Amri mpya ya Putin na kuongezeka uwezekano wa kutumiwa silaha za nyuklia

Rais Vladimir Putin wa Russia Jumanne, Novemba 19, alitia saini amri ambayo inaipa Moscow ruhusa ya kutumia silaha za nyuklia dhidi ya “nchi isiyo na silaha za nyuklia” ilimradi nchi hiyo iwe inaungwa mkono na nguvu za nyuklia.

Maamuzi hayo yamechukuliwa sambamba na kutimia siku ya 1,000 ya oparesheni za kijeshi za Russia nchini Ukraine, na inakuja siku moja baada ya Washington kuiruhusu Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu ya kilomita 300 ya ATACMS ya Marekani dhidi ya shabaha mbalimbali katika ardhi ya Russia. Uamuzi huo wa Marekani ilikaribishwa na Umoja wa Ulaya na nchi za Ufaransa na Uingereza ambazo pia zimeiruhusu Ukraine kutumia makombora yazo ya anga ya masafa marefu kuishambulia shabaha ndani ya ardhi ya Russia.

Jumatatu tarehe 18 Novemba, Russia iliutaja uamuzi wa Rais Joe Biden wa Marekani wa kuiruhusu Ukraine itumie makombora ya masafa marefu ya Marekani dhidi yake kuwa ni ya “kutowajibika” na kuonya kuwa Moscow italipiza kisasi dhidi ya hatua kama hiyo. Rais Putin alisema mwezi Septemba uliopita kwamba hatua ya nchi za Magharibi ya kuiruhusu Kiev itumie makombora ya masafa marefu dhidi ya Russia ina maana ya kushiriki moja kwa moja nchi za NATO katika vita vya Ukraine dhidi yake. Hii ni kwa sababu kiutendaji miundombinu ya kijeshi na maafisa wa NATO watahusika katika kulenga na kurusha makombora yaliyotajwa dhidi ya Moscow.

Rais Vladimir Putin wa Russia

Kremlin ilitangaza mapema jana Jumanne kwamba, mabadiliko yamefanyika katika sera za nyuklia za Russia na kuwa yatarasimishwa ikilazimu kufanya hivyo. Jambo hili bila shaka linaonyesha wasiwasi mkubwa  wa Moscow kuhusu uamuzi wa hivi karibuni wa Marekani kuhusiana na mashambulizi ya makombora ya masafa marefu ndani ya ardhi ya Russia. Dmitry Peskov, Msemaji wa Kremlin amesema kuhusiana na suala hilo kuwa kurasimishwa sera hizo kunapaswa kuchukuliwa na nchi zisizo rafiki kuwa ujumbe mzito.

Vladimir Putin, katika mkutano wake na wajumbe wa Baraza la Usalama la Russia mnamo Septemba 25 mwaka huu, alisisitiza juu ya nafasi ya sera za nyuklia katika kudhamini usalama wa Russia na kupendekeza kuwa sera hizo ziendane na hali halisi ya sasa na kwa kuzingatia kuongezeka vitisho kutoka nje. Putin amebainisha kuwa kwa mujibu wa hati  nyukli ya Russia silaha za nyuklia zinapasa kutumika tu kama chaguo la mwisho la kulinda utawala na ardhi ya nchi. Amesema nguvu za nyuklia pia zinatumika pale nchi isiyo ya nyuklia inapotumiwa na madola ya nyuklia kufanya mashambulizi dhidi ya Shirikisho la Russia.

Russia, ambayo sasa inakabiliwa na uchokozi wa NATO na Marekani kwa njia ya msaada mkubwa wa kijeshi kwa Ukraine na vilevile usaidizi wa kijasusi na kutumwa vikosi vya Magharibi kusaidia Kyiv, haina chaguo jingine isipokuwa kuongeza nguvu zake za kimkakati na kujitayarisha kwa silaha za nyuklia kwa ajili ya kukabiliana na adui ili kulinda usalama na ardhi yake. Kuhusu suala hilo, Vladimir Putin amesisitiza mara kwa mara juu ya udharura wa kuongezwa nguvu za kawaida za kijeshi za nchi hiyo, na pia kuimarisha silaha zake za kimkakati za nyuklia kama mbinu muhimu ya kuzuia mashambulizi ya adui.