Amorim afungua milango Alejandro Garnacho

Manchester, England. Kocha wa Manchester United, Ruben Amorim ameacha wazi milango ya kupokea ofa ya kumpiga bei winga Alejandro Garnacho kwenye dirisha hili la uhamisho wa Januari huku Chelsea ikiripotiwa kuweka ofa yake ubaoni.

Staa huyo wa kimataifa wa Argentina amekuwa akihusishwa na klabu za Napoli na Chelsea zinazohitaji huduma yake katika dirisha hili la Januari.

Kocha, Amorim amefichua hilo juu ya hatima ya Garnacho baada ya kuishuhudia Man United ikiichapa Rangers kwenye Europa League.

Ripoti zinafichua kwamba juzi Alhamisi, Chelsea ilipeleka ofa rasmi ubaoni kwa ajili ya kumsajili Garnacho na imeonyesha dhamira ya dhati ya kunasa saini ya mchezaji huyo baada ya Napoli kuhamishia nguvu yao kwa winga wa Borussia Dortmund, Karim Adeyemi.

Chelsea ilipeleka ofa yake ya awali wiki iliyopita ikihitaji huduma ya staa huyo wa Man United kwa ada ya pauni 65 milioni, huku Garnacho, 20, akipata nafasi ya kucheza kwa dakika 90 zote katika mchezo wa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Rangers kwenye Europa League.

Napoli ilipeleka ofa huko Man United inayodaiwa kuwa kati ya pauni 45 milioni hadi Pauni 50 milioni, lakini sasa imehamishia mipango yake kwa mchezaji Adeyemi na kinachoonekana ni kwamba itahitaji kusajili winga mmoja tu kwenye dirisha la mwezi huu.

Mawakala wa Garnacho, Carlos Cambeiro na Quique de Lucas walikuwapo katika mechi kati ya Chelsea na Wolves, Jumatatu iliyopita kwenda kuanzisha mazungumzo ya kumpeleka mteja wao huko Stamford Bridge.

Na baada ya ushindi dhidi ya Rangers uwanjani Old Trafford juzi Alhamisi, ambapo Garnacho alianzishwa na kucheza kwa dakika zote na mashabiki wa Man United kuimba wimbo wa jina lake, kocha Amorim amefunguka juu ya hatima ya mchezaji huyo.

“Sifahamu nini kitakwenda kutokea,” alisema na kuongeza. “Acha tuelekeze akili kwenye timu kwanza na wachezaji waliopo.

“Hatufahamu nini kitatokea hadi hapo dirisha litakapofungwa. Chochote kinaweza kutokea.”

Amorim aliongeza: “Nimewekeza akili kwenye mechi na yeye yupo hapa, ni mchezaji wa Manchester United. Alikuwa mchezaji muhimu kwetu kwenye hii mechi ya leo, hivyo tusuburi kuona siku zijazo. Nadhani amekuwa akiboresha kiwango chake baada ya mechi. Alikuwa vizuri leo alipocheza ndani na alipocheza nje, alikuwa akibadili nafasi uwanjani, alionekana kuboresha makali yake. Ninachofanya mimi ni kuwasaidia wachezaji, lakini wao wanapaswa kufanya kazi zao.”

Kikiwa kipaji kilichokuzwa kwenye akademia ya Man United, kuuzwa kwa Garnacho kutaipa faida kubwa timu hiyo katika kuweka sawa vitabu vyao vya kipesa kuendana na kanuni za PSR, ambayo inaweza kuibana Man United endapo kama itashindwa kukamatia tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Chelsea imeripotiwa kutanguliza ofa ya pauni 60 milioni, ambayo itakuwa na nyongeza nyingine ambazo zinaweza kulifikisha dau hilo hadi kwenye pauni 65 milioni na Garnacho anaonekana kuwa tayari kwa uhamisho huo. Na gwiji wa Man United, Rio Ferdinand amekiri kwamba kwa mtindo wa uchezaji wa kikosi cha Amorim unamfanya Garnacho kuondoka kwenye kikosi hicho cha Old Trafford.

“Nadhani mashabiki wanapaswa kufahamu wazi. Wanaimba nyimbo za jina lake na hiyo ilikuwa hisia zao. Wanampenda, wanamzungumzia sana, ndio maana wanamuimba sana,” alisema Ferdinand na kuongeza. “Siku zote amekuwa akicheza soka la moja kwa moja, lakini nadhani mfumo wa sasa unakwenda kinyume. Amorim hapendi kuchezesha mawinga wanaochezea pembeni tu. Anataka mawinga wa kuingia ndani. Hicho kitu Garnacho hakiwezi.