Manchester, England, Mambo yameanza kuwa mabaya kati ya mshambuliaji wa Manchester United Marcus Rashford na kocha wake Ruben Amorim.
kuanzia Amorim ametua kwenye timu hiyo mshambuliaji huyo raia wa England amekuwa hana uhusiano mzuri na kocha huyo na sasa amekuwa akifanya mazoezi tu lakini kwenye mechi anawekwa jukwaani, huku mara mwisho kuitumikia United ikiwa Desemba mwaka jana.
Basi kocha wao, Amorim ameibuka na kupiga nyundo nyingine kali zaidi baada ya kusema kwamba ni bora amweke benchi kocha wake wa makipa kama mchezaji wake wa akiba kuliko Rashford.

Rashford aliwekwa kando na kocha Amorim kwa mara nyingine kwenye mechi ya juzi Jumapili wakati Man United ilipoichapa Fulham 1-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, shukrani kwa bao pekee la beki wa kati, Lisandro Martinez uwanjani Craven Cottage.
Kocha huyo Mreno alipoulizwa kwanini hamtumii Rashford alisema haonyeshi juhudi zozote mazoezini na kwamba kocha wa makipa mwenye umri wa miaka 63, Jorge Vital anastahili zaidi kuwekwa kwenye benchi kama mchezaji wa akiba kuliko fowadi huyo Mwingereza.
“Nitamweka Vital kwenye benchi mbele ya mchezaji ambaye kila siku hana juhudi zozote. Sitabadilika kwenye hilo eneo. Siku zote itakuwa sababu ileile. Sababu ni mazoezini. Kwa namna ninavyoona mchezaji anavyofanya mazoezini, kwenye maisha yake, kila siku. Kama vitu havibadiliki, basi nami sitabadilika.

“Kitu hicho kipo kwa kila mchezaji kama unafanya ziada, kama unafanya vitu sahihi, tutamtumia huyo mchezaji. Unaweza kuona kwenye benchi letu hapa. Tulihitaji kasi, kujaribu kuweka udhibiti wa mipira ya kutenga hivyo ndivyo nilivyoamua.”
Rashford amekuwa kwenye mipango ya kunaswa kwa mkopo na klabu za Borussia Dortmund, Monaco na AC Milan, licha ya kwamba mwenyewe anapendelea zaidi kwenda kukipiga kwa miamba ya Nou Camp.
Mara ya mwisho Rashford kuichezea Man United ilikuwa Desemba 12 kwenye ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Viktoria Plzen na hajawahi kuwa kwenye kikosi tangu kwenye mechi ya kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Newcastle United, Desemba 30 mwaka jana.

Baada ya ushindi wa juzi Jumapili, Rashford aliposti kwenye ukurasa wake wa Instagrama aliposema: “Hongereni kwa ushindi vijana.”
Bao la mpira wa kubabatiza la beki Martinez kwenye dakika 78 liliisaidia Man United kupanda hadi nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Lakini, mashabiki walimgeukia mmiliki mwenza wa timu hiyo, bilionea Sir Jim Ratcliffe, ambaye alikuwapo jukwaani Craven Cottage walipokuwa wakiimba: “Ni kama Glazer tu, Jim Ratcliffe ni …”.
Tajiri Ratcliffe amepandisha bei ya tiketi uwanjani Old Trafford kwa Pauni 66, Desemba zikiwemo za watoto. Bilionea Ratcliffe anajaribu kupandisha mapato ya Man United ili kwenda sawa na kanuni za mapato na matumizi endelevu. Na kuhusu usajili, kocha Amorim alisema “Nahitaji msaada kuboresha timu”.
Wakati Amorim akimweka mbali kabisa na kikosi chake mchezaji Rashford, matumaini yake kwenye wachezaji wa safu ya ushambuliaji ipo kwa Joshua Zirkzee na Rasmus Hojland. Kwenye mchezo wa Fulham, Amorim alianza na Hojlund.
Staa huyo wa zamani wa Atalanta ameichezea Man United kwenye mechi 48 za Ligi Kuu England tangu alipotua klabuni hapo mwaka 2023.