
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Abbas Araqchi ametoa mjibizo kwa uamuzi wa Umoja wa Ulaya wa kutaka kuyawekea vikwazo mashirika ya vyombo vya majini ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kueleza kwamba hatua hiyo ya Ulaya haina msingi wowote wa kisheria, kimantiki wala kimaadili.
Umoja wa Ulaya umetangaza kuwa unataka kuyawekea vikwazo mashirika ya vyombo vya majini ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambapo kisingizio kilichotumiwa kwa ajili ya vikwazo hivyo vipya, sawa na kilichotumiwa dhidi ya shirika la ndege la Iran, Iran Air, ni madai ambayo hayajathibitishwa na ya uongo mtupu kwamba Iran imeipatia Russia makombora ya balistiki kwa ajili ya kutumia katika vita vya Ukraine.
Kwa mujibu wa mtandao wa Sahab, Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba: Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amethibitisha binafsi kwamba hakuna makombora ya balistiki ya Iran ambayo yamesafirishwa kupelekwa Russia. Hata hivyo, Umoja wa Ulaya hauko tayari kukomesha ulengaji usio wa haki wa wasafiri wa safari za anga kwa kuyawekea vikwazo mashirika ya ndege ya Iran. Hatua hiyo inavyoonekana, imechukuliwa kwa kutegemea madai ya uongo ya kupelekwa makombora yetu Russia.
Araghchi ameongeza na kusema kuwa: “sasa hivi Umoja wa Ulaya unapanga kutumia kisingizio hichohicho cha uongo cha kusafirisha makombora ili kuyawekea vikwazo mashirika ya meli za Iran. Hakuna msingi wowote wa kisheria, kimantiki, au wa kimaadili wa kuhalalisha mwenendo huu. Kwa kweli, tabia hizi husababisha kutokea kile ambacho Umoja wa Ulaya unataka kukizuia”.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza kuwa: Uhuru wa usafiri wa baharini ni mojawapo ya misingi mikuu ya haki za baharini. Wakati watu wachache wanapolitumia suala hilo kipendeleo, matokeo ya uono wao finyu mara nyingi huwarudia wao wenyewe.