Amani ya kweli haiji bila haki- Askofu Chambala

Unguja. Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kiteto, Isaya Chambala amesema amani ya kweli haiji bila haki, huku akiwataka viongozi wanapohubiri amani kukumbuka kutenda haki.

Askofu Chambala amesema hayo leo Aprili 20, 2025 katika mahubiri wakati wa ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika Kanisa la Anglikana Mkunazini, Unguja.

“Amani ya kweli haiji bila haki, pale penye dhuluma, unyanyasaji, ubinafsi haiwezi kuwapo amani. Lazima tuhakikishe unapotafuta amani yako, tafuta amani ya wengine bila kuleta ubaguzi na kufanya dhuluma,” amesema.

Amesema wakati Taifa likielekea kwenye uchaguzi mkuu Oktoba, mwaka huu wananchi wajitokeze kwa wingi kuchagua viongozi wenye maadili.

“Tujitokeze kupiga kura kwa amani, ninaamini kura yako ni takatifu kwa sababu ina uamuzi wa Mungu ndani yake, kwa hiyo usiposhiriki unazuia mpango wa Mungu katika kusudio la kumpata mtu anayefaa,” amesema.

Amesema: “Tunapaswa kuchagua viongozi waadilifu na waaminifu, mimi si mwanachama wa chama chochote, mtu analetwa na chama huyo lazima tumuangalie kwa uadilifu wake.”

Amevitaka vyama ambavyo vimepewa jukumu kikatiba la kuteua wagombea, kuleta watu ambao ni waadilifu na wananchi watumie nafasi yao kusema ndiyo au hapana kwenye boksi la kura.

Amevitaka vyombo vinavyosimamia uchaguzi vitimize wajibu wao wa kulinda haki za wananchi bila upendeleo wala rushwa.

“Yesu alifufuka ili tuwe huru, tuishi kwa haki na tuwe vyombo vya amani. Pasaka iwe mwanzo wa maisha mapya binafsi, familia na kwa Taifa zima. Yesu Kristo ameleta amani na waumini ni wajumbe wa kusambaza amani hiyo, hivyo tuwe mstari wa mbele katika kukamilisha hili,” amesema.

Amesema Tanzania ni nchi ya amani na utulivu lakini lazima itegemee misingi ya kuidumisha kama ilivyoasisiwa na viongozi wa kwanza Julius Nyerere na Abeid Aman Karume.

Askofu wa Kanisa la Zanzibar International Christian Center (ZICC), Donath Kaganga amewataka wananchi na viongozi kuendesha uchaguzi wa haki na amani.

Katika kuthibitisha hilo amesema tayari wametoa kitabu cha mwongozo wa uchaguzi wa amani.

Amesema kila Mzanzibari ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa ila wanataka uchaguzi ufanyike kwa amani.

Amewaasa vijana ambao mara nyingi wanatumika kueleza mambo ambayo yanaweza kusababisha fujo.

“Tunawaasa vijana waende katika mikutano kwa lengo la kusikiliza sera na siyo kufanya fujo, unapotumika kuharibu amani watakaoathirika siyo chama fulani wala dini fulani ni watu wote,” amesema.

Amesema kawaida ya risasi haichagui dini, kabila wala chama cha siasa.

“Tuelewe kuwa maisha yetu ni sawa na kuku wa kienyeji hatuwezi kula hadi tutoke ndio tule, ikitokea vurugu hali itakuwa ngumu kwetu sote,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *