Anko Kitime: Safari za bendi enzi hizo hazikuwa lelemama

Dar es Salaam. Moja ya sifa kubwa ya bendi za zamani ni utaratibu wa kufanya ziara. Bendi ziliweza kufanya ziara hata za miezi mitatu kabla ya kurudi kwenye kituo chao.

Katika kipindi ambacho nilikuwa mwanamuziki wa Tancut Almasi Orchestra na Vijana Jazz Band kati ya mwaka 1986 hadi 1994, niliweza kuzunguka katika mikoa yote nchini kasoro sikupata bahati ya  kuvuka kwenda Pemba. 

Pamoja na kuweko kwa radio  moja tu ya taifa na magazeti machache, safari hizo karibu zote zilikuwa za mafanikio, japo zilikuwa na changamoto kubwa sana.  Bendi kufanya safari za muziki haikuwa rahisi kama ilivyo siku hizi.

Kwanza kulikuwa na tatizo la barabara mbovu, barabara chache sana zilizokuwa na lami, pili vyombo vya mawasiliano vilikuwa haba, vyombo vya utangazaj vilikuwa vichache, mawasiliano ya simu tu nayo yalikuwa adimu. 

Kabla ya kuanza safari kulikuwa na taratibu za kuomba kibali, bendi ilipoamua kusafiri ililazimika kuomba kibali cha kutoka nje ya mkoa, kibali hiki kilitolewa na Afisa Utamaduni wa Mkoa, baada ya kupata kibali hiki, ndipo iliwezekana kumpatia Afisa Utamaduni wa Mkoa ambao bendi imepanga kufanya maonyesho ili kuruhusiwa kuingia katika mkoa huo na kufanya maonyesho.

Afisa Utamaduni wa Mkoa akitoa ruksa ndipo ruksa hiyo unaitumia kuomba kibali kwa Afisa Utamaduni wa wilaya ambako ndiko muziki utaporomoshwa. Afisa yoyote kati ya hawa alikuwa na uwezo wa kukunyima kibali na safari ikafutika.

Ni mara chache sana hilo lilitokea, lakini lilikuwa linawezekana. Katika vibali vya wilaya, kulikuwa na masharti ya urefu wa onyesho na pia ada ya kupiga muziki ambayo ilitofautiana kati ya wilaya moja na nyingine.

Wilaya nyingine zikiwa na ada iliyopangwa na nyingine zilichukua asilimia fulani ya pato la bendi.  Kwa kawaida baada ya kupata kibali, bendi ilimtuma meneja wake kutangulia sehemu ambazo bendi  ilitegemea kupiga muziki ili kufanya mipango, ikiwemo kutafuta ukumbi na kufanya makubaliano ya mgao wa mapato, maana siku hizo mara chache sana ambapo bendi ilikodishwa na kulipwa. 

Mapato yalitokana na kiingilio cha mlangoni, hivyo ililazimika kuwa na makubaliano ya namna ya kugawana kitachopatikana. Meneja pia alitafuta sehemu za malazi na mara nyingine hata sehemu ambazo wanamuziki watakuwa wanakula.

Pia kazi nyingine muhimu ilikuwa ni kusambaza matangazo ya ujio wa bendi. Kama nilivyosema zamani hakukuwa na radio za mikoani, na magazeti yalikuwa machache, hivyo kazi moja kubwa  ilikuwa ni kuandika matangazo kwa mkono kisha kuyarudufu na kubandika sehemu mbalimbali za mji.

Kwenye ile miji ambayo haikuwa na mashine za kurudufu, matangazo yote yaliandikwa kwa mkono na kusambazwa. 

Pia kuna miji ilikuwa na watu ambao walikuwa wakifanya kazi ya kutangaza biashara, hawa walikuwa na vipaza sauti vilivyotumia betri za tochi. Hawa walikodishwa na kuzunguka mji kwa baiskeli au hata kwa mguu na kutangaza kuhusu ujio wa bendi. 

Nakumbuka safari moja ambayo tuliifanya kule Mpanda, tulimkuta bingwa wa kutangaza katika mji ule aliyekuwa kapewa jina la mtangazaji maarufu wa RTD. Bwana huyu aliitwa na wenyeji Mshindo Mkeyenge. Kazi yake ilikuwa kuzunguka mji wa mpanda akiwa na ngoma yake ambayo kila mtaa akifika alikuwa anaipiga na watu wakikusanyika anawataarifu kuhusu ujio wa bendi.

Kwa mtindo huu bendi ilisafiri kutoka mji mmoja mpaka mwingine. Usafiri ulikuwa wa kila aina, mabasi ya kawaida ya abiria, malori na usafiri mwingine wowote sehemu ambazo kulikuwa na matatizo ya usafiri. 

Kwa mfano mwaka mmoja Vijana Jazz Band tuliwahi kufanya ziara ya mikoa ya kusini chini ya mwaliko wa Jeshi la Magereza Lindi. Maonyesho mawili ya kwanza tuliyafanya kwenye Ukumbi wa Magereza Lindi mjini na kisha kuanza kuzunguka, mkoa wa Lindi na Mtwara kwa kutumia lori la Magereza aina ya Isuzu ‘long base’, humo tulijazana wanamuziki na vyombo vyetu. 

Vumbi, mvua na jua vyote vilikuwa vyetu. Lakini hakukuwa na malalamiko kwani hali halisi ilikuwa ndio ile. Usafiri wa aina hiyo pia ulitukuta tukiwa bendi ya Tancut tulipokuwa wenyeji wa machimbo ya Mwadui ambapo tulisafiri sehemu nyingi kwa kutumia lori aina ya Leyland kufanya ziara hiyo.

Mara nyingi sana bendi hasa za binafsi tulikuwa tukianza safari tukiwa na fedha ya kujikimu siku moja au mbili tu, na kutegemea mapato ya maonyesho kwa matumizi mengine, hili lilikuwa ni jambo la hatari, bendi nyingi zilifia kwenye ziara baada ya mambo huko kutokuenda ilivyotegemewa.

Aprili 12, 1984 ilikuwa Alhamisi, nilikuwa katika bendi ya Orchestra Mambo Bado ambayo ilikuwa inaongozwa na Tchimanga Assossa. Tulikuwa katika moja ya safari za bendi siku hiyo tuliingia mji wa Shinyanga asubuhi na kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha tuliweza kukodisha vyumba viwili tu katika nyumba ya kulala.
 
Chumba kimoja kwa ajili ya wasichana waliokuwa kwenye bendi na kingine kwa ajili ya wanaume. Tulitegemea tungepiga usiku ule ndipo tungepata fedha za kukodi vyumba zaidi. Bahati mbaya siku ile ndipo ilipotokea ajali ambayo ilisababisha kifo cha  Mheshimiwa Edward Moringe Sokoine.
 
Tulipigwa na bumbuwazi kwanza kutokana na kifo hicho, swala la pili likawa tusipopiga siku hiyo, nini hatima yetu? Nakumbuka tulimfuata Afisa Utamaduni kwani ndiye aliyekuwa mwenye uamuzi wa hatma yetu, bahati nzuri akasema hajapata maelekezo yoyote hivyo tukapiga dansi usiku ule, pesa iliyopatikana ikatumika mara moja kwa ajili ya nauli ya kurudi kwetu Dar es Salaam, usiku uleule serikali ilitangaza wiki kadhaa za maombolezo na kati ya mambo yaliyozuiwa yalikuwa maonyesho ya muziki.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *