Amri ya Trump yang’ata, MDH yapeleka wafanyakazi likizo

Dar es Salaam. Taasisi ya Management and Development for Health (MDH) imetangaza likizo isiyo na malipo kwa wafanyakazi wa mradi wa afya jumuishi nchini Tanzania kufuatia agizo la kusitisha kazi, huku Serikali ikitoa ufafanuzi wa upungufu utakaotokea.

Leo Jumatano, Februari 12, 2025 Mwananchi imeiona barua iliyosainiwa jana Jumanne Februari 11 yenye maelekezo hayo kutoka kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Dk David Sando.

Barua hiyo imeelekezwa kwa wakuu wa mikoa, wakurugenzi wa halmashauri, wakurugenzi wa hospitali, waganga wafawidhi wa hospitali za mikoa na wilaya na hospitali maalumu.

“Kama ilivyoelezwa katika mawasiliano ya awali kuhusu makubaliano haya ya ushirikiano, kwa mujibu wa Amri ya Rais (Donald Trump) kuhusu tathmini na urekebishaji wa misaada ya kigeni ya Marekani, shughuli zote zinazohusiana na fedha za PEPFAR zilisitishwa.

“Ikijumuisha shughuli zilizofanyika chini ya mikataba midogo na kandarasi ndogo, wakati wa kipindi cha tathmini ya siku 90 kilichoagizwa katika amri hiyo,” imeeleza barua hiyo.

Barua hii inalenga kutoa muhtasari rasmi wa marekebisho ya muda katika utekelezaji wa miradi, katika maeneo kadhaa ikiwemo ombi la likizo ya hiari bila malipo.

“Tunaomba kila mfanyakazi wa mradi awasilishe ombi la likizo ya hiari isiyolipwa haraka iwezekanavyo, lakini si zaidi ya mwisho wa siku ya leo (Februari 11).

“Likizo hii ya hiari isiyolipwa itaanza rasmi kwa muda wa siku 90, kuanzia Februari mosi hadi Mei mosi 2025, au hadi tutakapopokea maelekezo zaidi kutoka kwa mfadhili kuruhusu kuendelea kwa utekelezaji wa mradi, lolote litakalotangulia,” imesema barua hiyo.

Pamoja na hayo imefafanua na kusisitiza kuwa hatua hiyo ya muda si ya kupunguza wafanyakazi au kusitisha ajira; bali ni hatua muhimu na ya tahadhari ya kusimamia majukumu ya kifedha kwa uwajibikaji, huku MDH ikisubiri kurejelewa kwa ufadhili.

Vilevile, barua hiyo imetoa taarifa kwa mamlaka husika, ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Mfumo wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB) kuhusu mabadiliko hayo, ili kuepusha adhabu yoyote inayoweza kutokea kutokana na kutolipa au kuchelewa kwa malipo.

Pamoja na hayo barua hiyo imewaelekeza wafanyakazi wote kutozungumza na vyombo vya habari.

“Hakuna mfanyakazi yeyote anayeruhusiwa kuzungumza na vyombo vya habari kwa niaba ya mkuu wa mradi, isipokuwa kwa idhini maalumu kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa MDH.

“Tunathamini uelewa na ushirikiano wenu katika kipindi hiki kigumu. Tunatambua kujitolea kwenu kwa dhamira yetu na tumejizatiti kuwahabarisha kila hatua kadri hali inavyoendelea kubadilika,” imeeleza barua hiyo.

Kauli ya Serikali

Alipoulizwa na Mwananchi Mkurugenzi Idara ya Tiba, Wizara ya Afya nchini Tanzania, Dk Hamad Nyembea amesema tayari uchambuzi umeshafanyika kuhusu upungufu utakaotokea na tayari vituo vimeshafanya marekebisho kwa kuangalia mbadala.

“Kama ni hospitali, kituo cha afya, wameshaangalia maeneo ambayo yatakuwa na upungufu na kufanya mtawazo wa watumishi wale ambao wameajiriwa na Serikali, ili waweze kujaza hizo nafasi huduma zisitetereke,” amesema.

Kufuatia hilo amesema Serikali haitegemei kama kutakuwa na shida, huduma zitaendelea kutolewa kama kawaida na haitegemei changamoto.

“Serikali mwaka huu wa fedha iliajiri watumishi wengi na miaka miwili iliyopita, hili limetokea kipindi ambacho tayari kuna ajira mpya, hawa wengine walikuwa wanaongeza nguvu,” amesema.

Alipoulizwa iwapo upungufu huo utaleta mzigo kwa watumishi watakaobaki vituoni, Dk Nyembea amesema:

“Mzigo unakuwepo ndio, lakini vituo vinajipanga vizuri sehemu ambazo watumishi wapo wengi zaidi vimewapeleka sehemu zenye watumishi wachache, hili ni suala ambalo Serikali italibeba,” amesema.

Alipoulizwa nini Serikali inafanya ili kuhakikisha huduma haziyumbi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Ofisi ya Waziri Mkuu, kazi, vijana, ajira na wenye ulemavu, Ibrahim Hamidu amesema:

“Sisi tupo kuhakikisha stahiki za watumishi zinashughulikiwa kwa mujibu wa mikataba, suala la huduma itakuwaje linashughulikiwa na Tamisemi pamoja na Wizara ya Afya. MDH tunashirikiana naye katika masuala ya vijana, masuala ya uzazi na afya yapo chini yao,” amesema Hamidu.

MAT yatoa angalizo

Hatua hiyo imeleta sintofahamu kwa kuwa maelfu ya watumishi wa afya kwenye sekta nyeti kama maabara, huduma za VVU (CTC) kifua kikuu, wauguzi na baadhi ya madaktari walikuwa chini ya shirika hilo.

Kwa mujibu wa Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania MAT, Dk Mugisha Nkoronko, maelekezo hayo yataitikisa sekta ya afya kwa kuwa baadhi ya wataalamu walio kwenye vituo vya afya mijini na vijijini wanategemea mishahara kutoka mashirika yanayopata ufadhili kutoka Marekani, ikiwemo MDH.

Amesema licha ya watumishi wanaofanya kazi moja kwa moja kwenye mashirika hayo na asasi za kiraia, asilimia kubwa ni watumishi waliopo katika sekta ya afya walioajiriwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya umma, mishahara yao inatoka katika shirika hilo.

Amewataja wanaoibua wagonjwa kwenye jamii, wahamasishaji wa jamii kupima VVU na watoa huduma ngazi ya jamii.

“Kuna madaktari, wauguzi wameajiriwa vituo kadhaa, ustawi wa jamii, wataalamu wa maabara, maofisa miradi wanaofanya tathmini ya miradi, wahasibu, wanaoshughulika na ugavi, wafanyakazi kada ya kati ya tiba, matabibu na wengine wengi,” amesema.

Amesema karibu kila kada kwenye afya ilipata nafasi ya kufanya kazi kwenye miradi mbalimbali inayohusishwa na USAID au PEPFAR.