Arajiga kuamua Dabi ya Kariakoo, rekodi zake zipo hivi

WAKATI zikisalia siku tatu kabla ya mtanange wa watani wa jadi, Yanga dhidi ya Simba kupigwa, Kamati ya Waamuzi imemteua Ahmed Arajiga kutoka Manyara kuwa mwamuzi wa kati kuamua mchezo huo.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Bara raundi ya 23, utachezwa Jumamosi ya Machi 8, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 1:15 usiku.

Mbali ya Arajiga, mwamuzi msaidizi namba moja ni Mohamed Mkono kutoka Tanga na Kassim Mpanga wa Dar es Salaam akiwa ni mwamuzi msaidizi namba mbili wakati Amina Kyando kutoka Morogoro akiwa ni mwamuzi wa nne (Fourth Official).

Hadi sasa Arajiga ameshachezesha mechi nne za dabi, mbili ligi kuu na nyingine Kombe la Shirikisho (FA), kwenye mechi hizo Yanga imepoteza mara moja na ushindi tatu.

Simba kwenye mechi hizo zilizochezeshwa na Arajiga imepoteza mara tatu na kushinda mchezo mmoja wa fainali ya FA mwaka 2021 uliochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma kupitia bao la Taddeo Lwanga.

REKODI ZA ARAJIGA KARIAKOO DABI

(1)- Simba 1-0 Yanga (Fainali ASFC, Lake Tanganyika, Kigoma, Julai 25, 2021) (Bao la Taddeo Lwanga)

(2)- Yanga 1-0 Simba (Nusu Fainali ASFC, CCM Kirumba, Mwanza, Mei 28, 2022) (Bao la Feisal Salum ‘Fei Toto’)

(3)- Simba 1-5 Yanga (Ligi Kuu Bara, Benjamin Mkapa, Dar, Novemba 5, 2023)

(4)- Yanga 2-1 Simba (Ligi Kuu Bara, Benjamin Mkapa, Dar, Aprili 20, 2024)

(5)- Yanga vs Simba (Ligi Kuu Bara, Benjamin Mkapa, Dar, Machi 8, 2025)