Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nia ya dhati ya kupanua ushirikiano kati yake na Syria katika nyanja jzote.
Sayyid Abbas Araqchi alieleza haya jana katika kikao na waandishi wa habari akiwa pamoja na Bassam al Sabbagh, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria aliyeko ziarani Tehran.
Araqchi ameeleza kuwa amekuwa na mazungumzo yenye tija na chanya na waziri mwenzake wa Syria kuhusu matukio ya kikanda, Gaza na Lebanon na pia kuhusu uhusiano imara na wa kimkakati wa pande mbili. Amesema kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku zote iko na itaendelea kuwa pamoja na watu na serikali ya Syria.

Araqchi amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono hali ya utulivu na mshikamano wa Syria na kulaani njama zozote zenye lengo la kuvuruga amani nchini humo.
Kwa upande wake, Bassam al Sabbagh Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amesema kushtadi mivutano ya utawala ghasibu wa Israel katika eneo la Asia Magharibi kunakwenda sambamba na mradi wa Marekani na Wazayuni wenye lengo la kulipanga upya eneo la Magharibi mwa Asia.