Araghchi: Bodi ya Magavana ya IAEA inahitaji kupinga azimio la E3 dhidi ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amesema wajumbe wa Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) wanapaswa kupinga jitihada za nchi tatu za Ulaya za kupitisha azimio dhidi ya Tehran.

Araghchi aliyasema hayo katika mazungumzo ya simu na mawaziri wenzake ambao nchi zao ni wajumbe wa Bodi ya Magavana, zikiwemo Brazil, Afrika Kusini, Bangladesh, Algeria, Burkina Faso, Pakistan na Ufaransa.

Siku ya Jumatano, nchi tatu za Ulaya za Ufaransa, Uingereza na Ujerumani ziliwasilisha azimio jipya dhidi ya Iran kwa IAEA kabla ya kufanyika mkutano wa bodi hiyo.

Marekani na waitifaki wake wa Ulaya wamekuwa wakitoa shutuma zisizo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kwamba eti Iran haitoi ushirikiano wa kutosha kwa wakala huo. Madai hayo yanakwenda kinyume na ushirikiano wa Iran na wakala huo wa Umoja wa Mataifa wa nyuklia.

Araghchi amesema Bodi ya Magavana yenye mataifa 35, moja ya vyombo viwili vya kuunda sera za IAEA, haipaswi kuruhusu Troika ya Ulaya kugeuza chombo hicho kuwa jukwaa la kuendeleza maslahi ya kisiasa ya baadhi ya nchi za Magharibi zenye silaha za nyuklia na wafuasi wao.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amebainisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikifuata sera ya ushirikiano na IAEA na akaonya kwamba hatua “zisizo na uhalali” za baadhi ya nchi za Magharibi za kupitisha azimio dhidi ya Iran zinaweza kuvuruga kazi za kiufundi na kitaaluma za wakala huo.

Araghchi amesema hatua “isiyo ya kujenga” ya E3 dhidi ya mpango wa nyuklia wa amani wa Iran itadhoofisha tu mwingiliano kati ya Iran na IAEA.