Arab League: Kunyamazia kimya hali ya Palestina na Lebanon ni sawa na kushiriki katika jinai

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) amesemam kuwa kukaa kimya mkabala wa jinai zinazotekelezwa na utawala wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina na Lebanon ni sawa na kushiriki katika jinai hizo.

Ahmad Abu Gheit amesema hali ya mambo ya Palestina na Lebanon haipasi kunyamaziwa kimya. Katibu Mkuu wa Arab League alieleza haya jana wakati wa ufunguzi wa mkutano wa utangulizi wa viongozi wa nchi za Kiarabu na Kiislamu huko Riyadh, Saudi Arabia. 

Kushtadi jinai za  Israel dhidi ya Gaza 

Ahmad Abu Gheit amesema kusitishwa vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza na Lebanon ni jukumu la wote la kibinadamu, na wakati huo huo ni suala la dharura ya kiusalama na kistratejia ili kuliepusha eneo hili zima kuelekea katika mustakbali usiofahamika. 

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amesisitiza kuunga mkono amani na uthabiti wa wananchi wa Palestina katika ardhi yao na kuunga mkono haki zao. Ahmad Abu Gheit amebainisha kuwa nchi ya Palestina inapaswa kuasisiwa katika ardhi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza na katika mipaka ya mwaka 1967,  mji mkuu wake ukiwa Quds Tukufu.

Mkutano wa viongozi wa nchi za Kiarabu na Kiislamu uliotishwa kwa lengo la kujadili hali ya mambo ya Ukanda wa Gaza na Lebanon unafanyika leo mjini Riyadh, Saudi Arabia.