Amuua nduguye kwa shoka wakigombania ugali

Kakamega, Kenya. Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Reuben Lutaboni (42) ameripotiwa kumuua mdogo wake Michael Lukala (40) kwa kinachodaiwa kupishana kauli juu ya kiasi cha ugali walichotakiwa kukipika.

Tukio hilo limetokea katika Kijiji cha Kilimani Kaunti ya Kakamega nchini Kenya, kama lilivyoripitiwa na tovuti za Jambo Radio na Tuko.

Kwa mujibu wa kaka yao mkubwa, Peter Lukala, wadogo zake waliingia kwenye mzozo huo wakati wakipika ugali baada ya kutoka kwenye kazi ya kuchimba kisima.

Lukala amesema wadogo zake hao walipishana kauli kutokana na kiasi cha ugali uliokuwa unapikwa, ambapo Lutaboni anadaiwa alichukua shoka na kumshambulia mdogo wake Lukala, hali iliyosababisha kifo chake.

Mama mzazi wa Michael na Reuben amesema alijaribu kuingilia kati ugomvi huo, lakini alizidiwa nguvu na Reuben.

Mama huyo amesema Reuben alikuwa na nguvu zaidi na alifanikiwa kumfukuza kutoka ndani ya nyumba na kumfungia nje.

“Walikuwa wakishikana mashati kwenye shingoni. Nililia kuomba msaada lakini hakuna aliyekuja kutusaidia. Nilizunguka kutafuta mtu wa kusaidia, lakini sikumpata yeyote, niliwekwa nje ya nyumba wakati Reuben alipokuwa akimshambulia ndugu yake,” amesema mama huyo.

Kufuatia tukio hilo, mzee mmoja katika kijiji hicho, Cleophas Barasa ametoa wito kwa watu kutatua tofauti zao kwa njia zifaazo kuliko mapigano.

“Mambo kama haya ya chakula haistahili ndugu kupigana mpaka mwingine anaua mwenzake kwa sababu ya chakula na alitahadharisha vijana wenye umri wa miaka 40 kuishi pamoja ni hatari.

Mzee Barasa pia amekemea maisha ya ndugu hao watatu waliokuwa wakiishi nyumba moja, akisema walipaswa kuwa huru na kila mmoja kujitegemea.

Amesema ni hatari kwa kuwa hakuna mtu anayeweza kutabiri hatua au mipango ya mwenzake, hivyo ni vyema waishi kila mmoja kwenye mji wake.