
Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, imemuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, Haridi Ntamoye, baada ya kumkuta na hatia ya kumuua mke pamoja na mtoto wake kisha kuwafukia kwenye shimo shambani kwao.
Miili ya Ashura Moshi (mke) pamoja na mtoto wao, Alibika Khalid, iligunduliwa shambani humo ikiwa imeanza kuharibika.
Hukumu hiyo imetolewa jana Machi 10, 2025 na Jaji John Nkwabi, aliyesema baada ya kupitia hoja za pande mbili, Mahakama imejiridhisha kuwa upande wa mashitaka umethibitisha kosa la mauaji pasipo kuacha shaka.
Awali, miili hiyo ilipatikana shambani kwa mtuhumiwa ikiwa imeanza kuoza ambapo alikamatwa akihusishwa na tukio hilo.
Kabla hajakamatwa mshtakiwa huyo alitoa taarifa kwa kiongozi wa kitongoji kuhusu kupotea kwa mkewe na mtoto wao Agosti 27, 2023 alipoenda kutafuta maharage kwa ajili ya kupika.
Kiongozi huyo alimshauri kuendelea kufuatilia huku akifuata maagizo ya polisi, walipanga makundi ya wanakijiji wa Nengo kwa ajili ya msako wa watu hao katika maeneo tofauti.
Ilidaiwa baada ya kufanyika upekuzi wa kina, kuligunduliwa eneo lililotiliwa shaka karibu na nyumba ya mshitakiwa huyo (shambani).
Eneo hilo lilipochimbwa kwa kutumia jembe, mkono wa binadamu ulijitokeza ndipo walilazimika kutoa taarifa polisi ambao waliambatana na madaktari wawili.
Ilidaiwa baada ya kuwasili, shughuli ya ufukuaji wa miili hiyo ilianza ambapo baadaye ilitambuliwa ni ya Ashura na Alikiba.
Haridi alishtakiwa kwa makosa ya mauaji ambapo alidaiwa kwa tarehe zisizojulikana kati ya Agosti 28 hadi Septemba 2, 2023 katika eneo la Kumkenga katika Kijiji cha Nengo wilayani Kibondo mkoani Kigoma, aliwaua mkewe na mtoto wao.
Katika kesi hiyo upande wa mashitaka uliwakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Nestiry Kuyula, huku mshtakiwa huyo akiwakilishwa na Wakili Elinisadi Msuya.
Katika kuthibitisha kesi hiyo, upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi 12 pamoja na vielelezo sita.
Ushahidi wa shahidi wa sita na saba, Dk Doreen Mushobozi na Dk Allen John, walidai marehemu hao walikufa kifo kisichokuwa cha kawaida na kuwa Ashura alipata jeraha kubwa kwenye ubongo lililosababishwa na kupigwa na kitu kizito chenye ncha kali.
Kuhusu Alikiba, ilidaiwa chanzo cha kifo chake ni upungufu wa oksijeni kwenye ubongo uliosababishwa na kukabwa koo.
Akijitetea mahakamani hapo mshtakiwa huyo alikiri Ashura alikuwa mke wake na Alikiba alikuwa mtoto wake na kuwa ni kweli miili yao imekutwa ikiwa imezikwa shambani kwake, lakini marehemu hao walikuwa wamevamiwa.
Katika hukumu hiyo Jaji Nkwabi amesema masuala yatakayoamuliwa na Mahakama hiyo ni iwapo mshtakiwa ndiye aliyewaua watu hao na kama alikuwa na nia mbaya ya kuwaua.
Jaji amesema kuhusu suala la iwapo mtuhumiwa ndiye aliwaua marehemu hao, kuna ushahidi wa upande wa mashitaka kuhusu maelezo ya ziada ya Mahakama na kile kinachoonekana kuwa kukiri kwa mdomo kwa mtuhumiwa kwa viongozi wa mitaa na wananchi wengine.
Amesema shahidi wa nane, Haman Kayandabila, mlinzi wa amani alirekodi maelezo ya ungamo ya mtuhumiwa huyo ambapo alisema mshtakiwa huyo alieleza kuwa alikuwa wakala huru kutoa ungamo hilo kwani hakuwa chini ya nguvu wala tishio.
Jaji huyo amesema kauli hiyo inathibitishwa na ungamo la mdomo alilolitoa kwa viongozi wa eneo hilo na wananchi wengine aliposema, alizika mwili wa Alikiba chini ya mwili wa mama yake.
Jaji Nkwabi amesema kupatikana kwa miili hiyo miwili katika shamba la mshtakiwa kunaonyesha kwamba alikuwa na lengo la kuficha ushahidi.
Jaji amesema katika utetezi wa mshtakiwa alidai kulazimishwa na shemeji yake na wanakijiji, kukubaliana na chochote ambacho angeulizwa na polisi katika eneo ambalo miili ilipatikana na kuwa kesi dhidi yake ni ya kutungwa.
Jaji Nkwabi amesema kwa ushahidi uliopo kwenye upande wa mashitaka, haukubali utetezi wake ila katika kesi za jinai mshtakiwa hapaswi kutiwa hatiani kwa sababu ametoa utetezi dhaifu, bali ushahidi unaoongozwa na upande wa mashitaka unamtia hatiani.
“Baada ya kuzingatia ushahidi wote wa upande wa mashitaka na kuzingatia utetezi wa mshtakiwa, nimeridhika kwamba mshtakiwa aliwaua marehemu wote wawili, hivyo anatiwa hatiani kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu,”amesema Jaji.
Jaji Nkwabi amesema katika kosa la mauaji adhabu ni moja tu ya kunyongwa hadi kufa, hivyo kumuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa mujibu wa kifungu cha 197 cha Kanuni ya Adhabu.