Leo ni Alkhamisi tarehe 8 Rabiul Awwal 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 12 Septemba 2024.
Siku kama ya leo miaka 1,188 iliyopita aliuawa shahidi Imam Hassan Askari (as) ambaye ni mmoja wa wajukuu wa Mtume wetu Muhamamd (saw) katika mji wa Samarra nchini Iraq.
Imam Askari alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina mwaka 232 Hijria na alishika hatamu za kuongoza Umma baada ya kuuawa baba yake mwema Imam Ali al Hadi (as). Kipindi cha uongozi wa Imam Hassan Askari kilijawa na misukosuko mingi kutokana na kuzaliwa ndani yake Imam wa Zama Mahdi (as). Kwani viongozi wa utawala wa kizazi cha Abbas walikuwa wakichunga mno na kumsaka Imam huyo aliyeahidiwa kudhihiri katika aheri zamani.
Alisifika kwa elimu, ukarimu na ucha-Mungu. Imam aliuawa shahidi na watawala madhalimu wa Bani Abbas kwa kupewa sumu katika siku kama hii leo.

Miaka 127 iliyopita, inayosadifiana na 12 Septemba 1897, Irene Joliot- Curie mtaalamu wa fizikia na kemia wa Ufaransa, alizaliwa katika mji wa Paris.
Baada ya kufanya utafiti wa muda mrefu, Irene Joliot- Curie alifanikiwa kuvumbua mada za nunurishi au radioactive. Baadaye akishirikiana na mmoja wa wasaidizi wa mama yake, mwanafizikia huyo alifanya utafiti na uhakiki katika uga huo na kupata mafanikio makubwa. Irene Joliot-Curie aliaga dunia 1957.

Katika siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, nchini Ethiopia kulitokea mapinduzi yaliyopelekea kuondolewa madarakani utawala wa Haile Selassie.
Haile Selassie alizaliwa mwaka 1892 nchini Ethiopia. Awali alikuwa mkuu wa mikoa kadhaa nchini humo na baadaye akawa mrithi wa kiti cha ufalme. Mwaka 1930 alishika hatamu za uongozi wa Ethiopia akiwa mfalme wa nchi hiyo. Awali alifanya jitihada kubwa za kuyaunganisha makabila ya Ethiopia kwa shabaha ya kuyadhibiti.
Haile Selassie aliwaajiri wataalamu wa kigeni na kuanza kufanya marekebisho ya kiidara hatua kwa hatua. Alikomesha utumwa, akafanya marekebisho ya masuala ya kifedha na kuanzisha mfumo wa mahakama nchini Ethiopia.
Hata hivyo mashambulio ya Italia dhidi ya Ethiopia mwaka 1935 yalisitisha mpango wake huo na alibakia nje ya nchi hadi mwaka 1941 aliporejea nchini kwa msaada wa Waingereza na kutwaa tena madaraka. Aliendeleza marekebisho yake ambayo zaidi yalijikita katika mji mkuu Addis Ababa na mambo yasio ya msingi huku sehemu kubwa ya Waethiopia wakikosa suhula za kimsingi za maisha. Selassie alikuwa tegemeza sana kwa nchi za Magharibi.
Tarehe 12 Septemba mwaka 1974 Selassie aliondolewa madarakati katika mapinduzi yaliyofanywa na wanajeshi wa nchi hiyo na mwaka mmoja baadaye utawala wa kifalme ulikomeshwa kabisa nchini Ethiopia.

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 12 Septemba 1977, alifariki dunia Steve Biko mwanaharakati wa kupigania haki za wazalendo wa Afrika Kusini, akiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Steve Biko alikuwa kiongozi wa wanafunzi aliyefanya jitihada kubwa za kuwawezesha wazalendo waliokuwa wakibaguliwa wa Afrika Kusini na kuratibu harakati zao.
Baada ya kufariki dunia akiwa mikononi mwa polisi, Biko alitambuliwa kuwa shahidi wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi. Alikuwa mashuhuri kwa kaulimbiu ya “Weusi ni Uzuri” (black is beautiful) ambayo ililenga kuwapa moyo wazalendo wa Afrika Kusini waliokuwa wakibaguliwa kwa sababu ya rangi ya ngozi yao.

Na siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, nchini Uturuki kulitokea mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Jenerali Kenan Evren na kupelekea kuondolewa madarakani Waziri Mkuu Suleyman Demirel na kisha kuundwa serikali ya kijeshi.
Kuibuka kashfa ya ufisadi wa fedha na kuendelea hali ya kulegalega kisiasa na kijamii nchini Uturuki kulipelekea kutokea mgogoro wa kiuchumi ambapo hatimaye katika siku kama ya leo Jenerali Kenan aliyekuwa mkuu wa majeshi alifanya mapinduzi.
Baada ya mapinduzi hayo, Jenerali Kenan akiwa pamoja na Baraza la watu sita walishika hatamu za uongozi wa nchi.
Mbali na Waziri Mkuu kuondolewa madarakani kulitolewa amri pia ya kuvunjwa Bunge sambamba na kupigwa marufuku shughuli za vyama vya siasa na nchi ikawa inatawaliwa na serikali ya kijeshi.
