Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa zama za siasa habithi za kugawa na kutawala za Wazungu katika eneo la Asia Magharibi zimefikia kikomo.
Nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na Umoja wa Ulaya zimetoa taarifa dhidi ya Iran zikiendelea kukariri madai yao yasiyo na msingi kuhusu visiwa vitatu vya Iran vya Tomb Kubwa, Tomb Ndogo na Bu- Musa.

Sayyid Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza leo asubuhi akijibu madai yasiyo na msingi na ya uingiliaji kati ya nchi za Ulaya kuhusu visiwa vitatu vya Iran kwamba visiwa hivyo vitatu yaani Tomb Kubwa, Tomb Ndogo na Bu- Musa siku zote ni milki ya Iran na vitaendelea kuwa hivyo daima.
Ismail Baqaei Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia amelaani vikali kukaririwa madai yasiyo na msingi kuhusu visiwa hivyo vitatu mali ya Iran katika taarifa iliyotolewa mwishoni mwa kikao cha pamoja cha wakuu wa Umoja wa Ulaya na Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi; na kuyataja madai hayo kuwa ni ishara ya wazi ya kutoheshimiwa misingi ya malengo ya Hati ya Umoja wa Mataifa na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na hasa msingi wa kuheshimu mamlaka ya kitaifa ya kujitawala na umoja wa ardhi nzima ya serikali nyingine.
Baqaei amesisitiza pia kuwa visiwa hivyo vitatu ni sehemu muhimu ya ardhi ya Iran na itaendelea kusalia hivyo. Amesema: “Kutumia dhana potofu au kukariri madai ya uwongo na ya upotoshaji kuhusu sehemu hiyo muhimu ya ardhi ya Iran hakubadili chochote kuhusu uhakika wa mambo uliopo.”