
Congo. ‘Le Intrepide Bavon Marie’ ndio lilikuwa jina la albumu ya mwisho ambayo Bavon Marie Marie alishiriki, album hiyo ilitolewa mwezi Machi mwaka 1970, ndani yake kulikuwa na nyimbo zifuatazo.
Upande A: i. Maseke ya meme ii. Bilambambongo ya nani, iii. Nalimbisa Bijou na Upande B, ulikuwa na nyimbo zifuatazo i. Libanga na libumu 1, ii. Libanga na libumu 2. iii, Nakata swear ya bolingo.
Maseke ya meme na Libanga na libumu zote zilikuwa ni tungo za Bavon Marie Marie na zilihusu ushirikina. Maseke ya meme au pembe za kondoo ilihusu binti aliyekuwa akilalamika kuwa kalogwa, wimbo ulikuwa na maneno yafuatayo, “Balongola ngai motema, batia ngai motema ya soso mpo nakoma lokoso nasilisa mibali.
Ndoki mpe akufaka, kisi mpe epolaka. Malamu boboma ngai nakufu nalembi ngai mwana ya moto” tafsiri yake ikiwa ni “Wachawi wametoa moyo wangu wamebadilisha na moyo wa kuku ili niwe nalala na wanaume hovyo.
Mchawi hufa, na ulozi hupotea, heri waniue nimechoka”
Libanga na libumu au jiwe tumboni, ilikuwa nayo ni tungo iliyohusu mwanamke aliyedai haolewi tena na amekuwa malaya kwa kuwa wamemloga na kumuwekea jiwe tumboni ili asizae, heri angekufa. Miezi minne baada ya kutoka album hii Bavon alifariki katika ajali ya gari, hadithi kubwa ikawa, tungo zake za kufakufa zilikuwa zikitabiri kifo chake. Bavon alifariki katika ajali Agosti 5, 1970.
Bavon Luambo Siongo, mdogo wake Franco Luambo Luanzo Makiadi alizaliwa tarehe 27 Mei, 1944. Baada ya kifo cha baba yao Bavon akiwa bado mdogo analelewa na mama yao, akaanza kuonyesha nia ya kuwa mwanamuziki.
Kaka yake hakutaka mdogo wake aingie kwenye maisha ya muziki kwani maisha yalikuwa magumu na jamii iliwachukuliwa wanamuziki kama watu walioshindwa maisha.
Franco akampeleka mdogo wake kusoma jimbo la Bas-Congo, lakini mvuto wa gitaa ulikuwa mkubwa kuliko mvuto wa kusoma, uamuzi wa Bavon kung’ang’ania magitaa badala ya shule ukamfikia Franco kupitia binamu yao mmoja, Franco alikasirika sana lakini pamoja na kumtisha mdogo wake, Bavon akang’ang’ania kuwa katika maisha yake lengo lake ni kuwa mpiga gitaa.
Mwaka 1961, Bavon akiwa na miaka 17 aliamua kutoroka kwao na kwenda kuendeleza ndoto zake za muziki, kundi lake la kwanza lilikuwa ni Orchestre Jamel na baada ya hapo zikafuata bendi kadhaa zikiwemo Cubana Jazz, alipokuwa pamoja na muimbaji aliyekuja kuwa maarufu sana Bumba Massa, baada ya hapo likafuatia kundi la Orchestre Jamel, na hatimaye akajiunga na kundi la Negro Success.
Kundi la Negro Success lilianzishwa mwaka 1960 na Vicky Longomba ambaye awali alitengana na mwanamuziki wa OK Jazz ya Franco. Vicky Longomba alipokuja kupatana na Franco akarudi OK Jazz, Leon Bholen akawa kiongozi mpya wa Negro Success, na katika kipindi hicho ndipo Bavon alipojiunga na kundi hilo.
Bavon aliyekuwa sasa akijulikana kama Bavon Marie Marie akiwa na mwenzie Leon Bholen Bombolo wakaja kuwa wapenzi wa vijana wapenda muziki katika Jiji la Kinshasa.
Kati ya wanamuziki wengine waliopitia bendi hiyo ya Negro Success walikuwa ni wapiga saksafon Empompo Loway, Andre Menga na Moro Maurice, waimbaji walikuwa Zozo Amba, Singer Gaspard “Gaspy” Luwowo , Tshimanga Assosa na Nyboma Mwandido, Hubert “Djeskin” Dihunga, mpiga gitaa la ridhim alikuwa Jean Dinos, mpiga gitaa la bezi alikuwa Alphonse ‘Le Brun” Epayo, na mpiga drums alikuwa Samy Kiadaka.
Tarehe 5 Agosti mwaka 1970, ilitokea ajali iliyochukua maisha ya Bavon Marie Marie kijana wa miaka ishirini na tano tu aliyekuwa ndio kwanza anaanza kupata umaarufu.
Mpaka leo kuna hadithi nyingi kuhusu aina ya ajali, wengine wakisema aligonga lori la jeshi lililokuwa limeegeshwa pembeni ya barabara, sababu ikiwa ni ulevi, wengine wakisema ajali ilitokana na hasira za kugombana na kaka yake, Franco Luambo, baada ya kuhisi alikuwa na mahusiano na mpenzi wake. Kulikuwa hata na tuhuma kuwa Franco alimtoa kafara mdogo wake ili apate umaarufu zaidi.
Franco ni wazi alikuwa na majonzi makubwa kwani kwa muda aliacha kabisa kupiga muziki kutokana na kifo cha ndugu yake. Franco aliwahi kutunga wimbo ulioitwa Kinsiona, katika wimbo huo alihadithia jinsi alivyoumizwa na kifo cha mdogo wake.