Anguko la kimaisha kwa wasanii Bongo linaanzia hapa

Dar es Salaam, Unaweza kusema sanaa bila ubunifu ni sawa sifuri, maisha ya usanii yanahitaji bunifu zenye athari chanya kwa jamii kwa lengo la kuendelea kukuza majina na kazi zao kwa ujumla. 

Katika kutafuta athari hizo hupelekea baadhi ya wasanii kujitengenezea utofauti katika mambo mbalimbali, ikiwemo maisha binafsi, ya usanii na hata jinsi ambavyo wasanii hao uonekana kwenye jamii.

                     

Wengi wanaita kulinda brandi, yaani hapo ndipo wasanii hutengeneza picha kwa jamii kuwa wao ni watu wenye maisha mazuri, wasioijua njaa, shida wala taabu. Huku picha zao zikiwa zimepambwa mbele ya magari ya kifahari, pamba kali na hata majengo ya maana.

Licha ya kufanya hayo kwa mlengo wa kukweza kazi zao, huku wengine wakiwa tayari wameingiza sokoni kazi nyingi zenye kuvuma mjini, maswali huibuka kwa mashabiki pale ambapo msanii akipatwa na matatizo, kwani baadhi yao hurudi kwa mashabiki kuomba misaada, huku wengine wakigeuka maudhui kwa mapaparazi wakieneza picha zao wakiwa wametupiwa vyombo nje kwenye nyumba za kupanga baada ya kukosa kodi.

Hapo ndipo akili za mashabiki hucheza na kugundua kuwa yapo wanayoishi mitandaoni hayana uhalisia kwenye maisha yao na badala yake baadhi yao huangukia kwenye maisha duni licha ya kuwa ngoma zao hukita kwenye spika za bei mbaya na kwenye kumbi ambazo watu huponda mali wakiamini kufa kwaja.

                          

Pamoja na hayo inaonekana uduni wa maisha siyo tu tatizo binafsi bali ni alama ya udhaifu wa mfumo mzima kiwanda cha burudani. 

Akizungumza na Mwananchi mtayarishaji wa muziki nchini Joachim Kimario Master Jay amesema sababu kubwa inayosababisha  baadhi ya wasanii kuishia kwenye maisha duni licha ya kufanya kazi nyingi za sanaa ni kutokuwa na elimu.

“Sisemi elimu ya darasani, kuna muziki kama sanaa, wengi wanashindwa kuelewa kuwa sanaa ni biashara, muziki unaweza kukutoa kwenye sifuri ukawa na hela nyingi na mara nyingi inatokea kwa watu ambao hawana elimu na hata Marekani ni watu wa kawaida siyo ambao wamesoma mpaka chuo kikuu.

“Sasa changamoto ipo hapo mtu alikuwa wa kawaida anakipaji, anafahamika na anatengeneza hela nyingi lakini wengi wanasahau kama ukiwa mwanamuziki wewe ni kama bidhaa, wachache wanadumu kwa miaka kumi wakiwa wanajulikana wanasahau kama kuna siku watachokwa, wanashindwa kuwekeza,” amesema.

                         

Amesema kwa nchi zilizoendelea mbali na mameneja wanaosimamia kazi za wasanii wapo wengine wanaosimamia fedha za wasanii na hao wanakuwa watu wawili tofauti jambo ambalo nchini hakuna.

Aidha kwa upande wake Rita Poulsen ambaye ni muandaaji wa shindano la kusaka vipaji la (BSS) amesema wasanii siyo wafanyabiashara wao ni kwa ajili ya sanaa tu na siyo kujisimamia kama ambavyo nchini wamekuwa wanafanya.

“Mungu amemuumba msanii kufanya sanaa siyo kusimamia pesa, wanaofanya vizuri wanawasimamizi ambao wanasimamia mapato yao na kuwekeza, kwa hiyo sisi Tanzania hakuna meneja wazuri wengi wanawatafuta wasanii wakiwa tayari wame-hit,”amesema

Licha ya hayo amesema changamoto nyingine ni usumbufu wa wasanii kwani mara nyingi huonekana wakivunja mikataba hivyo majukwaa ya kutoa elimu kuhusiana na hilo yanahitajika ili kuwafanya wawe na heshima.

Naye mwanamuziki Webiro Wassira ‘Wakazi’ ameiambia Mwananchi kuwa pesa siyo kila kitu kwani wapo wasanii ambao wanaimba kwa ajili ya kutunza utamaduni 

“Kila kazi na kila taaluma ina watu ambao wamefanikiwa, wengine kawaida na wengine hawajafanikiwa ni kama kwenye muziki. Lakini pia utajiri na umasikini haupimwi kwenye pesa. Sanaa ni ajira na burudani kuna watu wanafanya ngoma za asili hawafanyi kwa ajili ya kuwa mabilionea.

“Uhalisia muziki ni kama kazi nyingine, kufanya tu haijitoshelezi kuwa na pesa nyingi au tajiri lakini waliotengeneza pesa kupitia muziki ni wale waliotumia jina kuweza kufanya biashara nyingine.

“Ila ni wachache sana wale ambao wimbo umesikilizwa wakaingiza pesa wengi wanatumia majina kufungua biashara ambayo itasaidia kuingiza kipato hapo ndiyo linakuja jambo jingine je kuna elimu ya biashara?”, ameeleza

Ameongezea kuwa baadhi ya wasanii hawana elimu ya kujiongeza na kutafuta pesa upande wa pili wengi wanasahau kama umaarufu huisha.

“Mikataba hata iwe mizuri vipi siyo kama itafanya utajirike lakini kama hauna uelewa wa mambo mengine na uwekezaji huwezi kutajirika. Wakati mwingine utajiri siyo kila kitu ni namna ambavyo umewezaje kuigusa jamii,”amemalizia Wakazi

Hata hivyo, akitolea ufafanuzi suala hilo Dk Herbert Makoye ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TASUBA), amesema kwa sasa wasanii wameanza kubadilika badala yake baadhi wanawekeza kwa ajili ya kupata pesa nje ya muziki.

“Zamani sanaa ilikuwa hailipi kwa sababu ilikuwa inaitwa burudani na siyo biashara lakini kwa sasa inaanza kuchukuliwa kama biashara, nyuma ulikuwa unamuona msanii anatembea na CD zake kwenye baa mwenyewe.

“Kwa hiyo hapo unaona anatafuta hela ya kula tu lakini kwa sasa mwelekeo tunaanza kuuona baadhi ya wasanii wanaanza kuwekeza sehemu nyingine. Mimi ninachoweza kusema mtazamo unabadilika na wapo wanaonekana wameanzisha biashara”, amesema.

Walichosema BASATA

Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji na Maendeleo ya Sanaa, Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Edward Buganga, amesema sababu kubwa inayosababisha baadhi ya wasanii kuishia kwenye maisha duni licha ya kufanya kazi nyingi za sanaa ni ukosefu maadili

“Ukitaka kujua tabia ya mtu mpe pesa, kikubwa ni maadili na ndiyo maana kama Baraza tumetengeneza mwongozo wa maadili ambao unafanya asikosee. Pia tumetengeneza fursa nyingi kama wanasheria ambao wasanii wanaruhusiwa kuja kupata ushauri bure.

“Kwa hiyo mambo mengine ni tabia za wasanii, kama Baraza tunawajibu mkubwa sana wa kuendeleza sana na kusimamia kukuza vipaji na tunafanya hivyo. Ili kuepukana na hayo. Kwa sasa somo la sanaa linafundishwa kuanzia shule ya msingi hadi vyuo vikuu. Na bahati nzuri tulishirikishwa kwenye hiyo mitaala.

Anasema kupitia taaluma wanaamini wasanii watakuwa na misingi mizuri katika kulinda maslahi yao na uchumi wanaopata ili uwasaidie wao na vizazi vyao vijavyo.

Walichosema COSOTA

Kutokana na janga hilo  Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Haki Miliki Tanzania (Cosota), Doreen Sinare ameeleza kuwa wasanii wengi hawawekezi kwenye vitu vya kuendelea kuwaingizia mapato na hawajiungi  na bima za afya na mifuko ya huduma za jamii.

“Wengine wanasaini mikataba ambayo inawafaidisha mwanzo zaidi na baadaye inakua haiingizi kipato. Pia kutokurasimisha kazi husika (kujisajili na kusajili kazi za ununifu) na kutokuwa na elimu au kudharau kutekeleza masuala ya ulinzi wa kazi hadi pale tatizo linapojitokeza,”ameeleza.

Amesema wao Cosota wanatoa elimu, misaada kwa baadhi ya wasanii au waandishi pamoja na ushauri wa kisheria bila gharama yoyote, pia wanasaidia katika migogoro ya hakimiliki na pale ambapo mgogoro unashindikana kesi ikienda mahakamani wao wanakua mashahidi katika kesi hiyo.