
Licha ya timu yake kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Leicester City jana, Ijumaa, meneja wa Manchester United, Ruben Amorim amedai kuwa bao la pili walilofunga kwenye mchezo huo halikuwa halali.
Beki Harry Maguire alifunga bao hilo kwa kichwa katika dakika za majeruhi akiunganisha krosi ya Bruno Fernandes.
Hata hivyo bao la Maguire limegeuka mjadala kwanj picha za marudio zimeonyesha kuwa beki huyo alikuwa ameotea wakati akifunga.
Pengine bao hilo lingekataliwa ikiwa teknolojia ya video ya usaidizi kwa marefa (VAR) ingekuwa inatumika kwenye mechi hiyo.
Amorim alisema kwa kifupi kuwa matokeo hayo ni mazuri kwake ingawa haamini kwamba bao la Maguire walistahili kupewa.
“Pasipo kuweko na VAR, sio goli. Nadhani ni muhimu sana kuwa na VAR kwa sababu inaleta uungwana kwenye mchezo. Ni ngumu kupoteza kama vile kwa mchezo. Lakini tunahitaji. Lakini tulistahili kupata bahati kidogo,” alisema Amorim.
Nyota wa zamani wa Man United, Roy Keane alisema uamuzi huo ni matokeo ya marefa kutotimiza wajibu wao.
“Ni uamuzi wa ovyo sana. Mshika kibendera alipaswa kuona. Unatakiwa kutoa maamuzi sahihi,” alisema Keane.
Nyota wa zamani wa Arsenal. Ian Wrights alisema kuwa kama bao hilo lisingekubaliwa, ingekuwa na maana kubwa kwa Leicester City ambayo kwa sasa inanolewa na mchezaji wa zamani wa Man United, Ruud Van Nistelrooy.
“Ingesaidia kwa kiasi kikubwa wachezaji kujenga hali kubwa ya kujiamini. Lakini wanatakiwa wajipandishe wao wenyewe kwa sababu ya marefa,” alisema Wrights.