Anko Kitime: Verckys mpiga sax aliyetikisa Afrika

Dar es Salaam, Georges Kiamuangana Mateta aliyejulikana zaidi kama Verckys alizaliwa Kisantu, Congo-Kinshasa mwezi Mei 19, 1944. Jina la Verckys alijipa baada ya kusikia vibaya jina la mpiga sax wa Kimarekani King Curtis. Mwenyewe aliwahi kusema alisikia ‘Verckys’ na si ‘Curtis’. 

Verckys, alipata elimu nzuri na hasa kwa vile alikuwa mtoto wa mfanyabiashara tajiri, toka utoto alipenda sana muziki, alikuwa na uwezo wa kupiga  vyombo kadhaa vya kupuliza kama vile  flute and clarinet, baadaye akajifunza  saxophone wakati akiwa kwenye kikundi cha muziki cha kanisa lililokuwa chini ya mchungaji wa Kicongo aliyejulikana kwa jina la Nabii Simon Kimbangu. 

Mwaka 1962 alijiunga na kundi  la Los Cantina, kisha akahamia kundi lililojiita  Jamel Jazz.  Kwa muda mfupi alijiunga na kundi la  Paul “Dewayon” Ebengo lililoitwa  Conga Jazz na hatimaye akajiunga na  O.K. Jazz mwaka 1963.

Upigaji wake wa sax ulikuwa na vionjo vya jazz la Kimarekani, upigaji wake wa saxophone unaweza kusikika kwenye vibao  maarufu cha Polo kilichopigwa na OK Jazz miaka hiyo ya mwanzoni mwa 60, upigaji wake ukampatia sifa ya kuitwa ‘Mtu mwenye mapafu ya chuma. 

Verckys alikuwa karibu sana na Franco  lakini kuna wakati Franco alipoenda kwenye ziara Ulaya 1968 akawa na sehemu ya wapigaji wake, huku nyuma  Verckys akachukua wanamuziki waliobaki akiwemo muimbaji  Youlou Mabiala, wakaingia studio na kurekodi nyimbo nne. 

Franco aliporudi toka Ulaya moto uliwaka, baada ya ugomvi mkubwa, tarehe  5 April 1969 Verckys aliacha  OK Jazz  na kuanzisha kundi lake mwenyewe aliloliita Orchestre Veve. Waimbaji wake walikuwa vijana walioanza kujitokeza kwa uimbaji kule Kongo kama vile  Matadidi “Mario” Mabele, Marcel “Djeskain” Loko, and Bonghat “Sinatra” Tshekabu, vijana hao baadaye walikuja kuanzisha kundi lililoleta ushindani mkubwa katika muziki wa Kongo.

Kundi lao waliliita Orchestra  Sosoliso na waimbaji hao watatu wakajiita Trio Madjesi. Nyimbo za kwanza maarufu za Orchestra zilikuwa ni Mfumbwa, Bankoko baboyi na Fifi Solange .

Orchestre Vévé ili rekodi nyimbo nyingine nyingi sana baada ya hapo  ukiwemo Nakomitunaka au kwa Kiswahili Najiuliza, wimbo huu ulioimbwa na Pepe Kalle ulikuja kuleta ugomvi mkubwa na Kanisa Katoliki kutoka na maswali yake yaliyouliza kwanini malaika huonyeshwa ni wazungu weupe na shetani  weusi.

Na pia kanisa hilo lilikuwa likipinga mpango wa Rais Mobutu ulioitwa  wa Uhalisia ambapo watu waliambiwa warudie majina yao ya asili.

Baada ya bendi ya Veve kuwa  na mafanikio makubwa, Verckys akaanzisha lebo yake aliyoiita “Les Editions Vévé” kupitia lebo hii Verckys akaanza pia kusambaza nyimbo za bendi yake, na ilikuwa ni wakati huo alipojenga studio yake na kuanza kurekodi bendi nyingi zilizokuja kutingisha  Afrika.

Bendi kama Les Grands Maquisards, Orchestre Kiam, Bella Bella, Lipua Lipua, Les Kamale, Empire Bakuba, Thu Zaina, Victoria Eleison na  Zaiko Langa Langa zilipata bahati ya kurekodiwa katika studio za mwamba huyu.

Verckys akajenga kituo kingine alichokiita Veve Centre, ambapo kulikuwa na makazi ya wanamuziki sehemu za kufanyia mazoezi na studio iliyokuwa ya kisasa zaidi jijini Kinshasa.

Umaarufu wa Orchestra Veve ulisambaa Afrika nzima mwaka 1974 bendi ilifanya ziara ya miezi miwili nchini Kenya, ni wakati huo Orchestra Veve ilirekodi nyimbo tatu ambazo zilikuwa maalumu kwa ajili ya soko la Kenya, nyimbo hizo zilizopigwa kwa mtindo wa Afro Rock zilikuwa ni Bassala Hot, Cheka Sana na Talali Talala, baada ya hapo umaarufu wa bendi hii ukaiteka Afrika ya Mashariki yote.

Mwaka 1972 Verckys aliwapata waimbaji wawili Pepe Kalle na Nyboma, kupitia bendi ya Bella Bella waliimba nyimbo maarufu za Sola, Mbuta na Kamale, wimbo wa Kamale ulishinda zawadi ya wimbo bora wa mwaka 1973 huko Kongo.

Kipindi hicho hicho ndipo akaanzisha Orchestra Lipua Lipua ikiwa na muimbaji Nyboma Mwandido nao wakarekodi  Amba, Mombasa, Niki bue na nyimbo nyingine nyingi tamu lakini Nyboma na wenzake wakaihama Lipua Lipua na kuanzisha bendi nyingine maarufu iliyoitwa Orchestra Les Kamale.

Mwaka 1976 alibadili jina la lebo yake na kuiita ZADIS kifupi cha Zaire Disc. Mwaka huo huo Orchestra Veve ikatoa vibao viwili vilivyotungwa na mpiga gitaa la bezi la bendi hiyo Celi Bitsou, vibao hivyo Baluti na Muana Mburu bado vinapendwa na wapenzi wa muziki wa rumba mpaka leo.

Mwaka 1978 Verckys alimrekodi mwimbaji kijana aliyeitwa Koffi Olomide, matokeo ya muimbaji huyu dunia nzima yanajulikana.

Verckys alichaguliwa kuwa Rais wa wanamuziki wa Zaire mara baada ya Franco kumaliza muda wake 1978. Kiukweli Verckys ametoa mchango mkubwa sana katika maendeleo ya muziki wa Congo na Afrika kimuziki na kibiashara. Verckys alifariki tarehe 13 Octoba 2023.