Aliyeua mwizi wa ng’ombe ahukumiwa kifo

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Iringa, imemuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, Elias Ngaile, baada ya kumkuta na hatia ya kumuua Luka Mang’wata kwa kumkata na panga akimtuhumu kumuibia ng’ombe.

Tukio hilo lilitokea Mei 21, 2024 katika Kijiji cha Lundamatwe, Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa ambapo siku ya tukio, Elias akiwa na wenzake walienda kijiji alichokuwa akiishi Luka na kumvamia kwa mapanga kwa madai kuwa ameiba ng’ombe kijijini kwa baba yake.

Hukumu hiyo imetolewa Machi 7, 2025 na Jaji Angaza Mwipopo aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ya mauaji na nakala ya hukumu hiyo kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Jaji Mwipopo amesema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo, Mahakama imejiridhisha kuwa upande wa mashitaka umethibitisha kosa dhidi ya Elias na kumuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Ilivyokuwa

Katika kesi hiyo upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi wanne na vielelezo viwili ambapo shahidi wa kwanza Michael Madenge, alisema siku ya tukio saa 10 jioni marehemu alikuwa akinywa naye pombe ya kienyeji na watu wengine.

Shahidi wa pili ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kibati kilichopo Kijiji cha Lundamatwe, Bakari Kabogo, alisema alipokea simu kutoka kwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Lundamatwe, Ibrahim Nsemo, akiulizwa iwapo anamfahamu Luka Mang’wata.

Alipojibu anamfahamu alijulishwa kuwa ana mgeni wake (mshtakiwa) ambaye alimuomba akutane naye pamoja na Luka katika kilabu nyingine ya pombe ya kienyeji ambayo ilikuwa karibu na alipokuwa anaishi Luka.

Shahidi huyo alisema alikwenda kwenye kilabu hiyo iliyokuwa inamilikiwa na Daniel Kahiwanga kukutana na mgeni huyo.

Alidai baada ya kufika hapo alimkuta Zakaria Wilagila, Ben Nzigilwa, Festo Nzigilwa, na Elias (mshtakiwa) na  kila mmoja alikuwa ameshika panga na alipouliza ni nani aliyepiga simu, Elias akajibu kuwa ndiye aliyepiga na kusema Luka alikuwa ameiba  ng’ombe wake.

Shahidi huyo alisema Elias alikuwa akimtaka Luka, ambapo aliwataka wasubiri aite Polisi na kabla hajafanya hivyo, Luka alitoka ndani ya kilabu hiyo akakimbia, Elias na wenzake wakamfuata.

Shahidi huyo alisema naye aliamua kuwafuata na kuwa akiwa umbali wa karibu hatua 40 kutoka kilabu ya eneo hilo, alimuona Elias akimkata Luka panga la kisogoni na mkononi, Luka akaanguka chini.

Alisema alimtaka Elias asiendelee kumshambulia Luka ila Elias aligoma na kumpiga na ubapa wa panga katika shavu la kushoto, hivyo kulazimika kukimbilia kwenye shamba la mahindi.

Alisema akiwa huko alikutana na shahidi wa kwanza, Martin Madenge ambapo alimtaka asiende huko mbele kwani hakukuwa salama.

Shahidi huyo wa pili alisema aliamua kukimbia na kupanda juu ya mti ambapo akiwa juu ya mti alishuhudia Elias akimshambulia Luka kwa kumkata na panga miguuni na kuona watu wakikusanyika katika eneo hilo, ambapo Elias na wenzake walikimbia.

Alisema alishuka kutoka juu ya mti na kupiga kelele zaidi ambapo wanakijiji wengine walikusanyika na wakati maofisa wa Polisi wanafika eneo hilo Luka alikuwa haongei na alikuwa akivuja damu nyingi.

Shahidi wa tatu Dk Beno Ndomba wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, aliyeufanyia mwili huo uchunguzi alisema marehemu alikuwa na majeraha kichwani na miguuni yaliyosababishwa na kitu chenye ncha kali  na chanzo za kifo chake ni kupoteza damu nyingi.

Katika utetezi wake, mshtakiwa huyo alisema anaishi katika  Kijiji cha Ndiwili na baba yake alikuwa anaishi Kijiji cha Isoliwaya, mkoani Iringa.

Alisema akiwa katika Kijiji cha Isoliwaya anakoishi baba yake, usiku wa kuamkia Mei 18, mwaka huo ng’ombe wake wanne waliibiwa zizini na baada ya kugundua hilo alitoa taarifa kwa wanafamilia, wanakijiji na uongozi wa kijiji.

Alisema kuwa  Mwenyekiti wa Kijiji cha Isoliwaya alitoa barua ya utambulisho kwa mshtakiwa kwa lengo la kupata msaada kutoka kwa mamlaka.

Elias alisema aligundua kwato za ng’ombe kutoka kwenye zizi la baba yake zikielekea Kijiji cha Kitelewasi na alizifuatilia akisaidiwa na wanakijiji na kufika Kijiji cha Kitelewasi saa sita mchana.

Alifafanua katika Kijiji cha Kitelewasi, alifahamishwa kuwa Hussein na watu wengine watatu walipita kijijini wakiwa na ng’ombe, ambapo alipokamatwa Hussein alikiri kuiba ng’ombe na kuwataja watu sita waliomsaidia.

Mshtakiwa huyo alisema Hussein aliwaongoza na viongozi wa kijiji kuwakamata watu wengine watatu waliomsaidia kuiba ng’ombe hao katika vijiji tofauti usiku mmoja na mnunuzi wa ng’ombe hao wa wizi, Karisio Kalengela alikamatwa pia.

Alisema Mei 21, 2024 alirudi kituo cha polisi kuomba msaada wa kuwakamata wezi wengine waliotajwa na Hussein ambapo alikwenda Kijiji cha Lundamatwe na kutoa taarifa kwa ofisa mtendaji wa kijiji hicho na kuomba msaada wa kuwakamata wezi hao akiwemo Luka.

Alieleza Mwenyekiti wa kitongoji alikataa kuwaonyesha Luka alipo na wanakijiji walimvamia mwenyekiti huyo wakidai anawasaidia wezi ambapo wakati huo Luka alikuwa amejifungia kwenye kilabu chaa pombe za kienyeji.

Alisema Luka alitoka kwenye kilabu akikimbia huku akiwa ameshika kisu na panga, akapita katikati ya kundi la wanakijiji waliokusanyika, na wanakijiji walimkimbiza ambao walimjeruhi.

Mshtakiwa huyo alisema kuwa wananchi hao walikuwa wakimuuliza Luka ng’ombe walioibiwa wapo wapi na Luka akasema wasimwue kwani ng’ombe walioibiwa watapatikana na kudai aliondoka eneo hilo kwenda kuwafuatilia.

Alisema Mei 23,2024 alipigiwa simu na polisi akitakiwa kuripoti polisi na alipoenda alituhumiwa kwa mauaji ya Luka, jambo ambalo alikana na kuwa kesi dhidi yake ni ya uongo.

Uamuzi wa Jaji

Katika hukumu hiyo Jaji Mwipopo alieleza katika kesi hiyo ya mauaji upande wa mashitaka una wajibu wa  kuthibitisha kuwa marehemu alikufa kifo kisicho cha kawaida, mshtakiwa anahusika na kifo cha marehemu, na alikusudia kusababisha kifo hicho.

“Licha ya tuhuma kuwa marehemu alikuwa mwizi wa ng’ombe, mwenendo na maneno aliyoyatamka mshtakiwa kabla, wakati na baada ya kumshambulia marehemu yalithibitisha kuwa alikusudia kumuua au kumsababishia madhara makubwa,” amesema Jaji.

Jaji Mwipopo amesema mtuhumiwa alikwenda kumkamata marehemu siku tatu baada ya kuwakamata Hussein akiwa na wenzake na walikuwa na mapanga. Alisema hakuwa na sababu ya kuwa na silaha hizo ili kumkamata marehemu.

“Ushahidi ulithibitisha bila shaka kuwa mtuhumiwa alimuua marehemu kwa makusudi, hivyo anatiwa hatiani kwa kosa la mauaji. Ninamuhukumu Elias adhabu ya kunyongwa hadi kufa,”alihitimisha Jaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *