
Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za binadamu la Amnesty International, limeiitaka serikali ya Mali kufanya uchunguzi kuhusiana na mauaji ya raia wanane, wakiwemo watoto wadogo waliouawa katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani.
Mauaji hayo yalitokea kufuatia mashambulizi ya droni kaskazini mwa nchi hiyo ambako jeshi linapambana na makundi ya waasi wenye misimamo ya kufurutu ada na makundi ya wanaotaka kujitenga.
Taarifa ya Amnesty International imeeleza kuwa, mashuhuda waliripoti kwamba takribani raia wanane, wakiwemo watoto sita, waliuawa katika mashambulizi ya anga kwenye soko lenye shughuli nyingi katika kijiji cha Inadiatafane, eneo la Timbuktu, mnamo Oktoba 21.
Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa, kkwa akali watu wengine 15 walijeruhiiwa katika mkasa huo.
Shirika hilo la kutetea haki za binaadamu pia limesema, shambulizi hilo linapaswa kuchunguzwa kama uhalifu wa kivita kwa sababu lilisababisha vifo na majeruhi miongoni mwa raia huku miundombinu ya kiraia pia ikilengwa katika tukiio hilo.
Mali inakabiliwa na harakati za makundi yanayotaka kujitenga, na tangu mwaka 2012 imekuwa ikikumbwa na mgogoro mkubwa wa mashambulizi ya umwagaji damu ya makundi ya kigaidi yenye mfungamano na Al-Qaeda na Daesh, pamoja na magenge ya wahalifu.