Rombo. Mzee mwenye umri wa miaka 82, mkazi wa kijiji cha Kilema, kata ya Olele, wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro, anadaiwa kumuua na kumzika mwanaye, Oscar Msamanga (42), kufuatia ugomvi uliodaiwa kuzuka baada ya Msamanga kuvaa koti la baba yake bila idhini.
Tukio hilo la kusikitisha lilifichuka Aprili 29, 2025, baada ya mzee huyo kutoa kauli ya kushtua hadharani wakati wa sherehe kijijini, akidai kuwa alimuua mwanaye na tayari alikuwa amemzika kwenye shimo alilolichimba pembeni mwa nyumba yao.
Mwandishi wa habari hii, alifika katika eneo la tukio na kushuhudia polisi wakifukua mwili wa marehemu, ambapo baada ya kufukuliwa ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Karume kwa ajili ya taratibu za uchunguzi zaidi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, akieleza kuwa mauaji hayo yalitokea Aprili 27, huku mwili wa marehemu ukigundulika Aprili 29 na kufukuliwa Aprili 30 baada ya kukamilika kwa taratibu za kisheria.
“Ni kweli tukio hili limetokea katika Kijiji cha Kilema, Mzee huyu na marehemu walikuwa wakiishi pamoja na walikuwa na mgogoro, inadaiwa kuwa chanzo cha tukio ni kitendo cha kijana huyo kuvaa koti la baba yake, jambo lililomghadhabisha mzee huyo,” amesema Kamanda Maigwa.
Aidha, Kamanda Maigwa amesema kuwa kufuatia ugomvi huo, mzee huyo alimpiga mwanaye kichwani kwa kutumia rungu hadi kusababisha kifo, kisha akausitiri mwili wa marehemu kwenye shimo alilochimba karibu na nyumba yao.
“Baada ya kukamatwa, alikiri kutekeleza mauaji hayo na aliongoza polisi hadi eneo alikozika mwili wa mwanaye,” amesema Kamanda Maigwa
Kamanda Maigwa amesema, mtuhumiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea.
Wasimulia tukio la mauaji lilivyogundulika
Akisimulia tukio hilo la mauaji lilivyogundulika, mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, Shadrack Massawe amedai Aprili 29, 2025 wakiwa kwenye sherehe kijijini hapo, Mzee huyo aliropoka kumuua kijana huyo na ndipo viongozi waliokuwepo kwenye eneo hilo walifuatilia na kubaini ukweli.
“Juzi tulikuwa na sherehe ambayo Oscar (marehemu) ndio alikuwa muhusika kwenye hiyo sherehe Aprili 29 baba yake akawa anapiga stori kuhusu Oscar, wakati huo watu walimuuliza Oscar yuko wapi? akasema aah mimi nishamuua huyu kijana bana, nimemzika sehemu fulani,” amedai mwananchi huyo.
Amedai; “Bahati nzuri kwenye hiyo sherehe alikuwepo ofisa mtendaji wa kijiji wakaandamana pamoja balozi na mwenyekiti kwenda nyumbani kwake na walipofika huyu mzee alionyesha sehemu ambayo amemfukia kijana wake.”
Mwananchi huyo amedai kijana huyo alikuwa akiishi vizuri na watu na kwamba alikuwa akipendwa na kila mtu kijijini hapo kutokana na shughuli zake za kujitafutia maisha.
“Oscar alikuwa sio mtu mwenye kuchukua kitu cha mtu, alikuwa anapendwa na kila mtu kwa sababu akiamka asubuhi anashughulika na shughuli zake za kawaida za kujitafutia riziki,” amesema mwananchi huyo
Naye, Balozi wa mtaa aliokuwa akiishi marehemu, Matern Tesha amelaani tukio hilo na kusema ni tukio la kinyama na kwamba halipaswi kufanywa na binadamu.
“Tukio hili ni la kinyama na halipaswi kufanywa kwa nchi yetu, huyu mzee kafanya tukio la ajabu sana, nimesikitika sana kuona huyu ndugu yetu kuuawa kikatili hivi, imetuumiza,”amesema Balozi huyo
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Modesti Kimario amedai baada ya kuchunguza wamebaini inaonekana Mzee huyo na kijana wake walikuwa hawaelewani.
“Nimechunguza hili tukio, ni kwamba huyu mtoto na baba yake walikuwa na bifu siku nyingi walikuwa hawaelewani, na mpaka tukio hili la mauaji linatokea ugomvi ulikuwa ni koti, kwa kweli ni tukio la kusikitisha na la kinyama mno,” amedai mwenyekiti huyo.

Amedai tukio kama hilo linapaswa kukemewa kwa nguvu zote kwa kuwa ni tukio baya na halipaswi kutokea kwenye jamii.
Mmoja wa ndugu wa marehemu, Prisila Swai amesema tukio hilo limewaumiza kama familia na kitendo kilichofanywa na baba mdogo wao ni cha kikatili.