
Thibilisi. Rais wa zamani wa Georgia, Mikhail Saakashvili amehukumiwa kifungo cha miaka tisa jela kwa ubadhirifu wa mali ya Umma.
Mamlaka za Georgia zilimkamata Saakashvili Oktoba 2021 alipoingia kwa siri nchini humo akitokea uhamishoni Ukraine wakati wa uchaguzi na kumshutumu rais huyo wa zamani kwa matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu wa fedha na makosa mengine aliyodaiwa kuyafanya wakati wa uongozi wake.
Akiwa gerezani, Saakashvili amekuwa akilalamika mara kwa mara kuhusu hali yake mbaya ya kiafya.
Kituo cha televisheni cha Georgia, Mtavari Arxi, kimeripoti Jumatano kuwa Saakashvili amepatikana na hatia ya kufuja dola milioni 3.2 (zaidi ya Sh8.4 bilioni) fedha za serikali katika kesi inayojulikana kama “kesi ya suti na mashada ya maua.”
Aliyekuwa mkuu wa usalama wa rais huyo, Teimuraz Janashia, pia alikutana na hatia huku akitozwa faini ya Lari 3,000 (takriban dola 1,000).
Saakashvili kwa mara ya kwanza alishtakiwa kwa ubadhirifu w fedha za umma mwaka 2014.
Waendesha mashitaka walisema wakati wa urais wake, alitumia fedha za serikali kununua suti, makoti, saa na vitu vingine kwa matumizi yake binafsi.
Pia alishtakiwa kwa kutumia fedha za umma kulipia elimu ya mtoto wake, kufanyiwa upasuaji wa urembo, kukodisha magari ya kifahari na ndege.
Agosti 2008, Saakashvili aliwaagiza wanajeshi wa Georgia kuivamia Jamhuri iliyojitenga ya South Ossetia, jambo ambalo lilisababisha mgogoro wa kijeshi na Russia, baada ya walinda amani wa Russia waliokuwa kwenye eneo hilo kushambuliwa.
Urais wake pia unakumbukwa kwa ukandamizaji mkali wa maandamano dhidi ya serikali.
Saakashvili alikimbia nchi baada ya kipindi chake cha uongozi kumalizika. Mnamo 2015, alipewa uraia wa Ukraine na kuteuliwa kuwa Gavana wa Mkoa wa Odessa na Rais wa wakati huo, Pyotr Poroshenko.
Hata hivyo, alidumu kwenye wadhifa huo kwa mwaka mmoja pekee kabla ya kujiuzulu, akiwatuhumu viongozi wa Ukraine kwa ufisadi.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.