Alkhamisi, tarehe 7 Novemba, 2024

Leo ni Alkhamisi tarehe 5 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 7 Novemba 2024.

Siku kama ya leo, miaka 1,438 iliyopita kulijiri vita vya Mu’utah, baina ya jeshi la Waislamu na jeshi la Roma na waitifaki wake.

Vita hivyo vilitokea baada ya mjumbe aliyekuwa ametumwa na Mtume (saw) huko Sham kwa ajili ya kulingania dini ya Kiislamu, kuuawa shahidi na askari wa kulinda mpaka wa eneo hilo. Baadhi ya wanahistoria wanasema kuwa, miongoni mwa sababu zilizomfanya Mtume (saw) kutuma jeshi la wapiganaji 3,000 kukabiliana na utawala wa Roma katika eneo hilo ni kuuawa shahidi walimu 14 wa Qur’ani Tukufu waliokuwa wametumwa na Mtukufu Mtume katika maeneo ya mpakani ya Sham.

Katika vita hivyo Mtume alimteua Jaafar bin Abi Twalib, mtoto wa ami yake, kwa ajili ya kuongoza jeshi la Kiislamu, na akawateua Zaid bin Haritha na Abdullah bin Rawaaha kwa ajili ya kukaimu nafasi hiyo.

Jeshi la Kiislamu ambalo lilikuwa limechoka kutokana na kwamba ilikuwa mara ya kwanza kwenda safari ndefu kama hiyo, lilipambana na jeshi la Roma na wapiganaji wa kikabila katika eneo la Mu’utah, magharibi mwa Jordan ya leo ambapo liliwapoteza viongozi wote watatu wa jeshi hilo la Kiislamu. Hatimaye Waislamu walimpa jukumu la kuongoza jeshi hilo Khalid Bin Walid ambaye ndiye kwanza alikuwa amesilimu, ambapo naye alitoa amri ya kuwataka Waislamu kurudi nyuma. Japokuwa jeshi la Kiislamu halikushinda vita hivyo, lakini liliweza kusoma mbinu za jeshi la adui, hatua ambayo ilikuwa utangulizi wa ushindi dhidi ya jeshi hilo la adui katika vita vya baadaye.

Siku kama ya leo miaka 1441 iliyopita alizaliwa Bibi Zainab (s.a) binti mtukufu wa Imam Ali bin Abi Twalib na Bibi Fatimatu Zahra (as).

Bibi Zainab alikuwa mashuhuri miongoni mwa watu kutokana na maarifa na elimu kubwa aliyokuwa nayo. Katika tukio la Karbala, Bibi Zainab (s.a) alisimama kidete na kukabiliana na dhulma za watawala dhalimu na ujahili watu wa zama hizo ili kutimiza malengo matukufu ya kaka yake, Imam Hussein (a.s). Bibi Zainab alipelekwa Sham pamoja na mateka wengine wa Nyumba Tukufu ya Mtume (saw) baada ya mapambano ya Imam Hussein (a.s) huko Karbala.

Hotuba za Bibi Zainab mbele ya majlisi ya Ibn Ziyad mtawala wa Kufa na katika ikulu ya Yazid bin Muawiya huko Sham zilikuwa na taathira kubwa katika kufichua dhulma na ukandamizaji wa Bani Umayya na kuonesha jinsi Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume walivyodhulumiwa.

Siku kama ya leo miaka 464 iliyopita, alifariki dunia, Muhammad Mustafa Imadi, maarufu kwa jina la ‘Abus-Suud’, faqihi na mfasiri wa Qur’an Tukufu.

Abus-Suud alizaliwa karibu na mji wa Istanbul, magharibi mwa Uturuki na kuanza kujifunza masomo ya dini ya Kiislamu ambapo alipanda daraja na kuanza kufundisha. Mbali na msomi huyo wa Kiislamu kufahamu lugha ya Kituruki, alikuwa hodari pia katika lugha ya Kifarsi na Kiarabu ambapo aliweza hata kusoma mashairi kwa lugha hizo. Miongoni mwa athari za Abus-Suud ni pamoja na ‘Tafsir Abis-Suud’ ‘Dua Nameh’ ‘Qanun Nameh’ na ‘Mafruudhaat.

Siku kama ya leo miaka 157 iliyopita, Madam Escudo Doska ambaye baadaye alikuwa maarufu kwa jina la Marie Curie alizaliwa huko Warsaw mji mkuu wa Poland.

Baba yake alikuwa profesa wa fizikia na baadaye Madam Curie pia alielekea Paris, Ufaransa kwa ajili ya kuendeleza masomo yake katika taaluma hiyo hiyo ya baba yake. Madam Curie alifunga ndoa na Pierre Curie mwanafikizikia wa Ufaransa wakati alipokuwa masomoni katika Chuo Kikuu cha Sorbonne.

Hatimaye mwanamama huyo alifanikiwa kuvumbua mada ya radium baada ya utafiti miaka mingi.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa Madam Curie alitunukiwa tuzo ya Nobel mara mbili katika taaluma za fizikia na kemia na aliaga dunia mwaka 1934.

Madam Escudo Doska

Katika siku kama ya leo miaka 145 iliyopita, Leo Trotsky mmoja kati ya viongozi wakuu wa mapinduzi nchini Russia alizaliwa.

Alibaidishwa Siberia mara mbili katika zama za utawala wa Tsar kutokana na kujihusisha kwake na harakati za mapinduzi. Baada ya ushindi wa mapinduzi ya Russia, Trotsky alirejea nchini Russia. Hiyo ilikuwa mwaka 1917 na akapatiwa wadhifa wa Kamishna wa Masuala ya Kigeni. Mwaka mmoja baadaye akateuliwa kuwa Kamishna wa Vita ambapo baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani na Ujerumani wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, alianzisha mapambano dhidi ya wapinzani wa mapinduzi.

Hata hivyo baada ya kuaga dunia Lenin, mwanamapinduzi huyo alishindwa katika vita vyake na Joseph Stalin na mwaka 1925 alibaidishiwa Siberia na baadaye huko Uturuki. Hatimaye aliuawa mwaka 1940 huko Mexico na makachero wa Lenin.   

Leo Trotsky

Miaka 111 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Albert Camus mwandishi mashuhuri wa Ufaransa.

Licha ya kuwa familia yake ilikuwa masikini, lakini kutokana na kipaji, bidii pamoja na irada thabiti aliyokuwa nayo, Camus alifanikiwa kupata umashuhuri mkubwa. Mwandishi huyo wa Kifaransa ana vitabu vingi.

Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni The Firs Man, The Fall, The Stranger na A Happy Death. 

Albert Camus

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, ilianza kusikilizwa kesi ya Dakta Muhammad Musaddegh Waziri Mkuu wa wananchi wa Iran.

Miezi miwili kabla Musaddegh alikuwa ameondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Marekani na Uingereza. Kosa lake kubwa lilikuwa ni kuifanya sekta ya mafuta ya Iran kuwa mali ya taifa akisaidiwa na vikosi vya kidini na himaya ya wananchi.

Hatimaye kutokana na uzee, mahakama ya kijeshi ya Shah ilimhukumu Musaddegh miaka mitatu jela.

Dakta Muhammad Musaddegh

Na siku kama ya leo miaka 68 iliyopita vita vya mfereji wa Suez vilimalizika baada ya uingiliaji kati wa Umoja wa Mataifa.

Vita hivyo vilianza baada ya wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kushambulia jangwa la Sinai na kufuatia mashambulizi ya askari wa miavuli wa Uingereza na Ufaransa katika eneo la mfereji huo.

Serikali hizo tatu zilizotajwa zilianzisha vita hivyo kufuatia hatua ya rais wa wakati huo wa Misri, Jamal Abdulnassir, kuutaifisha mfereji huo.