
Dar es Salaam. Kwa bahati mbaya kuna vitabu vichache sana vinavyozungumzia historia ya muziki wa dansi na taarab Tanzania, na hata hivyo karibu vyote vimeandikwa na watu kutoka nje ya Tanzania. Na ni historia ya bendi na vikundi vichache vya Dar es Salaam na Tanga.
Kukosekana kwa kumbukumbu hizo taratibu unaona jamii ikisahau mchango mkubwa ambao wanamuziki walichangia katika kulifanya taifa hili kuwa lilipo. Muziki wa dansi na taarab, ulihamasisha kukua kwa lugha ya Kiswahili, muziki huu ulisaidia kuondoa tofauti za ukabila, muziki huu ulitumika kusambaza ujumbe wa kudai Uhuru na hata mara nyingine maonyesho ya muziki huu yalitumika kama nafasi kwa viongozi waliokuwa wakifanya mikutano ya kutafuta Uhuru wa nchi hii.
Matamko ya viongozi wengi wa sasa, hata wale wenye uzalendo mkubwa bado yanaonyesha kutokuwa na taarifa ya historia ya mchango wa muziki wa dansi na taarab katika historia ya nchi hii. Wanamuziki walianza kutunga nyimbo ambazo zilielezea hali halisi na hata kutabiri nchi yetu kupata Uhuru miaka kadhaa kabla ya nchi kupata Uhuru, nyimbo nyingine ziligeuka kuwa shubiri kwa utawala wa wakoloni kiasi cha kusakwa kwa udi na uvumba na kuharibiwa.
Santuri za wimbo wa Marehemu Frank Humplick na Dada zake ulioitwa ‘I am a democrat’ au wengi waliufahamu kwa jina la ‘English yes no, kizungu sikijui’, ilikuwa moja ya santuri ambazo zilisakwa nyumba kwa nyumba na kuvunjwa, kwa kuwa zilionyesha kuhamasisha wananchi kutafuta Uhuru toka kwa wakoloni.
Katika uchaguzi wa kwanza wa nchi hii, uchaguzi uliokuwa na utata mwingi, ulitaka kuwe na wagombea watatu kwa kila jimbo, Mwafrika, Muhindi na Mzungu. Salum Abdallah na kundi lake la Cuban Marimba walitunga wimbo ambao ulikuwa na maneno haya;
Siku moja nilipita barabarani,
Nikawakuta kuku watatu wanapigana,
Kuku mweusi anampiga kuku mweupe,
Kuku mweupe anampiga kuku mwekundu
Kuku mwekundu anapiga kuku mweusi
Wimbo huu nao ulileta tafrani kwa mkoloni. Lakini Mungu mkubwa hatimaye tulipata Uhuru na bendi nyingi sana zilitunga nyimbo kuhusu furaha ya kupata Uhuru..
Baada ya Uhuru wanamuziki walitegemea sana Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC), ambayo baada ikaja kuwa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kwa ajili ya kurekodi nyimbo zao.
Kulikuweko na masharti ya kurekodi katika studio za redio hii ya taifa, masharti haya yakibadilika au kuongezwa mara kwa mara na vyombo mbalimbali, vikiwemo Umoja wa Vijana wa TANU (TYL), uongozi wa kitaifa mara nyingine mkoa wa Dar es Salaam, na hata uongozi wa Radio yenyewe.
Kati ya masharti yaliyokuweko ni yale yaliyoelekeza kuwa nyimbo zote kabla hazijarekodiwa RTD, mashahiri yake ilikuwa lazima yapelekwe kuhakikiwa na kamati ya RTD, na hapo maneno yalichujwa na hatimaye nyimbo ambazo ziliruhusiwa kurekodiwa zilipitishwa na zile zenye utata aidha zilikataliwa au wanamuziki walishauriwa kuzifanyia mabadiliko.
Na ilitokea hata mara nyingine nyimbo ambazo zilipitia mchujo huu zilikuja baadaye kuzuiliwa kurushwa hewani na moja ya vyombo nilivyovitaja hapo juu.
Sharti jingine lilikuja kutolewa, ni kuwa kila bendi inapokwenda kurekodi ni lazima kuweko na wimbo mmoja au zaidi wa kizalendo au wenye ujumbe kwa jamii, sharti hilo ndilo lililofanya kuweko na nyimbo nyingi sana za kizalendo zilizotungwa na wanamuziki wa Kitanzania.
Pia kulikuweko na maazimio, matamko ya serikali, kampeni mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa, hata matukio makubwa na kwa yote hayo vikundi vya muziki vilihamasika kutunga na kurekodi nyimbo ambazo kwa sasa zimekuwa ni kigezo cha kuonyesha kuwa vijana zamani walikuwa watunzi wa nyimbo za kizalendo.
Labda nizungumzie nyimbo chache za aina hii ambazo binafsi nilishiriki. Nianze na wimbo ambao nilitunga na kushiriki kuimba wakati nikiwa katika bendi ya Orchestra Mambo Bado mwanzoni mwa mwaka 1983, wimbo ulioitwa CCM Itashinda, wimbo huu ulitungwa wiki chache kabla ya sherehe za kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi mwaka huo.
Wimbo huo ulikuwa ni wa kukamilisha album iliyokuwa na wimbo maarufu wa Bomoa Tujenga Kesho ambao ulikuja kupigwa marufuku na Umoja wa Vijana Mkoa wa Dar es Salaam kuwa usipigwe katika radio.
Mwaka 1988 nikiwa katika bendi ya TANCUT Almasi, marehemu Mzee Zacharia Daniel aliyekuwa maarufu kwa jina la Zacharia Tendawema, alitunga wimbo ulioitwa Kuwajibika, waimbaji katika wimbo huo walikuwa Mzee Daniel Tendawema, mapacha Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa, Hashim Kasanga na Mohamed Shaweji.
Marehemu Zacharia alipewa jina la Tendawema kutokana na kutunga wimbo Tenda Wema Uende Zako alioutunga na kuuimba akiwa na Shinyanga Jazz Band.
Nilihama kutoka bendi ya