
Dar es Salaam. Ahmed Arajiga ataandika historia mpya ya kuwa refa pekee aliyewahi kuchezesha mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu za watani wa jadi Yanga na Simba ‘Kariakoo Derby’ baada ya kupangwa kuchezesha mechi baina ya timu hizo, Jumamosi, Machi 08, 2025 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.
Kabla ya mechi hiyo ya Jumamosi, Arajiga ndiye alikuwa refa katika mechi mbili zilizopita za Ligi Kuu baina ya timu hizo mbili ambazo Yanga iliibuka na ushindi mara zote.
Refa huyo kutoka Manyara, alichezesha mechi ya mzunguko wa kwanza ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 5-1 na kisha akachezesha mechi ya mzunguko wa pili ambayo Simba ilipoteza kwa mabao 2-1.
Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania leo, Machi 5, 2025 imemtaja Arajiga kuwa refa wa kati akisaidiwa na Mohamed Mkono wa Tanga, Kassim Mpanga wa Dar es Salaam na mwamuzi wa akiba atakuwa ni Amina Kyando kutoka Morogoro.
Ni mechi inayoashiria hadhi ya nyota tano kwa ligi ya Tanzania kutokana na upangwaji wa maofisa 14 wa kuisimamia wakiwemo Arajiga na marefa wenzake, jambo ambalo ni nadra kuliona katika idadi kubwa ya michezo ya soka nchini.
Ukiondoa marefa hao wanne, kamishna wa mechi amepangwa kuwa Salim Singano na mtathmini wa marefa atakuwa ni Soud Abdi.
Baraka Kizuguto amepangwa kuwa mratibu wa mechi na atasaidiwa na Jonas Kiwia huku ofisa habari wa mchezo akipangwa kuwa Karim Boimanda.
Ofisa protokali wa mechi ni Fatma Abdallah, ofisa masoko akiwa ni Jerry Temu na daktari wa mechi ni Manfred Limbanga.
Ofisa wa ulinzi na usalama kwenye mechi hiyo ni mrakibu msaidizi wa Polisi, Hashim Abdallah na msimamizi wa kituo ni Ramadhan Misiru.
Timu hizo zinakutana huku Yanga ikiwa na kumbukumbu ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza baina yao msimu huu ambalo lilikuwa la kujifunga la beki Kelvin Kijili.
Kwa sasa Yanga inaongoza msimamo wa Ligi ikiwa imekusanya pointi 58 katika mechi 22 huku Simba ikiwa nafasi ya pili na pointi 54 ilizopata katika mechi 21.