Aliyeua mke na kukamatwa miaka minane baadaye, kunyongwa hadi kufa

Arusha. Mahakama ya Rufani nchini imebariki adhabu ya kunyongwa hadi kufa aliyohukumiwa mkazi wa Kijiji cha Kiongera kilichopo Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Nyamhanga Joseph, baada ya kukutwa na hatia ya kumuua mkewe, Rhobi Nyamhanga.

Upande wa mashitaka ulieleza kuwa Nyamhanga alitenda kosa hilo Juni 9, 2008 kisha akatoroka, lakini alikamatwa Februari 15, 2016 miaka minane baadaye.

Ilielezwa kuwa siku ya tukio Nyamhanga aligombana na mkewe na kuanza kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake akitumia fimbo huku mkono wa kushoto akiwa ameshika panga alilokuwa akilitumia kumtishia yeyote aliyekuja kuamulia ugomvi huo.

Ilidaiwa dakika chache baadaye Rhobi alikutwa akiwa amelala karibu na Mto Kamachage akiwa hana fahamu, lakini mumewe na watoto wao wawili hawakuwepo. Rhobi alipofikishwa hospitalini alifariki dunia.

Nyamhanga alishtakiwa kwa kosa la mauaji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Tarime ambapo Hakimu aliongezewa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, baada ya kusikiliza ushahidi na hoja za pande zote mbili, Mahakama hiyo ilimuhukumu Nyamhanga adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Kutokana na kutoridhika na adhabu hiyo, Nyamhanga alikata rufaa, Mahakama ya Rufaa ambayo ilikaa katika kikao chake Musoma, mbele ya majaji watatu ambao ni Jaji Barke Sehel, Lucia Kairo na Amour Khamis.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa Februari 28, 2025, majaji hao walieleza kuwa baada ya kupitia mwenendo wa shauri hilo, wamebaini upande wa mashitaka ulithibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka na kutupilia mbali rufaa hiyo kwa kukosa mashiko.

Jaji Sehel amesema mrufani hakupinga kuwa alikuwa mtu wa mwisho kuonekana akiwa na marehemu huku akiwa ameshika panga.

Amesema sheria iliamuliwa kuwa iwapo mtuhumiwa anadaiwa kuwa mtu wa mwisho kuonekana akiwa na marehemu, bila ya kuwepo maelezo ya kutosha ya kueleza sababu zilizzosababisha kifo hicho, atadhaniwa kuwa ndiye muuaji.

“Mrufani alijitetea, lakini kama ilivyochambuliwa hapo juu, upande wa utetezi haukutilia shaka kesi ya mashitaka. Katika suala hilo, tumejiridhisha kuwa, mrufani ndiye aliyemkata marehemu shingoni na kusababisha kifo chake,” amesema Jaji Sehel.

Jaji huyo amesema mwenendo wa mrufani kutoroka baada ya kutenda kosa hilo unaonyesha hatia yake, hivyo wanatupilia mbali rufaa hiyo.

Ilivyokuwa

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi wanne na vielelezo viwili.

Shahidi wa pili ambaye ni jirani wa wanandoa hao, Kasanya Magabe,, alisema  siku ya tukio akiwa anafanya kazi katika shamba lake la mihongo alisikia sauti ya ugomvi kutoka njiani alipokwenda kuangalia kuna nini alikuta wanandoa hao wakigombana.

Alisema alimuona mshtakiwa akimpiga marehemu sehemu mbalimbali za mwili kwa kutumia fimbo kubwa kwenye mkono wake wa kulia, huku akiwa ameshika panga kwenye mkono wake wa kushoto.

Alisema marehemu aliyekuwa akisukuma baiskeli alikuwa akilia kuomba msaada, akisema nisaidie, lakini alipojaribu kuzuia mrufani asimpige marehemu, mrufani aliinua panga na kutishia kumkata, kwa hofu akawaacha.

Shahidi huyo alisema kuwa dakika 25 baadaye alipowafuata tena, alimkuta Rhobi amelala karibu na Mto Kamachage akiwa hana fahamu huku akimuona mrufani akiwa na watoto wao wawili akielekea nyumbani kwao.

Alieleza kuwa alipiga kelele kuomba msaada miongoni mwa waliojitokeza ni pamoja na  mama wa mshitakiwa, Meng’anyi Chango, ambaye baada ya tukio hilo alienda kwa mwenyekiti wa kijiji na kuripoti kuwa mtoto wake alimpiga mkewe na kumjeruhi vibaya.

Ilielezwa mwili wa marehemu ulikutwa na umejaa majeraha na jeraha kubwa la kukatwa shingoni hadi kuning’inia ambapo daktari aliyemfanyia uchunguzi alieleza kuwa, marehemu alikutwa na alama na kuashiria kuwa alipigwa na kitu butu na chanzo cha kifo hicho ni kupoteza damu nyingi.

Mrufani alitoroka hadi alipokamatwa Februari 15, 2026 mkoani Mwanza.

Katika utetezi wake, mrufani huyo alikana kutenda kosa hilo na kueleza  siku ya tukio hakuwepo eneo na alirejea katika maziko ya mkewe Mei 6, 2008 kisha akarudi Dar es Salaam na kuendelea na shughuli zake za kawaida.

Mahakama ilimkuta mrufani huyo na hatia na hivyo kumtia hatiani na kumuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Katika rufaa hiyo mrufani huyo aliwakilishwa na Wakili Daud Mahemba, huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili Grace Madikenya.

Mrufani alikuwa na  sababu nne baadhi ni Mahakama kushindwa kuchambua na kuzingatia ushahidi wa upande wa utetezi na  kushindwa kuthibitisha kesi pasi na kuacha mashaka.