
Brazil imemfukuza kocha mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo ‘Selecao’, Dorival Junior siku mbili baada ya kupokea kichapo cha mabao 4-1 kutoka kwa Argentina.
Matokeo hayo yameifanya Brazil kuwa katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 kupitia kanda ya Amerika Kusini (Conmebol) jambo ambalo limeonekana kutowafurahisha viongozi wa Shirikisho la Soka nchini humo (CBF).
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 62, ameiongoza Brazil kwa muda wa mwaka mmoja na miezi miwili tangu alipopewa jukumu la kuinoa timu hiyo Januari mwaka jana.
Taarifa fupi ya CBF imeeleza kuwa kwa sasa shirikisho hilo linamsaka kocha wa kuchukua nafasi ya Dorival baada ya kocha huyo kutimuliwa.
“Bodi inamtakia mafanikio katika maendeleo ya kazi yake. Kuanzia sasa, CBF itafanya kazi ya kutafuta mbadala wake,” imefafanua taarifa hiyo.
Dorival hakuwahi kuichezea timu ya taifa ya Brazil wakati alipokuwa mchezaji lakini mafanikio aliyoyapata akiwa kocha wa Flamengo yalilikosha shirikisho la soka nchini humo ambalo lilishawishika kumpa ajira ya kuinoa timu yao ya taifa.
Kocha huyo mwaka 2022 aliiongoza Flamengo kutwaa ubingwa wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Amerika Kusini ‘Copa Libertadores’ ambalo kabla ya hapo ililichukua 2019.
Taarifa kutoka vyombo mbalimbali vya habari Brazil zinaripoti kwamba kocha anayepewa nafasi kubwa kurithi mikoba ya Dorival ni Jorge Jesus ambaye kwa sasa anainoa Al Hilal ya Saudi Arabia.
Mpango wa muda mrefu wa Brazil ulikuwa ni kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti lakini haukutimia ndipo ikaangukia kwa Dorival.