
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameionya Marekani dhidi ya kuanzisha tena kampeni yake “mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa” dhidi ya Tehran na kusisitiza kwamba majaribio ya hapo awali ya Washington ya kuishinikiza Iran yalishindwa na kugonga mwamba.
Sayyid Abbas Araghchi amesema hayo katika ujumbe aliouandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X na kubaiinisha kwamba: Toleo la kwanza la mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa lilikabiliwa na upinzani wa kiwango cha juu kabisa wa Tehran, na kuifanya Washington ishindwe kwa kiwango cha juu kabisa.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, “toleo la pili la mashinikizo ya kiwango cha juu” litasababisha kutokea “toleo la pili la kushindwa kwa kiwango cha juu” kwa Marekani, na hivyo amewashauri maafisa wa Marekani kutumia wazo la “akili na hekima ya kiwango cha juu kabisa” kwa sababu kuufanya hivyo ni kwa maslahi ya kila mtu.