Arajiga kiboko ya Dabi rekodi imesimama

Wahenga walisema ‘chanda chema huvikwa pete’, msemo ambao umejidhihirisha kufuatia uteuzi wa refa Ahmed Arajiga kutoka Manyara kuchezesha mechi ya Yanga na Simba, Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa uliofanywa na Kamati ya Marefa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi (TPLB) jana imeeleza kuwa Arajiga ndiye atakuwa refa wa kati akisaidiwa na Mohammed Mkono, Kassim Mpanga na refa wa nne atakuwa ni Amina Kyando.

HISTORIA TAMU

Hii itakuwa mara ya tano kwa Arajiga kuzichezesha Yanga na Simba ambapo katika mechi nne zilizopita alizoshika filimbi, mbili zilikuwa za Ligi Kuu na nyingine mbili za Kombe la Shirikisho (FA) ambalo zamani ilikuwa likijulikana kama Kombe la Shirikisho la Azam.

Yanga imekuwa na bahati kubwa na refa Arajiga, kwani katika mechi hizo nne za nyuma alizowahi kuichezesha dhidi ya Simba, imeibuka na ushindi mara tatu huku ikipoteza mechi moja, imefunga mabao manane na yenyewe imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu.

Kumbukumbu tamu na ya kipekee ambayo Yanga imekuwa nayo kwa refa Arajiga ni ushindi wa mabao 5-1 ambao iliupata katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita iliyochezwa Novemba 05, 2023.

REKODI IMESIMAMA

Kwa kuteuliwa kuchezesha Dabi ya Kariakoo Jumamosi, Arajiga, Mkono na Mpanga wanaweka rekodi ya kuwa waamuzi watatu waliochezesha mechi nyingi zaidi za Yanga na Simba kuliko wengine.

Waamuzi hao watatu walichezesha mechi baina ya timu Aprili 20, 2024 ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kabla ya hapo walichezesha mechi ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 5-1, Novemba 11, 2023.

HESHIMA KIMATAIFA

Arajiga alipata beji ya uamuzi ya kimataifa ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mwaka 2022 na tangu hapo amejitambulisha kama mwamuzi anayeweza kuzitafasiri na kuzisimamia vyema sheria 17 za mpira za miguu.

Kiwango hicho bora cha Arajiga kimempa fursa ya kuchezesha mechi kadhaa za kimataifa kwa mashindano ya ngazi ya klabu na timu za taifa.

Mechi yake ya kwanza kimataifa ilikuwa ni Septemba 10, 2022 iliyozikutanisha ASAS ya Djibouti na AS Kigali ya Rwanda kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ambayo ilimalizika kwa sare tasa.

Baada ya hapo amechezesha mechi nane za mashindano tofauti ya kimataifa ambazo alitoa idadi ya kadi 11 zote zikiwa za njano.

Kiwango chake kizuri cha uchezeshaji hapana shaka kimelishawishi Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kumteua kuchezesha fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (Chan) zitakazofanyika Agosti mwaka huu ambapo atakuwa na refa msaidizi Frank Komba kuiwakilisha Tanzania.

WASIFU UMENYOOKA

Arajiga alizaliwa mkoani Manyara, Julai 03, 1991 na ana familia yenye mke na watoto watatu.

Kwa misimu miwili mfululizo, Arajiga amefanikiwa kuibuka na tuzo ya refa bora wa Ligi Kuu Tanzania.

Katika msimu huu, refa huyo kwenye Ligi Kuu Bara ametoa kadi 24 ambapo mbili ni nyekundu na 22 za njano huku akitoa penalti tatu.