Leo ni Alkhamisi tarehe 13 Rabiuthani 1446 Hijria sawa na tarehe 17 Oktoba 2024.
Siku kama ya leo miaka 1227 iliyopita yaani tarehe 13 Rabiuthani mwaka 219 Hijria aliaga dunia Ibn Hisham, msomi na mwanahistoria mkubwa wa Kiarabu.
Ibn Hisham alizaliwa Basra nchini Iraq na alibobea katika elimu ya fasihi na utungaji mashairi. Alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufanya uchunguzi kuhusu maisha ya Nabii Muhammad (saw).
Umashuhuri mkubwa wa Ibn Hisham unatokana na kitabu chake cha “al Sira al Nabawiyya” ambacho ni miongoni mwa marejeo muhimu kuhusu maisha ya Mtume Muhammad (saw).

Miaka 51 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi za Kiarabu zinazouza nje mafuta zilianza kutekeleza vikwazo vya mafuta dhidi ya Marekani, Uingereza na makampuni yanayouuzia mafuta utawala wa Kizayuni wa Israel.
Hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na uungaji mkono mkubwa wa Marekani na Uingereza kwa utawala ghasibu wa Israel katika vita vya Israel dhidi ya Syria na Misri. Hatua hiyo ilipandisha sana bei ya mafuta katika masoko ya kimataifa na kutoa pigo kubwa kwa nchi hizo za Magharibi. Muda mfupi baadaye nchi za Kiarabu zilikiuka vikwazo hivyo vya mafuta na kuanza tena kuiuzia mafuta Marekani na Uingereza.
Vikwazo hivyo vilionesha kuwa nchi za Kiislamu zina silaha muhimu inayoweza kutumiwa dhidi ya uungaji mkono mkubwa wa nchi za Magharibi kwa utawala katili wa Israel.

Miaka 41 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia mtaalamu wa masuala ya jamii wa Kifaransa kwa jina la Raymond Aron.
Aron alizaliwa mwaka 1905. Msomi huyo wa Kifaransa alikuwa akifundisha pia taaluma hiyo ya masuala ya jamii katika Chuo Kikuu cha Sorbonne, Paris kwa miaka kadhaa. Vile vile alikuwa akiandika makala katika majarida ya Le Figaro na Express mjini Paris. Raymond Aron ameandika vitabu vingi.

Na leo tarehe 17 Oktoba ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Umasikini Duniani.
Umoja wa Mataifa uliainisha siku hii katika kuhamasisha jamii na serikali kupambana na umaskini. Mwaka 1992 Umoja wa Mataifa uliitangaza siku hii kuwa “Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Umaskini.”
Tangu wakati huo, juhudi zinafanyika kuhakikisha kuwa, kila mwanadamu anapata mahitaji muhimu ya kimaisha ikiwa ni pamoja na chakula, makazi, mavazi na huduma muhimu za kijamii na tiba. Hata hivyo wakati dunia ikiadhimisha siku ya kung’oa mizizi ya umaskini, idadi kubwa ya watu bado wanaishi katika umasikini wa kupindukia na wanashindwa kukidhi mahitaji yao ya kila siku, wengi wakiwa ni kutoka katika nchi za ulimwengu wa tatu.
