Amaan ndiyo tumaini jipya la Simba Afrika

Amaan ndiyo tumaini jipya la Simba Afrika

Dar es Salaam. Hekalu la soka la Benjamin Mkapa limebakia kimya kama msitu uliokosa ndege wa asubuhi. Sauti za mashabiki, kelele za midundo, na wimbi la rangi nyekundu sasa hazitafika tena huko Mei 25. Fainali ya Simba dhidi ya RS Berkane imeondoka kama upepo wa ghafla, ikavuka bahari, na kutua Zanzibar kwenye uwanja wa Amaan.

Ni habari iliyoingia kama radi katikati ya jua la saa sita mchana. Mashabiki wamejawa na mshangao, wengine wamebaki kimya, wengine wakijawa na maswali yasiyo na majibu. Lakini katika ukimya huo, kuna sauti moja ikilia kwa upole na matumaini.

Zanzibar si tu kisiwa cha mapenzi na mashairi bali sasa ni kisiwa kinachoandaa jukwaa la historia mpya ya soka la Tanzania na Afrika.

Uwanja wa Amaan, wenye nyasi zinazong’ara kwa kijani kibichi cha matumaini, unakuwa chumba kipya cha vita kwa Simba na sehemu ya kuandika rekodi mpya. Wengine watasema si nyumbani lakini ardhi ya Tanzania haijawahi kuwageuka watoto wake, kumbuka Simba walichofanya kwenye uwanja huo wiki kadhaa zilizopita ilipovaana na Stellenbosch.

Simba wameshateseka kwenye ardhi ya Morocco. Mabao mawili ya Berkane yamewaumiza, lakini hayajamaliza ndoto ya Wekundu wa Msimbazi ambao sasa wanapumua kwa hewa ya bahari ya Hindi, wakijua kuwa mbele yao si tu wapinzani bali pia nafasi ya kusahihisha yaliyopita.

Amaan inaweza kuwa kama jua la jioni linalozama kwa hadithi yenye mshangao mkubwa. Mashabiki wa Simba wanaweza kuligeuza kuwa moto wa upendo. Kuanzia Mlandege hadi Forodhani, Mangapwani hadi Chake Chake sauti ya Simba itasikika kama wimbi la baharini.

Katika soka, si kila kilichopangwa hufanyika. Na mara nyingine, ushindi huja pale ambapo hakuna aliyeutarajia. Simba hawahitaji miujiza, wanahitaji moyo, umoja, na mshikamano wa damu moja kutoka pande zote za muungano.

Amaan si mwisho wa historia ya Simba Afrika. Bali ni ukurasa mpya unaoenda kufunguliwa. Labda ndiyo mahali ambapo historia ya Simba itapigwa muhuri wa dhahabu. Labda ni huko, chini ya mbalamwezi ya Zanzibar, ndipo Simba itaunguruma kwa mara ya mwisho kwa nguvu, kwa fahari, na kwa ushindi.

Kuna furaha kubwa kwa Simba kutua na kombe bandarini na kuanza maandamano ya kulitembeza kombe jijini Dar es Salaam, hakuna jambo ambalo Simba imeshindwa kwenye aridhi hii linapokuja suala la soka la kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *