ANTI BETTIE: Mama mkwe anatuganda tutoke naye kustarehe

Swali:  Anti nimeolewa lakini ninaishi nyumba moja na familia ya mume wangu, akiwamo mama mkwe.

Kuishi nao siyo shida, kwani maisha ni ya kawaida na mume wangu anajitahidi kutuhudumia na kupunguza makelele mengi. Shida ni mama mkwe, amekuwa akitung’ang’ania na mume wangu tunapotaka kutoka kwa matembezi ya jioni.

Amefanya hivyo zaidi ya mara nne, kiasi kwamba tukitaka kutoka mume wangu anatokea kazini na mimi ninatoka nyumbani mapema, kwani akikuona umevaa kimtoko tu na yeye anang’ang’ania na unakuwa ugomvi kabisa mkimuacha.

Imefikia hatua mwanaye amepunguza kutoka na mimi kwa matembezi ya jioni kama ilivyokuwa zamani kabla hatujaamua kuishi nao baada ya kujenga nyumba inayotutosha sote. Roho inaniuma, kwani ndiyo kwanza ndoa yetu ina miaka mitatu, hatujapata mtoto bado wenyewe tunakula raha, ila mama amekuwa kikwazo. Nifanyeje? Maana hata mume wangu anakosa pozi.

Jibu: ….Kuna watu wanaamini wanawake wanaishi kwa ajili ya watu wengine. Ukiangalia kwa makini utabaini ni kweli kwa sababu wao ni kina mama, wake na walezi wa familia. Lakini pamoja na hayo yote bado kama binadamu wanapaswa kuishi tena maisha wayapendayo, namaanisha yanayowapa amani ya nafsi wanapopata wasaa wa kufanya hivyo.

Eti unashindwa kufanya yale yanayokupa furaha kwa sababu unaishi nyumba moja na mama mkwe, mawifi na shemeji zako, hapana.

Muhimu ni kuwaheshimu, kutimiza wajibu wako kama mke kwanza kwa mumeo kisha kwa familia yake, bila kuwadharau wala kujiona kama wao wanapaswa wakunyenyekee wewe kwa sababu zozote zile. Ila hayo yote yasikunyime fursa ya kuishi, kwa mfano unashindwaje kutoka na mumeo kwa ajili ya matembezi ya jioni au usiku kisha mnaishi na mama mkwe naye atang’ang’ania kutoka na ninyi. Umesema amekuwa akifanya hivyo kiasi kwamba wewe na mumeo mmekubaliana muache kutoka, haipaswi kuwa hivyo kabisa. Mama ana nafasi yake kubwa tu kama mzazi, lakini hapaswi kuwa kikwazo cha nyinyi kuishi kwa furaha katika umri wenu, kwa sababu kuna maeneo mnayotaka kwenda nyinyi yeye hapaswi kwenda, ukizingatia wewe ni mkwewe.

Mwambie mumeo atafute namna ya kumuelewesha mama kuwa mnapotaka kutoka yeye abaki, ila hakikisha siku mambo yakiwa mazuri mnatoka kama familia kwenda ufukweni, kula chakula cha mchana mahali anapopapenda badala ya kuwaganda.

Ukimwambia wewe anaweza asikuelewe sana na akaona unambania kwa mwanaye au unamvunjia heshima, aambiwe na kijana wake kwa lugha ya nidhamu na msisitizo ili aelewe.

Madhara ya kuvilea hivi vitu ni kumchukia mkweo, kwani itafikia hatua utaona anakunyima nafasi ya kufurahi na mumeo nje ya nyumbani na marafiki zenu, ila mkimuelewesha akawaacha mfanye safari zenu, muishi maisha yenu kama mke, mume, rafiki na mpenzi mtaishi naye maisha yote bila kuona kero wala kumchoka.

Pengine mama anashindwa kutofautisha mitoko ya wapendanao na ya familia ndiyo maana anang’ang’ania, akielewa ataacha.

Asipoelewa hapo ndiyo mnapaswa muwashirikishe wakubwa zake au ndugu wengine wa familia na si kufanya anachokitaka.

Ninahofia mtamuona kero hapo nyumbani na hatokuwa na raha. Akitambua nafasi yake kama mzazi mtaishi kwa amani. Pia hongera kwa kutoona kero kuishi na familia ya mumeo, wengi linawashinda hili.

Acha kujizima data mkeo ‘anayatindinganya’ mambo

Swali:  Anti pole na majukumu la kila siku na hongera kwa kutuponya. Nina jambo naomba nikushirikishe. Mke wangu anafanya kazi ofisi tofauti na mimi, ila fani zetu zinafanana, kwa hiyo kukutana watu wa ofisi yake na yangu ni jambo la kawaida.

Changamoto ninayopitia ambayo sijui nifanye nini kuikomesha ni watu kumsingizia mke wangu kuwa ana mahusiano nje ya ndoa yetu.

Wanaomsingizia ni watu tulionao kwenye fani na wa ofisini kwao. Kuna mmoja aliwahi kunionyesha SMS anazodai mke wangu alikuwa anachati na kijana anayetoka naye kimapenzi kazini. Kuna walionipigia picha na video anavyojirusha akiwa safarini kikazi na wanaume mbalimbali. Binafsi ninajua wanamsingizia kwa sababu amepata mafanikio ya haraka huko kazini kwake, pia ni mzuri.

Ushauri ninaoomba kwako ni namna gani watu wataacha kumjadili mke wangu kwa mabaya. Nifanye nini ili waachane naye aendelee kupambania maisha yetu?

Jibu: …. Kuna kitu hakipo sawa mahali. Mtu mwenye ndoa, achana na kusingiziwa kwa video, picha na sms hapaswi hata kuhisiwa kuenenda kinyume na ndoa yake.

Sikufundishi tabia mbaya, ila kuna jambo linafanyika halijakaa sawa kwa mke wa mtu, anaruhusu vipi kuwa karibu na wanaume wakichati na kujirusha ilhali ameolewa. Hata kama hatoki nao ila haina afya sana kwenye ndoa yenu. Acha kudharau unachoambiwa, kifanyie kazi ili kunusuru ndoa yako kabla haijakwenda mrama.

Pia sitaki kukuficha, huyo mkeo ni muhuni, anapenda mambo yanayopaswa kufanywa na wasiokuwa ndani ya ndoa.

Kama ana hamu ya kujirusha si akuchukue wewe mkajirushe wote, ukiona hadi wenzake wanasema atakuwa anafanya mambo ya ajabu akiwa nje ya nyumbani.

Kusingiziwa kupo, lakini mpaka wanampiga picha na video, ujue amekubuhu na anawakera wengi.

Unaweza kumuuliza mwenyewe au kufuatilia ili ujue ukweli mapema umkanye kunusuru ndoa yako.

Pia umeruhusu mno watu kukuingia kirahisi hadi wanakutumia hayo mavideo na mapicha, usiwape waja nafasi kubwa kiasi hicho kwenye ndoa yenu, watakuchosha.