Amerika ya Kusini chini ya shinikizo kuchagua kati ya Marekani au China

Amerika ya Kusini imekuwa uwanja wa vita kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na China, chini ya shinikizo kutoka Washington kuchagua kambi yake.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Utawala wa Trump hadi sasa unatumia vitisho na ushawishi katika mkakati wake wa kukabiliana na ushawishi unaokua wa China katika eneo hilo, ambao unaona kuwa tishio kwa usalama na uchumi wa taifa la Marekani.

Donald Trump ametishia mara kwa mara “kurudisha” Mfereji wa Panama uliojengwa na Marekani ikiwa Panama haitapunguza ushawishi wa China kwenye njia ya maji, ambayo inachangia asilimia 40 ya usafirishaji wa kontena za Marekani.

China pia ni lengo lisilo la moja kwa moja la ushuru ambao Rais Trump ametangaza kwa chuma na aluminium kutoka nchi washirika kama vile Mexico.

Ikulu ya White House inasema makampuni ya uzalishaji ya China yanatumia vibaya makubaliano ya biashara huria ya Amerika Kaskazini, USMCA, (United States-Mexico-Canada) kusafirisha aluminium hadi Marekani kupitia Mexico bila ushuru. China imelaani mawazo ya “Vita Baridi”, ikiishutumu Marekani kwa kutumia “shinikizo na shuruti kudhalilisha na kudhoofisha” uwekezaji wake katika Amerika ya Kusini.

“Hakuna shaka kwamba utawala wa Trump unaona uwepo wa China katika Amerika kama tishio kwa usalama wa taifa na masilahi ya sera ya kigeni,” Arturo Sarukhan, ambaye aliwahi kuwa balozi wa Mexico nchini Marekani kutoka mwaka 2006 hadi 2013, ameliambia shirika la habari la AFP.

“Hii  kimsingi ndiyo inaelezea uonevu wa kidiplomasia wa Rais Trump dhidi ya Panama, sera yake ya biashara ya ‘Marekani Kwanza’ … na vitisho vyake vya kuhalalisha USMCA,” ameongeza.

– Ushindani mkali –

Marekani imedai Amerika ya Kusini kama sehemu ya nyanja yake ya ushawishi kwa karne mbili.

Lakini China imefanya mafanikio katika kanda hiyo. Theluthi mbili ya nchi za Amerika ya Kusini zimejiunga na mpango wake wa miundombinu ya “Belt and Road”, na China imeipiku Marekani kama mshirika mkubwa wa kibiashara wa Brazili, Peru, Chile na nchi nyingine kadhaa katika eneo hilo.

Wasiwasi wa mara moja wa utawala wa Trump unaonekana kuzingatia ushawishi wa China karibu na nyumbani, haswa huko Panama na mshirika mkubwa wa kibiashara wa Marekani, Mexico.

Uwekezaji wa China nchini Mexico umeongezeka kwa kiasi kikubwa tangu muhula wa kwanza wa Trump (2017-2021), wakati makampuni katika sekta zilizolengwa na ushuru wa Marekani zilihamisha sehemu za hifadhi zao za usambazaji hadi Mexico.