Dar es Salaam. Alijulikana zaidi kwa jina la Pepe Kalle, lakini jina lake halisi lilikuwa Jean-Baptiste Kabasele Yampanya wa ba Mulanga, alizaliwa tarehe 30 Novemba mwaka 1951 katika jiji la Kinshasa, na katika jiji hilohilo alikuja kufariki tarehe 29 Novemba mwaka 1998.
Pepe Kalle alikuwa mwanamuziki muimbaji. Jina la Kalle alilichukua katika kumpa heshima mkongwe Joseph Kabasele aliyekuwa maarufu kwa kuitwa Grand Kalle. Joseph Kabasele ambaye husifiwa kuwa baba ya muziki wa Kongo alikuwa kiongozi wa kundi lililoitwa African Jazz.
Wakati wa ujana wake Kabasele Yampanya alisoma shule ya St Paul’s Catholic School iliyokuwa Kinshasa, shule ambayo Joseph Kabasele ‘Grand Kalle’ alisoma na katika shule hiyo alipata uzoefu wa awali wa kuimba katika kwaya ya shule, na hivyo alikuja kujipa jina la Pepe Kalle

Pepe Kalle alikuwa mrefu wa zaidi ya futi sita au sentimita mia mbili na alikuwa na uzito wa kilo mia moja na hamsini. Kifupi alikuwa ‘bonge la mtu’, na hata alikuwa pia akijulikana kwa jina la utani la ‘Tembo wa Afrika’.
Pepe Kalle alianza muziki katika bendi ya mtaani kwao iliyoitwa Orchestra Zulu na baadaye akabadili jina na kujiita African Choc.
Baada ya hapo Pepe akajiunga na Orchestra Myosotis ndipo kwa msaada wa mpiga drums wa Afrisa International Seskain Molenga, wakati huo Pepe akiwa na miaka 20 tu , yeye na wenzie wa African Choc wakaingizwa kwenye studio za Verckys na kurekodi nyimbo kadhaa ambazo zilisambazwa zikiwa zimetambulishwa kuwa zilipigwa na kundi la Les Bakuba.
Wanamuziki wote wa African Choc wakajiunga na kundi la Orchestra Bella Bella wakati huo likiwa chini ya Verckys. Pepe Kalle, Nyboma Mwan Dido na wale ndugu Soki Vangu na Soki Dianzenza ndio walikuwa waimbaji bendi hiyo ilipoporomosha vibao vikali kama Sola na Mbuta mwanzoni mwa miaka ya 70.
Nyboma na Pepe Kalle urafiki wao ulianza wakati wakiwa bado wadogo walipokutana kwenye mazoezi ya karate, urafiki wao ulikuja kuendelea mpaka kifo cha Pepe Kalle.
Mwaka 1973, Bella Bella ikiwa chini ya ndugu wawili Soki Vangu na Soki Dyanzenza ikajitoa mikononi mwa Verckys, Nyboma na Pepe Kalle wakabaki na hatimaye kuwa kati ya wanamuziki wa kwanza waliounda kundi la Orchestra Lipua Lipua, lakini baada ya miezi michache Pepe Kalle, Matolu Dode maarufu kwa jina la Papy Tex na Joseph Dilumona maarufu kwa jina la Dilu Dilumona wakamtosa Verckys na kwenda kuanzisha kundi lao la Empire Bakuba.
Kundi hili liliishi kiasi cha miaka 26 na hakika lilikuja kuwa moja ya makundi maarufu sana Afrika. Moja ya sifa kubwa ya kundi hili ni ule umoja waliokuwa nao Pepe Kale, Papy Tex na Dilumona, waliweza kuwa katika bendi hiyo pamoja kwa miaka 25, wenyewe walijiita ‘Trio Kadima’.
Pepe Kale na Papy Tex walianza kufahamiana wakiwa shuleni, Pay Tex alimpeleka nyumbani kwao Pepe Kalle na kumtambulisha kwa mama yake, kumbe hata baba zao walikuwa marafiki, hivyo baada ya kujua hilo, urafiki wao ukakua na kuwa udugu mpaka kifo cha Pepe Kale. Mwaka 1982 Empire Bakuba lilipigiwa kura kuwa ndio kundi bora katika nchi ya Kongo wakati huo ikiitwa Zaire.
Kati ya vibao vingi vya Pepe Kalle, wimbo wa Moyibi ambao aliimba na rafiki yake Nyboma, ulikuja kupandisha sana chati ya Empire Bakuba, wimbo huu ulikuwa unahadithia tabia ya wizi ya mwanamke mmoja ambaye licha ya kuwa kwenye ndoa nzuri, udokozi ulikuwa kilema chake kikubwa, hivyo kumtia aibu yeye mwenye, familia yake na wanawake wote kwa ujumla.
Watanzania wana kumbukumbu ya kudumu ya Pepe Kale kutokana na nyimbo zake mbili, Hidaya ambao uliokuwa una hadithia kuhusu Pepe Kalle na mpenzi wake aliyempoteza Arusha, na wimbo Yanga Afrika ambao ulihusu timu ya soka ya Young Africans.
Pepe Kalle alipata mshtuko wa moyo akiwa nyumbani kwake tarehe 28 Novemba 1998, akakimbizwa kwenye hospitali moja iliyoitwa Ngaliema Clinic. Kesho yake muda mfupi baada ya saa sita usiku Pepe Kalle alirudi kwa muumba wake.
Mwili wake ulipitishwa sehemu kadhaa za jiji la Kinshasa kuwapa watu nafasi ya kumuuaga mpendwa wao. Desemba 6, 1998 Pepe Kalle alizikwa katika makaburi ya Gombe akapewa heshima zote za mazishi ya Kitaifa. Alifariki na kuacha watoto watano. Mke wa Pepe Kalle naye alifariki mwaka 2019.
Mungu amlaze pema Jean-Baptiste Kabasele Yampanya wa ba Mulanga, Pepe Kalle..