Anko Kitime: Wanamuziki maarufu kikwazo utekelezaji wa hakimiliki

Dar es Salaam. Januari 25, 1993 ulifanyika uchaguzi mkuu wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania  (CHAMUDATA), katika uchaguzi huo nilichaguliwa mwenyekiti wa chama hicho, Said Mabela alichaguliwa Makamu wa Mwenyekiti, Katibu Mkuu  Rashidi Pembe na Haji Seseme akawa Naibu Katibu Mkuu.

 Ajenda yetu kubwa ilikuwa ni suala la Hakimiliki. suala ambalo harakati zake zilianza mwaka 1987 wakati CHAMUDATA ikiwa chini ya uenyekiti wa marehemu Kassim Mapili. 

Mwezi Mei mwaka 1993, ulifanyika mkutano mkubwa wa Hakimiliki ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu Mheshimiwa John Malecela, na mwenyekiti wa mkutano ule alikuwa Jaji Mkuu wakati huo, mkutano huo ulianzisha safari ambapo hatimaye mwaka 1999, sheria mpya ya Hakimiliki ilipitishwa na Bunge la Tanzania. Sheria hiyo iliitwa   Copyright and Neighbouring Rights Act 1999.

Ni mwaka wa 26 sasa toka sheria hiyo ilipopitishwa, kwa tuliokuweko toka mwanzo wa mchakato hiki ni kipindi kirefu, kamwe hatukutegemea kuwa miaka yote hiyo itapita na matunda ya hakimiliki hayajaliwa. 

Kati ya mwaka 1993 mpaka 1999, niliweza hudhuria mikutano na madarasa chungu nzima kuhusu Hakimiliki na haki nyingine za wanamuziki, mikutano hiyo ilifanyika hapa nchini na nchi nyingi za nje, kituo kimoja kikubwa kilikuwa wazi, katika nchi nyingine kwenye mikutano ya harakati za Hakimiliki au za kudai haki nyingine za wanamuziki, wanamuziki maarufu wa nchi hizo, au wawakilishi wao, ndio waliokuwa wakijazana katika mikutano hiyo, kwa kuwa ni wazi kama kulikuwa na kuibiwa kwa kazi za sanaa kadri unavyokuwa maarufu ndio unaibiwa zaidi. 

Lakini jambo hilo kila mara  limekuwa  tofauti sana na hapa kwetu, wasanii maarufu huona hawastahili kuwa katika mkutano mmoja na wasanii wasio maarufu.
Kwa vyovyote vile moja ya vikwazo vya kushindwa kuwa na maendeleo stahiki katika upande wa Hakimiliki ni wanamuziki maarufu.

Nitoe mifano michache, mwaka 1995, Radio Tanzania Dar es Salaam ilianzisha biashara ya kuuza kanda za nyimbo za vikundi vya muziki mbalimbali vya Tanzania, wanamuziki hawakuwa wanapata hata senti tano ya mauzo hayo, CHAMUDATA iliiandikia barua RTD kutaka aidha iache biashara hiyo au iwe inatoa mgao wa pato kwa wanamuziki ambao kazi zao zinauzwa. 

Wanamuziki waliokuwa maarufu zama hizo wakaenda kwenye gazeti moja na kuitetea RTD na kuonya kuwa CHAMUDATA isiisumbue RTD kwani imewasaidia sana. 

Vita hiyo ikakosa nguvu ikafa. Wanamuziki hao sasa ni wazee ambao maisha yao ni magumu japo nyimbo zao bado zinatumika sana, zinapigwa na bendi nyingine, zinasambazwa kwenye vikundi vya WhatsApp, zinapigwa kwenye redio, zinasambazwa kwenye mitandao kama YouTube, na kwa sasa uwezo wa kudai haki hawana tena, masikini. 

COSOTA, ambacho ni chama cha Hakimiliki Tanzania kilikuwa na mikakati kadhaa ya kusaidia kukusanya mirabaha ya wanamuziki, kati ya mikakati hiyo mmoja ulikuwa ni kusajili kumbi ambazo zinatumia muziki. Kumbi kadhaa zilikataa kulipa kwa kuwa wanamuziki wenyewe walizishawishi zisilipe mirabaha hiyo. 

Miaka michache iliyopita ilitengezwa kampuni iliyokuwa na vifaa vilivyokuwa na uwezo wa kutambua kila wimbo uliokuwa unapigwa katika vyombo vya utangazaji,  vifaa hivi vingeweza kurahisisha kupata taarifa ambazo zingewezesha kila wimbo uliopigwa kwenye vyombo vya utangazaji kulipiwa mirabaha stahiki, ni wanamuziki maarufu wenyewe walioipinga kampuni hiyo iliyokuwa katika mikakati ya kufanya kazi na COSOTA, na wakati huohuo wasanii hawahawa maarufu wakaunda kamati ya kupinga vyombo vya utangazaji visilipe mirabaha.

Pamoja na kwamba baadhi ya wanamuziki maarufu wameweza hata kufikia kuwa wabunge, jambo ambalo lilitegemewa lingebadilisha sana hali za wanamuziki, lakini loh! mchango wa wabunge hao kuhusu kufanikisha utendaji wa Hakimiliki ni kama haupo katika kumbukumbu, ni kama vile wakishapata ubunge, matatizo ya muziki hayawahusu tena. 

Katika zama hizi, wanamuziki wengi maarufu wana ukaribu sana na viongozi wa serikali na wanasiasa. Na ni wazi wanasikilizwa sana, ungetegemea ukaribu huu ungesaidia tasnia, lakini haiko hivyo, ukisikiliza maombi ya wasanii wengi  kwa viongozi wa kitaifa, ni matatizo yao binafsi na si matatizo kwa niaba ya tasnia nzima ya muziki. 

Hali hii inanikumbusha mkutano mmoja kati wa kundi moja la wanamuziki na wafadhili kutoka Norway, mkutano huo ulifanyika mwaka 1997 katika ukumbi mmoja ndani ya ubalozi wa Norway. 

Moja ya swali la wafadhili lilikuwa Je wanamuziki wanahitaji nini? Kuna aliyetaja bendi zipewe lori la kubeba vyombo  kupeleka eneo la maonyesho, na basi la kupeleka wanamuziki kazini, viongozi wa bendi waliombewa pikipiki ili wawe wanawahi kazini!  Wafadhili hawakurudi tena. 

Jambo jingine ambalo ni bahati mbaya sana, ni kuwa kwa miaka mingi kila Waziri wa Utamaduni anapoteuliwa hufanya mkutano na wanamuziki, nasema bahati mbaya kwa kuwa sijawahi kusikia matokeo ya mikutano hiyo, pili mikutano hiyo yote hufanyika Dar es Salaam tu, hivi mikoa mingine haina wanamuziki?

Kisha nitoe ushauri kwa wanamuziki maarufu, jamani  mkikutana na viongozi ombeni mambo yenye manufaa kwa tasnia nzima, kumbukeni umaarufu hupita, tayarisheni mazingira ya kuweza kuishi baada ya umaarufu. 

Na viongozi wetu, hasa wabunge, wakuu naomba niwakumbushe hata kwenye majimbo yenu kuna wanamuziki mnawasaidiaje? Inasikitisha sana mnapowatetea wanamuziki maarufu na kutowapa nafasi wasanii wa majimboni kwenu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *