Amissi Tambwe aibukia Singida Black Stars

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Yanga na timu ya taifa ya Burundi, Amissi Tambwe ameajiriwa kuwa meneja wa Singida Black Stars akichukua nafasi ya Freddy Chalamila.

Tambwe aliyewahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara katika misimu ya 2013/2014 na 2015/2016 ameingia Singida Black Stars pamoja na kocha msaidizi Juan Carlos Oliva kutoka Hispania.

Ingizo hilo la Tambwe na Oliva limetangazwa na Singida Black Stars leo Februari 19, 2025.

“Tunapenda kuwataarifu mashabiki na wapenzi wa Singida Black Stars SC kuwa tumefanya maboresho kwenye Benchi la Ufundi kwa kumuongeza Kocha Juan Carlos Oliva (MAGRO) kutoka Hispania kuwa Kocha
Msaidizi 1.

“Timu itaendelea kuwa chini ya Kocha David Ouma huku Muhibu Kanu sasa ni Kocha Msaidizi 2.

“Wakati huo huo, tumefanya mabadiliko madogo kwenye Benchi la Ufundi kwa kumuongeza Amissi Jocelyn Tambwe kuwa Meneja wa Timu na Fredy Chalamila amehamishiwa nafasi ya Mratibu Mkuu wa
Timu zetu zote. Tunawapongeza wote na kuwatakia kila la heri katika majukumu yao,” imefafanua taarifa hiyo ya Singida Black Stars.

Tambwe amewahi kuzitumikia klabu tatu tofauti za Tanzania akiwa mchezaji ambazo ni Simba, Yanga na DTB (sasa Fountain Gate).

Akiwa Simba na Yanga alifanikiwa kuibuka mshindi wa tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu kwa nyakati mbili tofauti.

Akiwa na DTB, Tambwe aliibuka mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza ambayo sasa inajulikana kama Championship.