
Swali: Habari za kazi. Nina changamoto inayonipa tabu kwa miezi karibu sita sasa. Mume wangu ana changamoto ya ulaji usiokuwa wa kistaarabu. Akitafuna lazima vyakula vya mdomoni vionekane, anaachama mdomo kila anapotafuna kiasi cha kutoa sauti.
Pia akinywa maji, chai lazima avute kwa sauti na apumulie kwenye kikombe au bilauli. Haya mambo yananiudhi sana, ila nashindwa nitamuambiaje.
Jibu: Katika ndoa, kila mtu ana tabia zake ambazo zinaweza kuwa kero kwa wengine, lakini mhusika anaona ni kawaida. Tabia hizi kwa walio wengi zinatokana na malezi waliyolelewa tangu wakiwa wadogo, wazazi au walezi wao hawakuona kama ni tatizo na kulikemea hadi limemea.
Kama hii tabia unayolalamika mumeo anayo ya ulaji wa kutoa sauti anapotafuna au anapokunywa maji, uji n.k wanayo wengi, ila hawajui kama ni tatizo.
Changamoto ni kumwambia mtu mzima kama mumeo anakula vibaya, lazima utafute mbinu sahihi za kumueleza ili asijisikie vibaya, ukizingatia wanaume huwa mara nyingi hawapendi kuambiwa wakiamini wanaongozwa ilhali kiasili wao ni viongozi.
Hivyo kwanza kabisa tafuta wakati wa kumwambia mume wako kuhusu anavyokukera kutokana na ulaji wake, hasa mbele za watu.
Unaweza kumchombeza kwa kumwambia wewe unapenda na huoni shida, ila mbele za watu wanamshangaa, jambo linalokutia aibu.
Usimwambie wakati mmoja wenu akiwa amekasirika, kwani hii inaweza kusababisha mazungumzo kuwa ya kushambuliana na kulaumiana badala ya kuelekezana. Ukizungumza naye mkiwa mmetulia wawili kwenye starehe au mmelala, itasaidia kuelewana.
Wakati wa kumwambia mume wako jinsi unavyohisi, tumia maneno yenye hekima na heshima. Badala ya kumwambia, “Hujui kula, unanifanya nihisi aibu,” unaweza kusema: “Napenda sana tunapokula pamoja, lakini wakati mwingine ninahisi unachanganya mambo unapokunywa maji”.
Ukizungumza hivi ataona hujamlaumu, badala yake unajaribu kurekebisha mambo yawe bora kwenu nyote.
Wakati mwingine mkiwa na furaha mtanie kwa kunywa maji kwa sauti ukivuta na kupumulia kwenye kikombe huku mkicheka. Hii itasaidia kujua zaidi ulichomaanisha anakikosea, hivyo kila akinywa atakumbuka utani huu na kuacha.
Unaweza pia kumwambia mkiwa mnakula akianza kutafuna kwa sauti, “najua mume wangu unafurahia chakula kitamu nilichopika, nami ninafurahi unavyokila kwa bashasha, lakini unavyotafuna na sauti zinatoka napoteza hamu ya kula”.
Hii itakurahisishia kazi ya kumweleza, kwani kila akikumbuka atakuwa anatafuna taratibu.
Unaweza pia kusema huko nyuma hata wewe ulikuwa unakula kama yeye na ilikuwa ni kawaida hadi ulipokwenda mahali, mathalani chuo, jeshini, kwenye kambi fulani, ndipo wenzako walikuambia unakula isivyo sawa ukajitafakari na kubadilika.
Ukijiweka kwenye changamoto atajiona ni sehemu yako na mabadiliko yanahitajika ili apone kama ulivyopona wewe.
Kwa msaada zaidi, kama kuna watoto unaweza kuwaambia: “Ili ukitafua sauti isitoke tafuna chakula ukiwa umefumba mdomo badala ya kuachama”, ukiwaelekeza hivi na yeye akiwa anasikia inaweza kumponya.
Ukitumia mbinu jumuishi ya mimi badala ya wewe inaondoa kulaumiana na inabaki kueleweshana.
Wakati mwingine, mtu anaweza kufanya mambo kwa sababu hajui namna nzuri ya kuyafanya. Toa mapendekezo ya jinsi mambo yanavyoweza kubadilika.
Zingatia ukitumia mbinu zote hizi za kumzunguka na bado asikuelewe, tenga siku ya furaha, mweleze moja kwa moja, kwani kuna wengine ni ngumu kuelewa jambo kwa mafumbo na mizunguko mingi.
Mweleze kuwa mkila pamoja namna anavyotafuna hufurahii kwa sababu nyumbani (mahali popote kwa kadiri unavyoona inafaa), ulielezwa hilo si jambo jema.