Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, Jamhuri ya Kiislamu haitaki kuzusha mivutano lakini inatambua haki yake ya kujilinda kwa mujibu wa Hati ya Umoja wa Mataifa.
Sayyid Abbas Araghchi ameyasema hayo leo mjini Islamabad katika mkutano na waandishi wa habari, akiwa na mwenzake wa Pakistan Seneta Mohammad Is-haq Dar, ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo na akaongeza kuwa: “khulka ya kishenzi na kinyama ya Wazayuni imeshtadi katika Ukanda wa Ghaza na Lebanon”.
Akishukuru misimamo ya viongozi wa serikali ya Pakistan dhidi ya uchokozi wa utawala wa Kizayuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Tehran inathamini na kupongeza misimamo ya wazi ya Waziri Mkuu wa Pakistan dhidi ya jinai za kichokozi za Israel.
Kwa upande wake, Seneta Muhammad Is-haq Dar, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Pakistan amelaani jinai za kichokozi za utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kutilia mkazo misimamo imara ya Tehran na Islamabad dhidi ya hatua haramu na za uvunjaji wa sheria za Israel katika ardhi inazozikalia kwa mabavu.

Is-haq Dar amelaani pia jinai zinazoendelea kufanywa na utawala huo ghasibu huko Ghaza na athari zake mbaya katika eneo la Magharibi mwa Asia, na akaongeza kuwa: “kwa uchokozi huu, Israel imefanya ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa, Hati ya Umoja wa Mataifa, mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi yote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran”.
Kadhalika, Naibu Waziri Mkuu wa Pakistan ameuelezea ugaidi na misimamo ya kufurutu mpaka kuwa ni tishio kubwa kwa eneo na kikwazo kwa ukuaji na maendeleo ya nchi za eneo hili na akasema: Tehran na Pakistan zimeazimia kwa dhati kushirikiana dhidi ya ugaidi na kupanua ushirikiano wao wa pande mbili.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araghchi aliwasili Islamabad mji mkuu wa Pakistan Jumatatu usiku, kwa lengo la kukutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu wa nchi hiyo kuhusu mahusiano ya pande mbili na kuchunguza matukio yanayojiri katika eneo…/