Argentina yafunga hesabu ikiidhalilisha Brazil bila Messi

Argentina imekuwa timu ya kwanza kutoka kanda ya soka ya Amerika Kusini kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-1 nyumbani dhidi ya Brazil  usiku wa kuamkia leo, Jumatano, Machi 26.

Jambo tamu zaidi katika ushindi huo mnono wa Argentina ni kuivuruga Brazil bila uwepo wa nahodha na mchezaji wake tegemeo Lionel Messi ambaye kwa sasa anauguza majeraha ya nyonga aliyoyapata Machi 18 mwaka huu.

Katika mchezo huo, mabao manne ya Argentina yalipachikwa na Julian Alvarez, Enzo Fernandez, Alexis Mac Allister na  Giuliano Simeone huku lile la Brazil likifungwa na Matheus Cunha.

Ushindi huo umeifanya Argentina kufikisha pointi 31 ambazo zimeihakikishia kumaliza katika nafasi sita za juu kwenye msimamo wa mashindano ya kufuzu Kombe la Dunia kupitia kanda ya soka ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Amerika Kusini (Conmebol) na hivyo kuwa timu ya kwanza kutoka huko kufuzu Kombe la Dunia.

Argentina inakuwa timu ya saba ya taifa kufuzu Fainali za Kombe la Dunia ikiungana na wenyeji Mexico, USA na Canada huku nyingine zikiwa ni Iran, Japana na New Zealand.

Brazil bado sana

Kichapo kutoka kwa Argentina kinamaanisha kuwa matumaini ya Brazil kufuzu Kombe la Dunia yamehamia katika mechi nne ilizobakiza kwenye mashindano hayo ya kufuzu ambazo itacheza dhidi ya Ecuador, Paraguay, Chile na Bolivia.

Kwa sasa, Brazil ina pointi 21 na inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa kanda ya Conmebol hivyo inahitaji pointi sita tu ili ijihakikishie kwenda Marekani, Canada na Mexico pasipo kutegemea matokeo ya timu nyingine yoyote.

Nahodha wa Brazil, Marquinhos ameomba radhi mashabiki wa soka wa nchi yake huku akikiri kwamba wamestahili kupoteza mchezo huo.

“Tulichokifanya hapa hakiwezi kutokea tena. Ni ngumu kuzungumzia hiki kwa joto ambalo lipo kwa wakati huu. Kinavuruga.

“Tulianza mechi vibaya mbali ya sana ya kile tlichotakiwa kufanya na wao (Argentina) wapo katika muendelezo mzuri wa hali ya kujiamini. Wanajua jinsi ya kucheza kwa akili na tunawaomba radhi mashabiki wetu,” amesema Marquinhos.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *