
Rais wa Argentina Javier Milei ametangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa baada ya mafuriko kuua takriban watu 16 nchini humo, ofisi yake imetangaza siku ya Jumapili, Machi 9. “Sekta zote za serikali ya zitaendelea kujitolea […] kusaidia waathiriwa katika wakati huu mgumu kwa Waajentina wote,” ofisi ya rais imeandika katika taarifa.
Imechapishwa:
Dakika 3
Matangazo ya kibiashara
Takriban watu 16 wamefariki na wengine kadhaa kutoweka katika mji wa bandari wa Bahia Blanca, Argentina, kutokana na mafuriko ya ghafla na makali yaliyosababishwa na dhoruba siku ya Ijumaa, mamlaka imetangaza jioni ya Jumapili, Machi 9.
Mafuriko hayo yalisababisha uharibifu wa takriban unaokadiriwa kuwa sawa na euro milioni 370, ametangaza meya wa jiji hilo, Federico Susbielles.
Ripoti 100 za watu waliotoweka
Mamlaka za eneo hilo pia zimepokea ripoti zaidi ya 100 za watu waliotoweka kufuatia kimbunga kilichopiga mji huo, kunakopatikana moja ya bandari kuu za Argentina, kilomita 600 kusini mwa Buenos Aires.
Wasichana wawili wametoweka baada ya kusombwa na maji katika muda wa sekunde chache na kuongezeka kwa ghafla kwa kina cha maji, janga ambalo limeshangaza raia wengi wa Argentina.
Mama mmoja alikuwa akijaribu kuwahamisha watoto hao wenye umri wa mwaka mmoja na mitano kutoka kwenye gari lake hadi kwenye gari lililokuwa likiendeshwa na mwanamume aliyekuwa akiwasaidia, ndipo maji yalipowasomba kwa umbali wa mita 350.
Gari hilo liliposimama, binti mkubwa na mama, akiwa na mdogo zaidi mikononi mwake, walipanda juu ya paa ili kujificha. Lakini wimbi jingine liliwasomba kwa sekunde kadhaa.
Mama huyo aliweza kuokolewa baada ya kuburuzwa takriban mita 1,200, lakini wasichana hao wawili wametoweka. Zoezi la kutafuta miili ya watoto hao linaloendeshwa na wapiga mbizi na uwezo mwiingine wa majini, lnaendelea katika eneo jirani, ambalo bado limefunikwa na zaidi ya mita moja ya maji, waziri wa usalama wa jimbo hilo, Javier Alonso, amekiambia kituo cha redio cha eneo la Radio Mitre.
Takriban euro milioni 370 kujenga upya Bahia
Baadaye alasiri, Javier Alonso amethibitisha kuwa mwili wa mwanamume aliyejaribu kumsaidia mwanamke huyo na binti zake wawili ulipatikana.
“Wengi wa waliofariki ni (…) wazee wenye umri mkubwa ambao walikuwa katika nyumba za kustaafu au katika nyumba zinazotunza wazee,” Federico Susbielles amesema katika mkutano na waandishi wa habari.
Kumi na mmoja kati yao tayari wametambuliwa na manispaa ya jiji inasema kuna uwezekano wa miili mingine kupatikana katika jiji hili lenye wakaazi 350,000.
Ujenzi mpya wa Bahia Blanca utagharimu “pesos bilioni 400”, au karibu euro milioni 370, meya wa jiji hilo amebainisha. “Tunahitaji msaada zaidi kuliko hapo awali.”
Mvua ilianza Ijumaa asubuhi na kuisha alasiri. Lakini jiji lilipokea milimita 400 za maji kwa saa chache, karibu kama vile mvua kawaida hunyesha kwa mwaka mmoja katika eneo hilo.
Mto Maldonado, unaopitia Bahia Blanca, ulipasua kingo zake na vitongoji vyote vilizama, na kuacha paa pekee zikionekana. Idadi ya watu waliohamishwa ilikuwa 960 siku ya Jumapili jioni, kulingana na takwimu rasmi.
“Ilikuwa kama vita”
“Rambirambi zangu kwa familia ambazo zimepoteza wapendwa wao na nguvu nyingi kwa wale wote wanaopitia wakati mgumu,” nyota wa kandanda Lionel Messi ameandika kwenye akaunti yake ya Instagram.
Jiji zima “limeshtuka,” mkurugenzi wa ufundi wa klabu ya soka ya Olimpo de Bahia Blanca, Gaston Lotito, ameiambia redio Dsports.
Maafa haya “ni mfano wa wazi wa mabadiliko ya Tabianchi,” amesema Andrea Dufourg, mkurugenzi wa sera ya mazingira wa mji wa Ituzaingo, karibu na Buenos Aires. “Hatuna budi ila kuandaa miji, kuelimisha wananchi na kuweka mifumo madhubuti ya tahadhari za mapema,” ameongeza.