Dar es Salaam. Moja ya mambo ambayo yamepungua sana kwenye bendi siku hizi ni suala la uhasama kati ya bendi moja na nyingine.
Bendi zilikuwa na wafuasi wenye upenzi wa hali ya juu, kiasi cha kwamba wapenzi wa bendi moja walikuwa hawaingii katika onyesho la bendi nyingine, waliamini bendi yao ndio pekee inayojua kupiga muziki mzuri, na hata mara nyingine kuona wapenzi wa bendi nyingine hawastahili kuwa rafiki zao kwani hawaelewi muziki bora.
Kulikuwa na bendi zilizokuwa na upinzani wa wazi wazi, na mashabiki wake waliweza hata kutwangana ngumi katika kutetea sifa au maslahi za bendi zao pendwa, hadithi za mapokeo zinasema si mara moja wapenzi wa Kilwa Jazz Band walitwangana na wapenzi wa Dar es Salaam Jazz Band. Hali hii ilifanya hata wanamuziki kuingia katika utamaduni huu na kujiwekea mipaka ya bendi ambazo wangeweza kuzitembelea au kutokuzitembelea.
Hali hii ya upinzani ambayo katika bendi nyingine iligeuka uhasama wa waziwazi ilikuzwa na tatizo jingine la imani za ushirikina. Haikuwa siri kuwa bendi nyingi ziliamini kuwa ni lazima ushirikina uhusike ili kupata umaarufu na pia kujikinga na kuharibiwa mambo na bendi nyingine.

Na hakika hakuna kitu kinachoweza kuleta uhasama mkubwa kati ya watu kama imani ya ushirikina. Hali hii ikafanya mwanamuziki kuonekana kwenye onyesho la bendi pinzani kuwa ni chanzo cha matatizo makubwa sana.
Kwanza katika kuingia kwenye onyesho la bendi pinzani kulikuwa na uwezekano wa mwanamuziki kujikuta unatengwa na wapenzi na wanamuziki wa bendi hiyo na hatimaye hata kufukuzwa ukumbini na wanamuziki wenzako. Na mara nyingi swali lililosababisha ufukuzwe lilikuwa, huyu kafwata nini hapa? Jibu lilikuwa lazima amekuja kumwaga uchawi.
Kama ikitokea utapokelewa vizuri na wanamuziki wenzio pengine ukapewa nafasi kushiriki jukwaani, kesi hiyo itahamia kwenye bendi yako, itakapojulikana ulipanda kwenye jukwaa la bendi pinzani, viongozi wako watataka kujua ulikuwa unatafuta nini kwenye jukwaa la bendi pinzani?
Wanamuziki wengi walijikuta wanafukuzwa kazi kwa kuhofia lazima wamepewa ‘kitu’ cha kuidhuru bendi yao. Nakumbuka mwaka 1988 wakati nikiwa katika bendi ya Tancut Almasi Orchestra kutoka Iringa tulikuja Dar es Salaam ili kurekodi albamu yetu ya kwanza iliyokuwa na nyimbo kama Nimemkaribisha Nyoka, Mtaulage, Kiwele, Kashasha na nyinginezo.
Mwanamuziki mmoja aliyekuwa mahiri sana kwa upigaji wa tumba miaka hiyo, Marehemu Siddy Morris (Tanzania One), alifika katika studio za RTD na kushiriki kurekodi nyimbo za Tancut Almasi, hii ilikuwa ni kutokana na urafiki aliokuwa nao kwa baadhi ya wanamuziki wa Tancut, bendi haikuona tatizo lolote kwani labda kutokana na kuwa ilikuwa bendi ya ‘mkoani’ haikuwa na ‘bendi pinzani’.
Basi ilionekana ni heshima kubwa kwa mwanamuziki mkongwe maarufu kutaka kushiriki katika kurekodi wimbo mmoja wa albamu ile. Tatizo lilitokea kwenye bendi iliyokuwa imemuajiri Siddy Morris, ilipopata taarifa ya ushiriki ule, akasimishwa kazi mara moja.

Kisa kingine kilikuwa katika bendi nyingine niliyokuweko iliyokuwa na makao yake makuu kule Mabibo, siku moja wakati wa mazoezi alitutembelea kiongozi mmoja wa bendi ya Maquis aliyefika pale na pikipiki yake, viongozi wa bendi yetu walionekana kupigwa butaa kwa kumuona yule mwanamuziki katika eneo letu la kazi ghafla vile, mazoezi yalisimamishwa na baada ya hapo ilianza kazi ya kuhakikisha bwana yule amemfukuza kutoka pale kwetu na kisha vijana wasaidizi wa bendi kuamriwa kupiga deki sehemu zote alizokanyaga mgeni wetu yule.
Kukiwa na imani kuwa kuja kwake pale haikuwa bure, hivyo kupiga deki sehemu alizozigusa kutasafisha hali ya ukumbi! Suala la kuwa mwanamuziki mwenzenu anaweza kuja kwa ajili tu ya upenzi wa muziki au urafiki tu na mtu katika bendi lilikuwa linachelewa sana kuingia akilini.
Ila ieleweke kwamba kuwa wanamuziki walikuwa hawatembeleani la hasha hilo lilikuwa jambo la kawaida lakini kulikuwa na bendi pinzani au zile zenye uongozi ulioamini mambo ya ushirikina, hapo ndipo kulikuwa na tatizo kubwa.
Shida ilikuwa kubwa zaidi pale mwanamuziki anapohamia bendi pinzani, matusi mengi yaliendelea kwenye bendi aliyokuwa akishiriki, na hata nyimbo ziliachwa na kusahauliwa kama mtunzi wake au muimbaji au mpigaji wake amehamia bendi pinzani. Kuna bendi iliwahi kununua gitaa jipya ili lile lililokuwa likitumia na mwanamuziki aliyehama bendi kwenda bendi pinzani lisiguswe tena. Kwani iliaminika kuwa inawezekana aliacha uchawi kwenye gitaa hilo ambao ungeweza kuiathiri bendi.
Katika zama za leo si ajabu kukuta mwanamuziki mmoja anashiriki hata bendi tatu au nne kwa siku tofauti. Jambo jema lakini hapo ndipo kimuziki unakuta bendi zikipiga muziki unaofanana, hata nyimbo zinafanana, unaweza kupita bendi tano zote ukakuta zinapiga Rangi ya Chungwa, Masafa Marefu, Kinyaunyau, Georgina, au sebene zinazofanana kabisa. Raha ya muziki tofauti kwa bendi tofauti imepotea sana.