
Nchi ya Angola, imetangaza kujiondoa rasmi kama mpatanishi wa mzozo wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kupitia kiongozi wake, rais Joao Laurenco.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Angola imetoa tangazo hilo siku ya Jumatatu, kupitia ukurasa wa facebook, uamuzi ambao nchi hiyo inasema, ni kwa sababu rais Laurenco kwa sasa ni Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, majukumu yatakayomzuia kuendelea na kazi ya upatanishi.
Rais Lourenco amekuwa katika mstari wa mbele, kujaribu kupatanisha pande zinazozana Mashariki mwa DRC, ikiwa ni kupanga mazungumzo ya moja kwa moja kati ya serikali ya Kinshasa na waasi wa M23 wanaosaidiwa na Rwanda.
Mazungumzo hayo yalikuwa yaanze wiki iliyopita jijini Luanda, lakini yaligonga mwamba, baada ya waasi wa M 23 kujiondoa kwa kulalamikia baadhi ya viongozi wake kuwekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya.
Kumekuwa na jitihada mbalimbali za Kimataifa, kutatua mzozo wa Mashariki mwa DRC kwa njia ya mazungumzo, wakati huu waasi wa M 23 wakipuuza wito wa usitishwaji vita na kuendelea kuchukua maeneo kadhaa, kama mji wa Walikale, wiki iliyopita.
Kujiondoa kwa Angola, kuwa mpatanishi kunaacha maswali kuhusu ni nchi gani itachukua kazi ya upatanishi kuhusu mzozo wa DRC, hasa baada ya rais Felix Tshisekedi na Paul Kagame, wiki iliyopita kukutana na kufanya mazungumzo ana kwa ana jijini Doha nchini Qatar.