Anko Kitime: Mkongwe wa muziki Kongo 

Dar es Salaam. Mwanamuziki Joseph Kabasele maarufu kwa jina la Grand Kalle, kama ilivyokuwa kwa Wakongo wengi kwa agizo la Rais Mobutu alibadili  jina lake na ili lisiwe na majina ya Kizungu naye akaanza  kuitwa Kabasele Tshamala. 

Joseph Kabasele alizaliwa Matadi nchini Kongo Desemba 16, 1930. Familia yake ilikuwa  ya washiriki wazuri wa Kanisa Katoliki,  kaka yake mkubwa alifikia hata kuwa Kadinali katika kanisa hilo.

Joseph alisoma vizuri kwa wakati wake na akaweza hata kumaliza shule ya sekondari na kazi yake ya kwanza ilikuwa ni ukatibu mukhtasi, kazi iliyokuwa kubwa wakati ule, na alifanya kazi hiyo katika kampuni kadhaa za kibiashara.

Lakini rohoni  muziki ulikuwa ukimuita. Bahati ilifika mwaka 1950, katika jiji la Kinshasa wakati huo likiitwa Leopordiville, ilianzishwa studio ya kurekodi muziki iliyoitwa Opika.

Kabasele akajiunga kama mwanamuziki muimbaji  wa studio. Kazi ya wanamuziki wa studio ni kuwasindikiza wanamuziki wanaokuja kurekodi wakiwa hawana kundi kamili au ujuzi wa kutosha, japo wanatungo ambazo zinaonekana ni nzuri.

Pale studio akakutana na wanamuziki wenzie vijana na hatimaye wakaamua kuanzisha kundi lao waliloliita OTC Band, hili jina lilikuja baada ya wao kurekodi tangazo la kuashiria kuanza kwa kituo cha redio kilichopitwa OTC, tangazo lilipendwa na wao wakaona kumbe wanaweza kuwa kundi huru na si wanamuziki wa studio tu.

Katika kundi hilo  pamoja na Joseph Kabasele, ambaye alishaanza kuitwa Kalle alikuweko kijana mdogo mpiga gitaa aliyeitwa Nicholaus Kasanda aliyekuja kujulikana baadaye kama Dr Nico, na kaka yake Nicholaus, Charlie Mwamba, baadaye alikuja kujulikana zaidi kama Dechaud.

Nicholaus alikuwa mpiga solo, na kaka yake akawa mpiga gitaa la ridhim, kuna madai kuwa Dechaud ndiye aliyekuwa muanzilishi wa upigaji wa solo la pili (second solo). Mapema kabisa bendi yao ikatoa vibao  vilivyopendwa sana.

Moja ya nyimbo ambazo bado maarufu mpaka leo ni wimbo Para fifi ambao waliurekodi mwaka 1952, wimbo huo ulikuwa ukimsifia mtangazaji wa redio moja  iliyokuwa ikirusha matangazo kutoka Kongo Brazzaville.

Wimbo wao mwingine maarufu wakati huo  ulikuwa unaitwa Kalekato ambao ulikuwa ni wa mapenzi ukielezea mapenzi kati ya Kalle na msichana aliyeitwa Katherina, na ulikuwa kati ya nyimbo za kwanza saksafon kuanza kutumika.

Nikumbushe hapa kuwa Pepe Kalle alianza kutumia jina la Kalle  kwa kuwa alisoma shule aliyosoma Joseph Kabasele, Grand Kalle , hivyo akaanza kujiita jina la mwamba huyo.

Mwaka 1954, OTC Band ikajipa jina jipya na kuitwa African Jazz. Bendi hii ndio ilikuwa ya kwanza kujiita Jazz. African Jazz haikuwa ikipiga muziki wa Jazz, bali waliiga jina tu kutoka kwa muziki wa Jazz wa Marekani. Mpaka leo bendi nyingi bado zinaendelea kujiita Jazz Band. 

Kabasele na bendi yake walianzisha mtindo mpya wa upigaji wa muziki wa dansi, hivyo bendi nyingi zilianza pia kuiga upigaji huo na kuwa muanzilishi wa rumba la Kongo. Mwaka 1980 umoja wa wanamuziki wa Zaire (UMUZA) ulipitisha azimio la kumuenzi Joseph Kabasele kuwa Baba wa Muziki wa Kongo.

Mwaka 1960 African Jazz ya Kabasele ilitunga wimbo ambao ulikuja kupendwa Afrika nzima, wimbo huu ulitungwa kusherehekea Kongo kupata Uhuru, wimbo huu uliitwa Independence Cha Cha, ulikuwa kama wimbo muhimu kwa kila nchi ya Afrika iliyopata uhuru baada ya hapo.

Bahati mbaya amani katika Kongo haikudumu muda mrefu baada ya kusherehekea uhuru wao, African Jazz wakatunga wimbo waliouita Toyokana Tolimbisana na Congo yaani tuelewane na kusameheana Kongo, ulikuwa wimbo wa kuomba Wakongo kuungana. 

Mwaka huo huo Joseph Kabasele, akaanzisha lebo aliyoiita Surboum African Jazz  na akawa Music Publisher Muafrika wa kwanza nchini Kongo. Mambo yalionekana yanakwenda vizuri sana kwa African Jazz lakini mwaka 1963 kundi la wanamuziki walioongozwa na Tabu Ley na Dr Nico likahama African Jazz na kuanzisha kundi lao la African Fiesta. 

Katika kujaribu kuokoa Jahazi Kabasele akamuita muimbaji nguli Jean Bombenga wa Vox Africa, lakini hawakuweza kufikisha ubora uliokuwa awali na hatimaye mwaka 1969 kundi lilivunjika, japo kwa wapenzi wa African Jazz hukumbuka kipindi hiki kwa kutokana na wimbo mzuri sana ulioitwa BB69. 

Baada ya hapo Kabasele alianzisha kundi aliloliita African Team, ambapo liliwahi kurekodi na wanamuziki kama mpiga saksafon Manu Dibango wa Cameroon, mpiga saksafon Jean Serge Essous kutoka Kongo Brazzaville, mpiga filimbi Don Gonzalo kutoka Cuba, na hakika muziki uliotoka hapo ulikuwa na mahadhi yanayotambulika kama Afro-Latin-Jazz Fusion.

Katika maisha yake Joseph Kabasele aliwahi kuwa rais wa chama cha kukusanya mirabaha cha Kongo kilichoitwa SONECA. Mwanzoni mwa miaka ya 80 akaanza kupata matatizo ya moyo, hatimaye  tarehe 11 Februari 1983 Joseph Kabasele alifariki jijini Kinshasa.