Amorim atambiana na Guardiola Manchester dabi

LONDON, ENGLAND: MechiI tano zilizopita. Manchester United imeshinda mbili, Manchester City imeshinda tatu. Jumapili, kinapigwa tena.

Kasheshe lipo huko Old Trafford, huku vikosi vyote vya mahasimu hao wa Manchester derby zikiwa kwenye viwango duni msimu huu. Nani atamtambia mwenzake?

Kwenye takwimu za jumla za miamba hiyo, katika michuano ya Ligi Kuu England, Man United na Man City zimekutana mara 55.

Kwenye mechi hizo, mara tisa zilimalizika kwa sare, lakini Man United imeshinda 26, mara 12 ilipocheza nyumbani kwenye Uwanja wa Old Trafford na mara 14 ilipoifuata Man City kwake uwanjani Etihad.

Kwa upande wa Man City, yenyewe imeshinda 20. Mara 11 ilipocheza nyumbani Etihad na tisa ilipoifuata Man United huko Old Trafford. Safari hii itakuwaje huko Old Trafford.

Kocha wa Man City, Pep Guardiola aliweka wazi kwamba anahitaji kumaliza ligi ya msimu huu kwa kukamatia tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Kwa maana hiyo, atahitaji kushinda ugenini huko Old Trafford katika kipute hicho cha mahasimu. Hata hivyo, atacheza mechi hiyo bila ya huduma ya straika wake wa mabao, Erling Haaland, ambaye ni majeruhi.

Kocha wa Man United, Ruben Amorim anapambana kushinda mechi hiyo ili kurudisha hali ya kujiamini kwenye kikosi baada ya kupoteza mchezo uliopita ilipokipiga na Nottingham Forest. Man United haina inachokitafuta kwenye mchezo huo zaidi ya kulinda tu heshima yake kwenye mechi dhidi ya mahasimu wao.

Mechi nyingine za Jumapili kwenye Ligi Kuu England, Brentford itakuwa nyumbani kucheza na Chelsea, wakati Liverpool kwenye msako wao wa pointi za kuwasogeza kwenye ubingwa watakwenda ugenini Craven Cottage kucheza na Fulham. Kwenye takwimu, Fulham na Liverpool zimekutana mara 35 kwenye Ligi Kuu England, huku saba zilimalizika kwa sare na wakali wa Anfield wakiwa watawala wa mechi hizo, wakishinda 21, mara 11 walipocheza nyumbani na 10 walipokwenda kukipiga Craven Cottage. Fulham yenyewe imeshinda saba tu, tano nyumbani na mara mbili ilipoifuata Liverpool kwao.

Tottenham Hotspur inayojikongoja itakuwa nyumbani kukipiga na Southampton katika moja ya mechi zinazosubiriwa kwa hamu kutokana na kubeba hatima ya wengi, akiwamo kocha wa Spurs, Ange Postecoglou.

Kwenye namba, Spurs na Southampton zimekutana mara 49 kwenye Ligi Kuu England, tisa zilimalizika kwa sare, huku Spurs ikishinda 26, mara 18 nyumbani na nane ugenini, wakati Southampton imeshinda 14, mara 10 nyumbani na nne ugenini.

Jumatatu kutakuwa na mchezo mmoja tu, ambapo Leicester City ya kocha Ruud van Nistelrooy itakuwa nyumbani King Power kukipiga na Newcastle United ya straika, Alexander Isak.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *