Anko Kitime: Miaka 59 kifo cha Salum Abdallah, nyimbo zake bado zinaishi 

Dar es Salaam. Kwanza kabisa nianze kwa kuomba msamaha kwa makosa mawili yaliyojitokeza katika makala iliyopita ya Simulizi za Muziki.

Kosa la kwanza ni dokezo lililosema, 1992, mwaka ilipoanzishwa Jamhuri Jazz Band’ na kosa la pili ni sentensi iliyosema, ‘katika kuenzi nchi yetu kuwa Jamhuri mwaka 1992’. 

Usahihi ni kuwa ya Jamhuri Jazz Band ilianzishwa mwaka 1955 ikiwa inaitwa Young Nyamwezi Jazz Band, na ilibadili jina na kuwa Jamhuri Jazz Band, kuenzi nchi yetu kuwa Jamhuri mwaka 1962.

Novemba 19 mwaka huu tutatimiza miaka 59 toka mwanamuziki nguli Salum Abdallah alipolazwa kaburini.

Tarehe 18 Novemba, 1965 ilikuwa siku ya Alhamisi, mji wa Morogoro ulikuwa unategemea ugeni mkubwa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na mheshimiwa Rashid Mfaume Kawawa, viongozi wa juu wa nchi wakati huo, walikuwa wakisubiriwa kwa hamu na wananchi wa Morogoro ili kufanikisha sherehe ya  kufungua chuo kikubwa na muhimu kwa maendeleo ya kilimo nchini.

Chuo cha Kilimo Morogoro, chuo ambacho kwa sasa kinajulikana kama SUA (Sokoine University of Agriculture). Pamoja na wageni hao pia alitegemewa kuweko Mbunge wa Morogoro mjini wakati huo Mheshimiwa Oscar Kambona.

Katika kukamilisha shamra shamra za siku hiyo bendi mbili kubwa za pale Morogoro mjini, Cuban Marimba Band iliyokuwa ikiongozwa na Salum Abdallah Yazidu aliyependa kujulikana kwa kifupisho cha majina yake yaani SAY, na bendi nyingine kubwa pale Morogoro, Morogoro Jazz Band, zilipangwa kufanya maonyesho ambayo yalipangiwa kutembelewa na viongozi hao wakuu wa nchi.

Kwanza ilikuwa heshima kubwa sana kwa wanamuziki, na kutokana na ushindani mkubwa wa bendi hizo, wanamuziki  na washabiki wa bendi hizo walikuwa roho juu kusubiri mpambano wa usiku huo muhimu katika historia ya mji wa Morogoro.

Siku hiyo Cuban Marimba Band walikuwa wamepangiwa kupiga  muziki katika ukumbi wa Community Center, wakati wenzao Morogoro Jazz Band walikuwa wapige katika ukumbi mwingine sehemu za  Kichangani.

Kwenye muda wa saa kumi na mbili jioni baada ya shamrashamra za mchana za  kupokea viongozi kumalizika,  Ramadhan Mdidi aliyekuwa msaidizi wa mmoja wa madreva wa malori ya Salum Abdallah alikuja kumueleza  tajiri wao kuwa, moja ya gari lake limenasa kwenye mchanga katika mkondo wa mto walikokuwa wakichimba mchanga, kwa hiyo ilikuwa busara kuliondoa gari usiku uleule maana kama mvua ingenyesha gari lingeweza kuzolewa na maji, Salum Abdallah akaagiza gari hilo likavutwe. 

Salum Abdallah pamoja na kuwa mwanamuziki, pia alikuwa na malori ya kubeba mchanga na wakati huo alikuwa na tenda ya kubeba mchanga kwa ajili ya mradi wa kujenga nyumba za National Housing pale Morogoro.

Salum akamtuma mwanamuziki wake Waziri Nyange atangulie kwenye ukumbi ambako wangepiga muziki ili kutayarisha vyombo  kwa onyesho la usiku, na yeye akaenda na lori jingine kwenda kuvuta gari lililonasa kwenye mchanga.

Kiasi cha saa moja hivi kijana mmoja aliokuwemo kwenye lori lililoondoka na Salum Abdallah alirudi mbio nyumbani Salum Abdallah na kuwataarifu ndugu kuwa kumetokea ajali na Salum ameumia.

Ajali hiyo ilikuwa ya ajabu na kwa miaka mingi baadaye ilikuwa kichwa cha habari cha mazungumzo kwa wapenzi wa muziki wa Cuban Marimba Band. 

Kwa maelezo ya waliokuwepo, giza lilikuwa limekwisha ingia na wakati lori alilokuwemo Salum Abdallah lilipokaribia Msamvu, taa za gari zilizimika ghafla, dereva akapoteza muelekeo na gari likayumba na kugonga kijiukuta pembeni mwa barabara, lakini taa zikawaka tena kiasi cha wasaidizi waliokuwemo nyuma kwenye lile lori kuanza kucheka, lakini kicheko chao kilikatika ghafla baada ya kugundua kuwa mlango wa upande aliokuwa amekaa Salum ulikuwa wazi naye amedondoka.

Walirudi nyuma na kumkuta akiwa kalala barabarani akiugulia kwa maumivu. Wakati huohuo Mzungu mmoja akiwa na gari dogo, alipita na kuwachukua watu wawili toka kwenye lile lori, mmoja akaenda nyumbani kwa Salum kutoa habari na mwingine akaenda kuchukua taxi iliyokuja kumchukua majeruhi na kumkimbiza hospitali. 

Alipofikishwa hospitali  madaktari walimtaka Salum anyooshe mikono na kisha miguu alipoweza, wakaamini hajavunjika bali ni maumivu ya juu juu ambayo yangeisha, kiasi cha kumruhusu arudi kwake na awahi matibabu kesho yake asubuhi.

Enzi hizo teknolojia ya X Ray ilikuwa bado adimu.  Salum akawaamuru wenzie wasipige  dansi siku ile, wengi wakakesha naye nyumbani kwake.

Usiku kucha ulikuwa wa maumivu makubwa, asubuhi mgonjwa alipelekwa hospitali akafanyiwa upasuaji ikagundulika alivunjika kiuno na mfupa mmoja  ukawa umepasua kibofu , jambo ambalo kutokana na kuchelewa kugundulika lilikuwa ni baya sana.

Kama saa 7 mchana alitolewa chumba cha upasuaji na wenzie waliokuwa wakisubiri wakaambiwa waende makwao wakale vizuri ili waje baadaye kutoa damu kwa ajili ya mgonjwa. Wakatoka kwa furaha wakijua mambo yatakuwa mazuri.

Walielekea kwenye klabu yao wakatengeneza chakula na kula kwa furaha. Kulianza hata kuwa na utani mmoja wao akisema, “Mwarabu akipona atatoa kibao  kikali cha tukio hili”.  Baba yake Salum alikuwa Mwarabu, rafiki wa Salum walikuwa na kawaida ya kumuita Salum ‘Mwarabu’.

Kwa bahati mbaya sana ilipotimu saa kumi jioni taarifa ya kusikitisha zikawafikia kuwa Salum amefariki. Watu wakaanza kumiminika nyumbani kwake, wakakuta hata maiti imeshafikishwa kwake na imewekwa katika chumba kimoja ambacho Salum alikuwa amekitayarisha kwa ajili ya frame ya duka. 

Kuna hadithi inayosimulia kuwa baada ya Salum kujulikana kuwa kafariki, Daktari Mkuu wa Mkoa aliendesha gari lake hadi nyumbani kwa Salum na kuliegesha pembeni ya nyumba na kuanza kulia jambo ambalo mara moja ndugu walielewa kuwa mambo yameharibika.

Hivyo waliweza kutayarisha  sehemu hiyo ambayo iliwezesha watu kuja  kuona mwili wa Salum kwa mara ya mwisho. Haikuchukua muda habari zilisambaa mjini Morogoro na kukawa na hekaheka kiasi cha ulinzi wa polisi kuhitajika kutokana na wingi wa watu waliokusanyika nyumbani kwa kipenzi chao Salum Abdallah.

Kesho yake hali ilizidi kuwa ngumu zaidi wakati wa kusindikiza maiti kwenda makaburini, ilikuwa kama kila mtu alikuwa akitaka japo aguse kidogo jeneza la Salumu ili kumuaga, ililazimu kikosi cha polisi cha kutuliza ghasia, FFU, kitumike kuleta amani.

Jeneza la Salum liliweza kubebwa kutoka Nunge nyumbani kwa mama yake hadi Msamvu kwenye eneo alipozikwa, watu wakiwa wamejipanga mstari mrefu kupokezana jeneza, pamoja na marehemu kuwa na magari mengi hakukutumiwa gari. Wapenzi walipokezana mwili mpaka makaburini.

Wimbo wa Salum Abdallah alioutunga muda mfupi kabla ya kifo chake, ulileta tafsiri nyingi na hasa kutokana na namna kifo chake kilivyotokea. Maneno machache ya wimbo huo yalisema hivi;
E Mola wangu E Mola wangu,
Nivue na ya dunia,
Hao walimwengu, hao walimwengu ,
 Wanitafuta kwa madawa,
Wataka wadhulumu roho yangu,
Wapate furahiwa,
Nami natoa salamu zangu,
Ningalimo mu dunia,
Kwa ndugu na jamaa zangu
Za mapenzi na furaha
Za kuwatoa uchungu
Ajali itakaponifikia
Nahadithi ndugu zangu,
Nyuma waliobakia,
Kubeba maiti yangu
Huku wakinililia
Nitamshtakia Mungu
Nilotendwa mu dunia.
MOLA AMLAZE PEMA SALUM ABDALLAH YAZIDU