ANTIE BETTIE: Anatumia tendo la ndoa kuniadhibu

Anti, nimechoshwa na tabia za mke wangu, narudia ni mke wangu wa ndoa na nilimuoa kwa mahari na heshima kubwa ukweni. Lakini hata sielewi ananichukuliaje tu jamani, kila nikikosea au akichukia kwa sababu zake adhabu napewa mimi kwa kunyimwa unyumba.

Hii adhabu ni kali kwangu. Nahitaji huduma ya tendo la ndoa ninapokuwa nina mawazo, sina pesa na lakini navutiwa tu na mke wangu kila ninapomuona, lakini sipati ushirikiano.

Ninamtunza, kadiri anavyokua ndivyo anavyozidi kuwa mrembo na kunichanganya kabisa, lakini hanipi tendo la ndoa ninapolihitaji, mpaka siku anayotaka yeye.

Anti, huwezi kuamini nilioa nikiwa kijana mdogo kwa sababu kuhangaika kutongoza wanawake ni jambo lililonishinda, sasa mke wangu akininyima ina maana nitakaa bila kushiriki hilo tendo hadi atakapoamua kunipa.

Kama kuna mwanamume anajua kumbembeleza apewe tendo la ndoa ingekuwa ni mtihani ningefaulu kwa kiwango kikubwa sana, kwani hiyo kazi ninaifanya kwa mwaka wa 19 sasa. Sijawahi kupewa bila kulalamika, kuomba na kulialia.

Yaani nikifanya kosa lolote la kibinadamu, ninajua nina wiki mbili za kuhukumiwa kwa kunyimwa tendo la ndoa. Hata sijui nifanye nini, naomba unishauri.

Kabla sijaanza kukujibu kwanza nianze na hawa wanawake walioolewa kwa hiari yao lakini wanawafanya watoto wa watu kama watumwa, hivi kuna uhusiano kati ya makosa na kumnyima mumeo unyumba? Nani anawaelekeza huko kwao kabla hawajaingia kwenye ndoa. Hivi viungo vya uzazi vina uhusiano gani na masuala ya kugombana, kwanza ninavyojua tendo la ndoa humaliza ugomvi hata uwe mkubwa kiasi gani. Sijui kuna nini kimeingia kwenye ndoa, walioolewa na wanaume wasiojali kuhusu kupewa huduma hiyo na wake zao wanalalamika, wanaoombwa kwa mashairi na vilio hawataki.

Acha nirudi kwenye msingi wa swali. Nikiri kuwa ninaelewa jinsi hali hii inavyokupa shida na kuathiri maisha yako. Kunyimwa tendo la ndoa kama adhabu ni hali yenye mzigo mzito kwa mwanaume, na ni muhimu kujaribu kuelewa chanzo cha tatizo hili ili uweze kupata suluhu ya kudumu.

Wasiliana na mke wako kwa uaminifu kuhusu jinsi unavyohisi. Ni muhimu kumueleza kwa upole na kwa heshima jinsi unavyohisi kuhusu adhabu hii na jinsi inavyokuthibitishia kuwa unahitaji zaidi ya vile anavyokupa sasa. Wakati wa majadiliano haya, ni muhimu kuepuka kulaumiana na badala yake, jaribu kuelewa mtazamo wake na hisia zake.

Ikiwa majadiliano haya hayakusaidii, unaweza kuzingatia kupata msaada wa mtaalamu wa mahusiano au mshauri wa ndoa. Wataalamu hawa wanaweza kusaidia katika kutatua migogoro, kuboresha mawasiliano, na kutatua matatizo yanayohusiana na mahusiano yenu.

Jaribu kuelewa ikiwa kuna sababu nyingine za kina zinazochangia hali hii. Je, kuna matatizo ya kihisia, kiakili, au kiafya yanayomkabili mke wako? Kutambua chanzo hiki kunaweza kusaidia katika kutafuta suluhu.

Mume wangu amekuwa mkimya mpaka naogopa

Siku za hivi karibuni mume wangu amekuwa mkimya sana, wakija wageni, hususan wa kutoka kwetu hazungumzi kama ilivyokuwa zamani. Wanaweza wakapiga stori tukacheka watu wote tuliokuwa sebuleni kasoro yeye, anapoulizwa jambo lolote anakuwa kama ndiyo kaamshwa usingizini, angalau wakija wageni kutoka kwao anajichanganya kidogo ingawa napo ni kwa shida shida pia.

Hii tabia hakuwa nayo miaka mitano nyuma, imeanza hivi karibuni, sijui ana shida gani, kibaya zaidi kila nikimuuliza anasema yupo sawa.

Ingawa nikiwa naye anakuwa na nafuu tofauti na kukiwa na watu ni kama anahisi kero, kuna baadhi ya ndugu zangu pia wameliona hilo.

Nifanyeje aniambie ana shida gani au unaweza kunisaidia pa kuanzia, maana sifurahishwi na hali hii, ninavyomjua mume wangu ni mkimya, lakini mcheshi hasa kwa wageni.

Mmh! Hapa sidhani kama kuna jibu la moja kwa moja la mume wako kuwa mkimya na kutokuwa na mazungumzo kama ilivyokuwa zamani, kunaweza kuwa na sababu nyingi, na ni muhimu kujua chanzo chake ili kupata suluhu.

Anza kwa kumdodosa mwenyewe kuhusu mabadiliko hayo, bila kumlaumu mueleze kuwa anawashangaza wengi, ikiwamo wewe mwenyewe na inakuumiza.

Zingatia kuweka mbali tuhuma unapomuuliza, itapendeza zaidi ukifanya hivyo siku ambayo amefurahi au umemfanyia kitu anachokipenda, mfano umempikia chakula kizuri akipendacho, umemnunulia zawadi, umefanya jambo lolote analolipenda. Akiwa na furaha anaweza kukueleza kinachomsumbua.

Pia shirikisha wataalamu wa afya ya akili kwa kuwaeleza hali ya mumeo, pia wanaweza kuwa na jambo la kukuambia la kitaalamu zaidi linaloweza kukusaidia. Kwa sababu si rahisi umwambie moja kwa moja mwende kwa hao wataalamu hatakuelewa, lakini ukiwatumia wao itakuwa rahisi.

Pengine ana shida ya kihisia inayomletea hali hiyo ya ukimya.

Pia pima wewe mwenyewe, katika maisha yenu au yake kuna kitu kimebadilika. Mabadiliko mfano sehemu ya kazi, kipato au matatizo ya kifamilia.

Haya mabadiliko kama yapo anaweza kukuambia ni kawaida, lakini kihisia yanamuumiza, hivyo ukibaini unaweza kumkutanisha na wataalamu wa saikolojia kwa ajili ya kumpa ushauri utakaomrudisha tena katika hali ya kawaida.

Au wewe mwenyewe unaweza kufanya kazi hiyo kwa kumtia moyo na kumueleza pamoja na mabadiliko hayo kama baba kwenye familia ana mchango mkubwa kuliko ilivyokuwa awali. Pia ninyi kama familia mnamtegemea bila kujali ana changamoto gani za kimaisha.