Arajiga, Kayoko wapigwa msasa wa VAR

WAAMUZI 20 wakiwamo maarufu kama Ahmed Arajiga, Herry Sasii, Ramadhani Kayoko na Tatu Malogo, wanatarajiwa kuingia darasani kuanzia kesho Jumatatu kwa ajili yua kupigwa msasa juu ya teknolojia ya usaidizi kwa waamuzi (VAR).

Kozi hiyo yenye lengo la kuboresha ufanisi wa waamuzi hao itafanyika kwa muda wa siku tano kuanzia kesho Jumatatu hadi Ijumaa ya wiki hii na itafanyikia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kozi hiyo imekuja siku chache kabla ya kupigwa kwa pambano la watani wa jadi wa soka nchini, Simba na Yanga litakalofanyika siku moja baada ya kumalizika kwake.

Kwa mujibu wa orodha iliyotolewa na TFF, washiriki katika kozi hiyo ni Ahmed Aragija, Amina Kyando, Herry Sasii, Tatu Malogo, Nasir Siyah, Mohamed Simba, Ramadhan Kayoko, Alex Pangars, Abdallah Mwinyimkuu, Esther Adabert, Frank Komba, Kassim Seif na Ally Ramadhan.

Wengine ni Hamdani Said, Mohamed Mkono, Janeth Balama, Glory Tesha, Zawadi Yussuph, Siraji Mkwaju na Shaban Mussa.

Hatua hiyo inakuja kufuatia baadhi ya makosa ya waamuzi ambayo msimu huu yameonekana yakijirudia rudia.

Hata hivyo, msimu ulipoanza TFF ilitangaza kutumika kwa vifaa hivyo vya teknolojia kuanza kutumika ikiwemo kuwapitisha brashi waamuzi namna ya kutumia kifaa hivyo.