Anko Kitime: Tanga ndipo kilipozikwa kitovu cha muziki wa dansi Tanzania

Dar es Salaam. Wiki chache zilizopita Rais Mama Samia Suluhu Hassan alimtunza mtunzi na muimbaji wa bendi ya Atomic Jazz Band ya Tanga, mzee Steven Hiza, kwa utunzi wake uliotukuka wa wimbo Tanzania Yetu ndio nchi ya furaha.

Kwa anayefahamu historia ya muziki wa dansi hapa Tanzania, si ajabu kwa Tanga kuchukua tuzo ya muziki kwani kwa kweli unaweza kusema Tanga ndipo kilipozikwa kitovu cha muziki wa dansi Tanzania, Tanga ndipo ulipoanza uchezaji wa muziki wa dansi.

Unapoongelea historia ya nchi yetu ni lazima uanze na Tanga,  kamwe huwezi kulikwepa jiji hilo la kihistoria. Tanga ndio ulikuwa mji mkuu wa kwanza wa kiserikali katika mipaka yetu.

Wakati nchi yetu iko chini ya utawala wa Wajerumani, wakoloni hawa waliiona bandari ya Tanga kuwa na umuhimu mkubwa kwao, hivyo wakaanza kuwekeza miundombinu kadhaa katika mji ule ili uwe kweli mji mkuu wa utawala wao.

Pengine nigusie hapa kuwa Tanga School ndio ilikuwa shule ya kwanza ya serikali nchini, nayo ilianzishwa enzi hizohizo za Wajerumani. Mpangilio mzuri wa mitaa kuwa na mitaa yenye majina maarufu ya barabara ya kwanza na kuendelea yalitokana na mipango miji ya zama hizo.

Wajerumani hao hao ndio walioingiza zao la katani nchini, zao ambalo lililimwa na kustawi sana mkoani Tanga. Mjerumani mmoja aliiba miche ya  zao hilo kutoka jimbo la Yucatan huko Mexico na kuweza kusafirisha miche hiyo kwenye ngozi ya mamba na hatimaye kuja kuipanda hapa nchini, jina la zao hilo kuitwa Katani ni kutokana na chanzo zilikotoka mbegu za zao hilo.

Mashamba makubwa ya katani yalisababisha vijana kutoka pande mbalimbali za Afrika Mashariki na kati kufurika Tanga kutafuta ajira, ajira hizi ziliendelea hata baada ya Wajerumani kufukuzwa na Waingereza, ambao nao walianzisha mfumo ulioitwa Sisal Labourers Bureau (SILABU), ili kupata vijana wa kufanya kazi katika mashamba ya katani.

Uwingi wa vijana katika mji wa Tanga ukaufanya mji huo kuchangamka sana, na historia ya uchangamfu wa Tanga bado inaongelewa mpaka leo. 

Palipo na vijana burudani ndio mahala pake, vikundi vingi vya burudani viliundwa. Kwa kuwa vijana waliokutana Tanga walitoka katika makabila mbalimbali, viliundwa vikundi vya ngoma za kiasili vya makabila mbalimbali, vikaundwa vikundi vya kushindana kucheza dansa la kisasa wakitumia muziki kutoka kwenye santuri, zikaundwa bendi na vikundi vya taarabu vizuri, Tanga ilikuwa motomoto. 

Tanga ikajipatia sifa kuwa kila kijana aliyekwenda huko hakutaka tena kurudi kwao. Kati ya vikundi  hivyo vya muziki,  vingine vilikuja kujitokeza na kuwa maarufu nje ya Tanga na hata nje ya mipaka ya nchi yetu.  Vikundi vya Taarab kama Young Novelty, Lucky Star, Black Star, viliweza kuweka alama ambazo zimebaki mpaka leo miaka mingi baada ya vikundi hivyo kutoweka.

Halikadhalika zilikuweko bendi nyingi zikiwemo Amboni Jazz Band iliyokuja kujipatia sifa kubwa na wimbo wake wa Kidomidomi, kulikuwa na Tanga International Orchestra, Watangatanga Band, ilikuweko White Star Jazz Band, pia Jamhuri Jazz Band ambayo kama nilivyowahi kugusia katika makala zilizopita kuwa bendi hiyo ilianza kwa jina la Young Nyamwezi Band, wenyewe waliita Yanga Nyamwezi, jina hilo lilikuja kutokana na bendi kuanzishwa na klabu ya vijana kutoka Unyamwezini.

Bendi nyingine kubwa iliyokuweko Tanga iliitwa Atomic Jazz Band, bendi hii ilianzishwa kwenye mwaka 1958, ilikuwa ndio bendi ya vijana wazawa  wa mji wa Tanga. Bendi hii ilikuwa na nyimbo nyingi sana maarufu ukiwemo Tanzania Yetu wa Mzee Hiza.

Kati ya nyimbo zilizotikisa Afrika ya Mashariki zilikuwa, Tumuondoe Smith, wimbo uliokuwa ukihamasisha kumuondoa mtawala Ian Smith wa Rhodesia ya Kusini ambayo sasa inaitwa Zimbabwe,  Aibu waliopata wenzetu Jumamosi, Masikini Suzy, Shemeji usimpige dada, Joyce, Duniani kuna mambo mengi na kadhalika. 
Atomic Jazz Band kama zilivyokuwa bendi nyingine pale Tanga ilikuwa bendi  ikipiga mitindo mingi, mtindo wao mmoja uliopata umaarufu sana  uliitwa ‘Kiweke’.

Moja wimbo maarufu wa Atomic Jazz Band ulikuwa ni wimbo ulioitwa Mado, katika wimbo huu gitaa la solo lilipigwa na nguli marehemu John Kijiko, ambaye pia hutambulika  kuwa ndiye mtunzi wa wimbo huu, lakini mtunzi halisi  wa wimbo huu wakati huo alikuwa bado mwanafunzi na wazazi wake hawakutaka kabisa ajiunge na mambo ya muziki, alikuwa rafiki mkubwa wa John Kijiko hivyo alipoutunga akampa rafiki yake  aurekodi.

Mtunzi huyo wa wimbo huo, mpaka leo rafiki zake wa karibu humuita Mado kutokana na kumbukumbu ya wimbo huo iliotamba miaka ya 70. Haya ndio mashahiri ya kibao Mado, kilichopigwa katika mtindo wa Kiweke.

Mado mpenzi wangu usiivunje ahadi
Nilikupenda tangu umdogo na hivi sasa  umekuwa 
Fanya haraka Mado umalize masomo yako
Tutayarishe harusi yetu
Tuishi sote kwa raha.
Mado mpenzi wangu usiivunje ahadi
Nilikupenda tangu umdogo na hivi sasa  umekuwa 
Fanya haraka Mado umalize masomo yako
Tutayarishe harusi yetu
Tuishi sote kwa raha.

Chorus
Oh Mado Oh Mado nakungojea mwenzio
Mimi sitaki mwingine wowo
Ni wewe Mado wangu
Oh Mado Oh Mado nakungojea mwenzio
Mimi sitaki mwingine wowo
Ni wewe Mado wangu
Mimi sitaki mwingine wowo
Ni wewe mado wangu
Mado Mado ehhhhh.