Lang kwa mkwaju wa penalti.

Ushindi huo umeifanya Arsenal kuweka rekodi ya kuwa iliyofunga idadi kubwa ya mabao ugenini katika hatua ya mtoano.

Bao moja alilofunga kinda Ethan Nwaneri limemfanya awe mchezaji wa tatu mwenye umri mdogo zaidi kufunga bao katika mechi ya hatua ya mtoano kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya  baada ya Bojan kufanya hivyo Aprili 2008 akiwa na miaka 17 na siku  217 pamoja na na Jude Bellingham ambaye Aprili 2021 alitikisa nyavu akiwa na miaka 17 na siku 289.

Katika Uwanja wa Santiago Bernabéu, wenyeji Real Madrid wamejiweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya robo fainali baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya watani wao wa jadi, Atletico Madrid.

Ushindi huo wa Real Madrid jana umetokana na mabao yaliyofungwa na Rodrygo na Brahim Diaz huku lile la Atletico Madrid likiwekwa kimiana na Julian Alvarez.

Jijini Brugge, Ubelgiji, Aston Villa imetamba ugenini katika Uwanja wa Jan Breydelstadion baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Club Brugge.

Wafungaji wa Aston Villa jana ni Leon Bailey na Marco Asensio huku lingine moja likiwa la kujifunga la Brandon Mechele huku lile la Club Brugge likipachikwa na Maxim De Cuyper.

Borussia Dortmund imelazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani na Lille ambapo bao lake limewekwa kimiani na Karim Adeyemi na la wageni likifungwa na Hákon Haraldsson.